Paul Kagame ambaye kimsingi yeyote angeweza kusema ndiye amekuwa kiongozi wa Rwanda tangu kukoma kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, anapambana na upinzani kutoka kwa kiongozi wa chama cha Kijani Frank Habineza.
Habineza ndiye mgombea pekee wa chama cha upinzani aliyeidhinishwa kugombea mwaka huu. Mgombea mwingine ni Philipe Mpayimana anayewania nafasi ya Urais kama mgombea huru
Kagame mwenye miaka 66 anasifiwa kwa kuuinua uchumi wa Rwanda baada ya mauaji ya kimbari. Ukuaji wa pato la taifa hilo ulifikia wastani wa asilimia 7.2 kati ya mwaka 2012 na 2022. Licha ya hilo, utawala wake umekuwa ukikosolewa pakubwa kwa kuuminya upinzani ndani ya taifa lake.
Pia, ripoti ya Umoja wa Mataifa ya hivi karibuni imelituhumu jeshi la Rwanda kwa kushirikiana na waasi wa kundi la M23 linalofanya operesheni zake katika taifa jirani la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Soma pia:Kagame atetea rekodi ya Rwanda kuhusu demokrasia wakati wa kampeni
Rais Kagame alishinda chaguzi tatu zilizopita kwa kupata zaidi ya asilimia 93 ya kura mwaka 2003, 2010 na 2017. Katika uchunguzi wa maoni ya umma wa hivi karibuni kabisa, unaonesha Kagame anakubalika kwa asilimia 99. Mwaka 2017, mpinzani wake Habineza alipata asilimia 0.48 ya kura zote, Mpayimana kwa upande wake alipata asilimia 0.73 pekee.
Mapema mwaka huu mahakama za Rwanda zilizikataa rufaa za wanachama wa upinzani Bernard Ntaganda na Victoire Ingabire zilizolenga kuwaondolea hukumu zilizowahi kutolewa dhidi yao zilizowazuia kuwania urais.
Tume ya uchaguzi nayo ilimzuia mkosoaji mkubwa wa Kagame, Diane Rwigara kuwa mgombea. Hiyo ni mara ya pili kwa Rwigara kuzuiwa kugombea.
Diane ni mtoto wa mfanyabiashara mkubwa na aliyekuwa mfadhili mkuu wa chama cha Kagame cha Rwanda Patriotic Front RPF Assinapol Rwigara. Alituhumiwa kwa kughushi nyaraka na alikamatwa mwaka 2017 kabla ya kuachiliwa na mahakama mwaka mmoja baadaye.
Uwiano kati ya Rais Kagame na washindani wake
Katika uchaguzi huu wa rais utakaofanyika sambamba na wa bunge kwa mara ya kwanza, raia milioni 9.01 wa Rwanda wamejiandikisha kupiga kura.
Kutokuwepo kwa uwiano kati ya Kagame na wapinzani wake kumeonekana wazi katika kipindi cha wiki tatu za kampeni. Bendera kwenye magari na mabango kando ya barabara yakiwa na rangi nyekundu, nyeupe na bluu za chama tawala zImesambaa kila mahali.
Tofauti na maelfu ya watu kwenye mikusanyiko ya kampeni zake, wapinzani wake wamekuwa wakipambana kusikika huku wakijikongoja kufikisha walau watu 100 katika baadhi ya mikutano yao.
Bi Beatrice Mpawema mwenye miaka 30 ni mmoja wa wananchi waliohudhuria mkutano wa Frank Habineza katika kijiji cha Juru. Aliliambia shirika la habari la AFP kuwa, nanukuu ” nilikuja hapa kusikiliza anachokisema lakini nitampigia kura Kagame.
Soma pia:Pazia la kampeni za uchaguzi mkuu lafunguliwa Rwanda
Ametupa sauti sisi wanawake, ametengeneza barabara, amejenga hospitali na mambo mengi…nataka awe rais milele, hakuna wa kuchukua nafasi yake.” mwisho wa kunukuu.
Hata hivyo makundi ya haki za binadamu yamekuwa yakiituhumu serikali yake kwa ukiukaji ikiwemo kuminya uhuru wa kujieleza na upinzani.
Mapema wiki hii shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilisema kuwa wapinzani wa kisiasa nchini humo wanakabiliwa na vikwazo vikali pamoja na vitisho, kukamatwa kiholela, tuhuma zilizotengenezwa, mauaji na watu kutoweka.