Singida. Watu 28 wamejeruhiwa katika ajali baada ya basi la kampuni ya Zube Trans lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza kupinduka.
Ajali hiyo imetokea leo Julai 11, 2024 asubuhi katika eneo la Njirii, Itigi mkoani Singida.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Dk Furaha Mwakafwila amesema wamepokea majeruhi 28, kati yao wanawake ni 15 na wanaume 13 huku wanne kati yao wakipewa rufaa kwenda Hospitali ya Mtakatifu Gasper Itigi.
Dk Mwakafwila amesema majeruhi wanaendelea na matibabu.
Wakizungumzia ajali hiyo, baadhi ya mashuhuda wamesema basi hilo lilianguka baada ya kugongwa ubavuni na lori walilokuwa wakipishana nalo na wamempongeza dereva wa basi hilo kwa namna alivyolimudu basi hilo na kutosababisha madhara makubwa.
Deogratius Senso, mmoja wa abiria kwenye basi hilo, amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori la mizigo walilopishana nalo kuligonga badi ubavuni na kusababisha liyumbe na hatimaye kuangukia ubavu.
Abiria mwingine, Masamba Erasto amemsifu dereva wa basi kuwa hadi linaanguka, amejitahidi kulidhibiti lisianguke vibaya na kusababisha madhara zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa singida hakupatikana mara moja kuzungumzia ajali hiyo, lakini Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemilembe Lwota amesema tayari wamefanya mawasiliano na ndugu wa majeruhi hao.
Amesema baada ya kutokea kwa ajali hiyo, Jeshi la Polisi na kambi ya jeshi ya Mkiwa, kwa kushirikiana na wananchi, walifika mapema na kutoa msaada kwa haraka, ambao pia umesaidia kutotokea kifo chochote.
Lwota amesema wanasubiri taarifa kutoka kwa wauguzi kuhusu majeruhi watakaoruhusiwa, ili wafanye utaratibu wa kuwawezesha kuendelea na safari yao.
“Hawa ni ndugu zetu, tutaendelea kuwahudumia hadi watakapokaa sawa huku tukiwaandalia utaratibu wa kuendelea na safari,” amesema.