Morogoro. Baada ya kuvunjika kwa daraja jirani na Shule ya Msingi Kilakala katika Manispaa ya Morogoro, ambayo inahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalumu, usalama wa wanafunzi hao kwa sasa ni mdogo hasa wanapovuka kupitia daraja hilo.
Wakati mwingine wanafunzi hao wanalazimika kuvuka kupitia korongo lenye maji kwa kupita juu ya mti uliovunjika ili kwenda upande wa pili.
Akizungumza na Mwananchi leo, Julai 11, 2024, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kilakala, Gabriel Ngondo, amesema ni zaidi ya miezi mitatu sasa tangu daraja hilo lililokuwa linaunganisha shule na makazi ya watu limevunjika.
Hofu yao kubwa ni usalama wa wanafunzi, kwani wakati wa masika, eneo hilo linajaa maji mengi, hivyo wanafunzi wanaweza kupata madhara.
“Tangu daraja hili kuvunjika, ni zaidi ya miezi mitatu sasa, inatulazimu kuvuka kupitia kwenye korongo lenye maji. Kama mnavyojua, wakati wa masika mvua zinakuwa nyingi sana, hivyo maji yanayopita hapa ni mengi. Hofu yangu kubwa ni hawa watoto wanaovuka hapa, kwani daraja hili lisipotengenezwa mapema litatusababishia matatizo mengine,” amesema Ngondo.
Ameongeza kuwa tayari wameshatoa taarifa kwa Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura) na kujibiwa kwa barua inayomtaka kwenda kuchukua mataruma ya reli ambayo yanagharimu Sh500,000.
Hata hivyo, kwa sasa hakuna fedha hizo, hivyo amepeleka barua hiyo katika ofisi ya kata ambapo ametakiwa kusubiri hadi pale fedha zitakapopatikana.
Mwanaidi Sadick, mkazi wa Kilakala, amesema wanafunzi wa eneo hilo wanapata wakati mgumu kuvuka eneo hilo, kwani wanalazimika kukanyaga maji na wakati mwingine wanateleza na kuangukia mawe yaliyopo katika korongo hilo.
Ameomba Serikali kuchukua hatua za haraka kutekeleza ujenzi wa daraja katika eneo hilo.
“Kwanza wanafunzi wanateseka, kivuko hakuna, wanalazimika kukanyaga maji na wakati mwingine wanateleza na kudondokea mawe. Wapo wanaopata majeraha kila kukicha, mimi kama mzazi sipendi kuona hivyo. Najua Serikali inatusikia, watusaidie angalau tupate daraja, hawa watoto wapite hapa kwa amani,” amesema Sadick.
Mkazi wa Kilakala, Anita James, ameongeza kuwa si wanafunzi pekee wanaokabiliwa na adha hiyo, bali pia wananchi wote wanaovuka katika eneo hilo kwani wote wanalazimika kukanyaga maji na wakati mwingine kuvuka hapo wakienda kazini. Amewasilisha ombi kwa Serikali kuchukua jitihada za haraka kurekebisha daraja hilo ili kuepusha madhara zaidi.
Kaimu Meneja wa Tarura Wilaya ya Morogoro, Wambura Waitara amesema wamepokea malalamiko ya daraja hilo na tayari wamefanya tathmini ya gharama inayohitajika. Kwa sasa wanachosubiri ni kuletewa fedha hizo kwa ajili ya utekelezaji.
“Tulipokea malalamiko ya daraja hilo na tayari tumeshafanya tathmini ya gharama inayohitajika. Tunachosubiri kwa sasa ni kukabidhiwa fedha hizo kwa ajili ya utekelezaji,” amesema Waitara.