Hakuna Mafuta, hakuna chakula – DW – 11.07.2024

Akiwa na umri wa miaka 75, Galiche Buwa ameishi na kushuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe, njaa na majanga ya asili, lakini mjane huyo wa Sudan Kusini, mama wa watoto wanne, mara zote alifanikiwa kupata riziki na maisha yalisonga, kutokana na biashara yake ya kuuza vyakula na mboga mboga.

Lakini sasa, hata biashara hiyo iko mashakani huku uchumi wa taifa hilo unaotegemea sana mafuta ukikabiliwa na hasara kubwa ya kupotea kwa mapato kufuatia kupasuka kwa bomba muhimu katika taifa jirani linalokabiliwa na vita la Sudan mnamo mwezi Februari mwaka huu.

Bomba hilo lililoharibika lilikuwa muhimu kwa usafirishaji wa mafuta ghafi ya Sudan Kusini katika nchi za nje, huku mauzo ya petroli yakichangia asilimia 90 ya pato jumla la taifa hilo linalokabiliwa na umasikini.

Soma pia:Mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini yaingia mkwamo

Athari zimekuwa nyingi, huku mfumuko wa bei ukiongezeka na thamani ya paundi ya Sudan Kusini ikiporomoka dhidi ya dola ya Marekani katika masoko ya fedha yasiyo rasmi, kutoka 21,000 Machi hadi 31,000 hivi leo.

Teddy Aweye, mama wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 28 alisema anapata shida kupata chakula, na hivyo kuilazimisha familia yake kula mlo mmoja kwa siku.

Maisha ni magumu Sudan Kusini

Ni kauli ya kawaida katika soko zima la mjini Juba ambako wafanyabiashara kadhaa waliliambia shirika la habari la AFP wanapata hasara kila siku.

Adulwahab Okwaki, muuzaji nyama mwenye umri wa miaka 61, alisema biashara yake iko kwenye matatizo. Mteja aliyekuwa akinunua kilo moja sasa ananunua nusu, aliyekuwa akinunua nusu sasa anachukua robo na aliyekuwa akichukua robo haji tena kununua nyama.

Baba huyo wa watoto wanane anapoteza fedha kwa kushindwa kuuza nyama kabla haijaharibika.

Sudan | Mwanamke akipolea chakula kutoka kwa afisa wa WFP
Afisa wa shirika la Mpango wa Chakula WFP akigawa chakula kwa mkaazi wa SudanPicha: World Relief via AP Photo/picture alliance

Wafanyabiashara wenzake wa kuuza nyama wamefunga biashara zao kwa sababu walishindwa kupata faida. Biashara kubwa kubwa pia zimeathiriwa.

Soma pia:UN yaongeza muda wa vikwazo vya silaha nchini Sudan Kusini

Harriet Gune, mjasiriamali mwenye umri wa miaka 27, alisema duka lake la nguo za fasheni ya kisasa lilikuwa linapoteza wateja. Alisema kadri unavyoongeza bei ya vitu dukani ndivyo unavyowatia hofu wateja wasije.

Jozi moja ya jeans iliyokuwa ikiuzwa paundi 25,000 za Sudan Kusini mnamo mwezi Machi, sasa inauzwa 35,000, akiongeza kusema kwamba alihitaji kuongeza bei ili aweze kupata fedha za kutosha kuagiza shehena nyingine ya bidhaa.

Maafisa wa serikali nao wanahali ngumu

Mnamo mwezi Mei waziri wa fedha Awow Daniel Chaung aliliambia bunge kwamba serikali ingesumbuka kuwalipa mishahara wabunge, wanajeshi, polisi wafanyakazi wa umma na maafisa wengine kwa sababu ya uhaba wa mapato.

Alisema nchi ilikuwa inapoteza asilimia 70 ya mapato ya mafuta kwa sababu ya kupasuka kwa bomba la mafuta, hali ambayo imeathiri mauzo ya mafuta nje ya nchi.

Sudan Kusini ilikuwa katika mgogoro hata kabla ya hatua ya bomba kufungwa kusababisha athari katika uchumi, huku kukiwa na hofu kwamba chaguzi zilizotarajiwa kwa muda mrefu zitacheleweshwa. Chaguzi hizo zimepangwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu.

Vurugu zauwa watu 38 El-Fashir Sudan

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Mbali na rushwa iliyokithiri inavyoyanyonya makasha ya serikali – huku watawala wakituhumiwa kwa wizi na uporaji – Sudan Kusini iko katika hatari kubwa ya sarafu yake kuyumba na kupoteza thamani, kwa sababu inaagiza karibu kila kitu kutoka nje, yakiwemo mazao ya kilimo.

Wachambuzi wanasema mapigano nchini Sudan kati ya jeshi la sertikali na kikosi cha wapiganaji wa Rapid Support Forces RSF tangu Aprili 2023, yamekoleza hali.

Soma pia:UN: Watu milioni saba wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula Sudan Kusini

Mgogoro huo umewaua maalfu ya watu na kuwalazimu wengine mamilioni kuyakimbia makazi yao – wakiwemo watu 700,000 waliokimbilia nchini Sudan Kusini – na kuisukuma Sudan kukaribia kutumbukia katika baa la njaa.

Mchumi na mshauri wa serikali Abraham Maliet Mamer ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, kwamba Sudan Kusini, ambayo ilitangaza uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011, ilihitaji kupanga mapema kuhakikisha mustakhbali wa taifa uko salama.

Alisema nchi inahangaika, wana fedha chache, huduma chache na usalama ni shida, na aliihimiza serikali ijenge vinu vya kusafishia mafuta na mabomba ya kusafirishia mafuta hayo kupitia nchi nyingine.

Alitahadharisha kwamba Sudan haitakuwa tena jinsi ilivyo na pasi na kutafuta njia mbadala, wataendelea kukabiliwa na changamoto.

 

Related Posts