MUNICH, UJERUMANI
KINDA wa miaka 16, Lamine Yamal, ameiongoza timu ya taifa ya Hispania kutinga fainali ya michuano ya Mataifa ya Ulaya akifunga bao lake la kwanza la michuano hiyo kwa staili ya aina yake wakati kikosi cha kocha Luis de la Fuente kikiibuka kutoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya Ufaransa ya Kylian Mbappe mjini Munich.
Katika mechi ya nusu fainali ya Euro 2024 iliyojaa ushindani ambayo Hispania ilianza vyema zaidi, ilishangazwa na bao la Randal Kolo Muani akiweka mpira wavuni kwa kichwa akimalizia krosi ya Mbappe katika dakika ya tisa tu.
Wahispania hawakubaki nyuma kwa muda mrefu, kwani Yamal alifunga bao ambalo bila ya shaka litaingia kuwania tuzo ya bao bora la michuano kutokea umbali ya yadi 25 dakika 12 baadaye. Na dakika nne baadaye, Dani Olmo akaweka chuma cha pili, bao ambao awali alipewa beki Jules Kounde, ambaye alijaribu kuuzuia mpira usiingie langoni akionekana kajifunga, hata hivyo baadaye UEFA ilibaini kwamba hata kama beki huyo wa Barcelona asingeugusa mpira huo ungeingia wavuni, hivyo akapewa mpigaji wa shuti, Olmo.
Habari ya mjini ilikuwa ni kinda wa Barcelona, Yamal ambaye aliwatia njaa Wafaransa na kushinda tuzo ya Nyota wa Mchezo.
Baada ya kufunga bao kali, Yamal alienda kwenye kioo cha kamera ya TV na kusema: “Sema tena.”
Kauli hiyo ilionekana kumlenga kiungo wa Ufaransa, Adrien Rabiot ambaye juzi alisema kwamba Lamine Yamal “anapaswa kufanya zaidi ya aliyofanya kufikia sasa. Kwa sababu atashindwa kufanya chochote katika mechi kubwa (ya nusu fainali) ya mashindano makubwa.”
Noma ni kwamba katika mechi ya jana, Yamal alimtumia huyo huyo Rabiot kuwa kama ngao mbele yake wakati anapiga shuti la mkunjo wa ndizi lililomshinda kipa Mike Maignan.
Bao hilo limemfanya Yamal kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kufunga bao katika michuano ya Euro. Hata hivyo, hilo ni bao lake la mwisho akiwa na umri wa miaka 16, kwasababu Jumamosi atatimiza umri wa miaka 17, ikiwa ni siku moja kabla ya mechi yao ya fainali itakayoikutanisha Hispania dhidi ya mshindi kati ya England na Uholanzi, ambazo zitakutana katika nusu fainali leo usiku.
HAKUANZA JANA
Halafu unaambiwa, Yamal hakuanza jana kuwadhuru, Ufaransa.
Kinda huyo aliifunga Ufaransa bonge la bao lililofanana na lile la jana, mwaka jana katika mechi ya nusu fainali ya Michuano ya Mataifa ya Ulaya (Euro U-17), wakati huo akiwa na umri wa miaka 15 ambayo hata hivyo Hispania ililala 1-3 siku hiyo.