Unguja. Licha ya Zanzibar kusifika kwa mazingira mazuri ya baharini, miamba ya matumbawe yenye uhai, na viumbe mbalimbali vya majini, kuna tishio la hali hiyo kutoweka kutokana na shughuli mbalimbali za binadamu, mabadiliko ya tabianchi, na uharibifu wa mazingira.
Hayo yameelezwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, alipozungumza kwenye jukwaa la uwekezaji wa visiwa vidogo Zanzibar, leo Alhamisi, Julai 11, 2024, kuwa rasilimali hizo za asilia si tu ni fahari kwa Taifa, bali pia ni sehemu muhimu ya uchumi, hasa kupitia utalii na uvuvi.
“Kwa hivyo, ni muhimu kwamba tuchukue hatua za pamoja ili kuhifadhi na kulinda rasilimali hizi muhimu,” amesema Dk. Mwinyi.
Ameipongeza Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa kujitolea kukuza uwekezaji endelevu unaoheshimu na kuhifadhi urithi wa asili na utamaduni wa visiwa vidogo.
Amesema dunia inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kwa kuwa Serikali imechukua hatua ya kimkakati ya kuvikodisha baadhi ya visiwa vidogo kwa wawekezaji watarajiwa wanaotaka kuwekeza fedha za hali ya juu na rafiki wa mazingira katika visiwa.
Amesema uamuzi wa kukodisha visiwa hivyo kwa uwekezaji wa muda mrefu ulikuwa wa kimkakati ambao ulisababisha kusajiliwa kwa miradi 16 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 384 za mtaji na kutarajiwa kutengeneza ajira zaidi ya 7,000 kwa wenyeji.
“Ninayo furaha kukutaarifu kwamba, baadhi ya miradi hii hivi karibuni itafunguliwa rasmi na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu,” amesema.
Amesema kongamano hilo litakuwa na mchango mkubwa katika kuwashauri wawekezaji na wale ambao wana shughuli zao za kila siku kuzunguka visiwani kuelewa umuhimu wa kuhifadhi na kulinda rasilimali hizi adhimu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi, na Uwekezaji, Shariff Ali Sharif, amesema uwekezaji unaenda vizuri na imewekwa mifumo kuhakikisha kuna uendelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA amesema ukodishaji wa visiwa unahusisha taasisi nyingi ikiwemo ZIPA, watu wa mazingira, kamisheni ya utalii, na watu wa bahari, lengo likiwa ni kulinda na kuhakikisha haviwekezi zaidi ya asilimia 10 ya eneo na mkataba lazima uangalie kutunza mazingira.