Faili la Malisa latua Ofisi ya Mashtaka, asubiri kupelekwa mahakamani

Moshi. Mwanaharakati na Mkurugenzi wa GH Foundation, Godlisten Malisa ameendelea kuripoti katika Ofisi za Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kilimanjaro (RCO) kufuatia tuhuma tatu zinazomkabili huku akieleza kuwa, kwa sasa anasubiri kupelekwa mahakamani.

Malisa ameripoti Kituo Kikuu cha Polisi Moshi leo Julai 11, 2024 ikiwa ni mara ya tatu kufanya hivyo baada ya kupewa dhamana Juni 8, 2024.

Malisa alikamatwa Juni 6, 2024, muda mfupi baada ya kesi inayomkabili yeye na Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob kuahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kusafirishwa hadi Moshi mkoani Kilimanjaro.

Tuhuma zinazomkabili Malisa ni pamoja na kuchapisha taarifa za uchochezi kuhusu mauaji ya Beatrice Minja, mkazi wa Rombo anayedaiwa kuuawa na nyingine juu ya mwanafunzi anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa wilayani Moshi.

Tuhuma nyingine ni kutoa taarifa bila kibali kwenye akaunti yake ya Instagram kuhusu walimu waliokuwa wakisahihisha mitihani ya kidato cha nne, Januari 2024 kuhusu kutolipwa posho zao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, baada ya kuripoti kituoni hapo, Malisa amesema baada ya kufika kituoni ameambiwa tayari jalada limepelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, hivyo kwa anasubiri kupelekwa mahakamani.

“Nimefika polisi wameniambia wamekamilisha upelelezi na wameshafunga jalada na kulipeleka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, hivyo narudi Dar es salaam kwa sababu hatujui Ofisi ya Mashtaka itakamilisha lini kazi yao.

Akizungumzia jambo hilo, mmoja wa mawakili wake, Hekima Mwasipu ambaye ameongozana na Malisa kwenda kuripoti kituoni, amesema wametakiwa kuripoti kituoni hapo tena Julai 25, 2024.

“Jalada limeenda Ofisi ya Mashata ya Mashtaka ili kuandaa au kuangalia kama kuna kesi au hakuna kesi, hivyo kama kutakuwa kuna kesi watatupeleka mahakamani,” amesema.

“Hivyo, anatakiwa kuripoti Julai 25, 2024 kwa kuwa bado hawajajibiwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambako faili liko, lakini kama faili litakuwa limerudi kwa ajili ya kupelekwa mahakamani atapelekwa mahakamani,” amesema.

Related Posts