MABINGWA wa Kenya, Gor Mahia ‘K’Ogalo’ imeanza vibaya michuano ya Kombe la Kagame, baada ya kulambwa bao 1-0 na Red Arrows ya Zambia katika mechi ya Kundi B, uliopigwa jana usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.
Bao lililoizamisha K’Ogalo liliwekwa kimiani dakika ya 73 kupitia James Chamanga na kuwafanya mabingwa hao mara tano wa michuano hiyo iliyoanzishwa mwaka 1974 kwa mfumo wa sasa kuungana na timu nne zikiwamo wenyeji Singida Black Stars na JKU ya Zanzibar zilizoanza michuano hiyo kwa kipigo.
Singida ilichapwa 1-0 na APR ya Rwanda katika mechi ya Kundi C, huku JKU ikizimwa na Al Wadi ya Sudan Kusini pia kwa bao 1-0, huku Dejedaha ya Somalia ikilimwa pia 1-0 na Coast Union katika mechi za Kundi A, wakati ASAS ya Djibouti ilinyooshwa mabao 2-0 na Al Hilal ya Sudan.
Mechi moja pekee kati ya SC Villa na Al Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini ndio uliomalizika bila kuzalisha bao katika michezo yote ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo iliyorejea tena baada ya kusimama tangu mwaka 2021. Timu hizo zilitoka suluhu katika mechi ya Kundi C lenye timu za Singida na APR inayoongoza.
Katika mchezo wa K’Ogalo dhidi ya Wazambia timu zote zilionyesha kandanda safi, lakini hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika hakukuwa a maajabu kabla ya kipindi cha pili kushuhudiwa maafande hao wa Red Arrows ikipata bao hilo lililowafanya wavune pointi tatu na kushika nafasi ya pili nyuma ya Al Hilal.
Gor Mahia ilitwaa taji la mwisho la michuano hiyo mwaka 1985 likiwa ni la tano, baada ya awali kutwaa mawili enzi ikifahamika kama Luo Union na mengine matatu ikitumia jina hilo la sasa na ilicheza fainali za mwisho mwaka 2015 fainali zilipopigwas hapa Tanzania na kulala mbele ya Azam FC kwa mabao 2-0.
Timu hiyo itashuka uwanjani tena Jumamosi kuvaana na ASAS mechi itakayopigwa saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, baada ya awali Al Hilal kumalizana na Red Arrows saa 12 jioni ya siku hiyo.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea kesho Ijumaa kwa mechi nne, mapema saa 7 mchana wenyeji Coastal Union na JKU zitakwaruzana kwenye Uwanja wa KMC kabla ya saa 10 jioni kwenye uwanja huo huo Al Wadi kuvaana na Dekadaha, wakati saa 12 jioni itakuwa zamu ya SC Villa dhidi ya Singida na saa 3:00 usiku APR na Al Merrikh zitamazana mechi zote hizo mbili za mwisho zikipigwa Azam Complex.
Jumla ya timu 12 zilizopangwa katika makundi matatu zinachuana kuwania ubingwa wa michuano hiyo, huku Simba, Yanga na Azam zilizokuwa zishiriki kuchomoa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo muingiliano na ratiba ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano kwa mwaka 2024-2025.
Timu itakayomaliza kama kinara wa kundi na nyingine moja itakayomaliza kama mshindwa bora zitafuzu hatua ya mechi za nusu fainali itakayopuigwa Julai 19 na fainali za michuano hiyo itachezwa Julai 21.