JKT Tanzania imesema msimu huu inapambana kuhakikisha inachukua ubingwa wa Ligi Kuu ambao unatetewa na Yanga na kushiriki michuano ya kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Masau Bwire alisema kama klabu wamejipanga kubeba kila taji mbele yao ikiwemo la Ligi Kuu.
Masau alisema anaamini usajili bora waliofanya wa kuongeza baadhi ya wachezaji wapya na kurekebisha benchi la ufundi litafanya vizuri na kufikia malengo ya timu hiyo ya kubeba ubingwa.
“Tumesajili wachezaji ambao tunaamini watatusaidia na sisi tunakuwa na utaratibu wa kipekee kutambulisha na hata wale tunaowaaga tunamalizana nao kwa amani, tumewatangaza tuliowasajili tuliowaacha ukija uwanjani kama hujawaona ujue ndio basi tena,” alisema Bwire na kuongeza
“Hadi sasa tumesajili wachezaji tisa, John Bocco, Abdulrahim Seif kutoka Uhamiaji, Charles Ilamfya (Mtibwa Sugar), Kipa Denis Richard kutoka KMC, Karim Mfaume (Biashara United), Elisha Ramso (Twalipo), Wilson Nangu kutoka TMA na wengine wawili kutoka KVZ ya Zanzibar Hamis Salum na Kombo Hatibu, kuna wachezaji wawili pia wataongezeka bado tunakamilisha taratibu za usajili.”
Mbali na wachezaji na benchi la ufundi lakini pia wamefanya mabadiliko kwenye eneo la uongozi kwa timu zote mbili, JKT Tanzania na Queens.
“Kuna mabadiliko makubwa kwenye uongozi kuna waliobadilishwa na kuletwa wapya lengo kuwa na viongozi bora watakaotuvusha kwenye safari yetu ya mafanikio.”
JKT imemteua Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Kanali Godfrey Mvula akisaidiana na wajumbe wake Luteni Kanali Javan Japhet, Luteni Ramadhan Salum Mangapi, Meja Mohamed Ayubu.
Mtendaji Mkuu, Jemedari Said Kazumari, Waratibu kwa JKT Queens, Meja Ester Rioba na kwa upande wa JKT Tanzania Stan Joseph Chahe.
MKurugenzi wa ufundi kwa timu zote mbili na kwa vijana, Hamad Ally huku Mkurugenzi wa mashindano, Luteni Said, Idara ya fedha, Meja Innocent Ndunguru na masoko, Sepelatus Lubinga.