MAGDALENA: Ondoeni hofu, medali ya Olimpiki ipo!

MWANARIADHA nyota wa Kimataifa wa Tanzania, Magdalena Shauri, ni miongoni mwa Watanzania wanne watakaoenda kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Paris, Ufaransa wakibeba mioyo ya wananchi zaidi ya milioni 60.

Magdalena anayetokea katika timu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ataungana na wenzake Jackline Sakilu, Alphonce Simbu na Gabriel Geay, kukata kiu yake ya kushiriki Olimpiki kwa mara ya kwanza baada ya kukosa nafasi hiyo mara kadhaa.

Alifuzu Olimpiki hii kupitia mbio za Berlin Marathoni zilizompa rekodi.

Magdalena mwenye umri wa miaka 28, ndiye bingwa wa marathoni kwa wanawake, rekodi ambayo aliiweka mwaka jana katika mbio za Berlin Marathon zilizofanyika Septemba 23, 2023, Ujerumani akimaliza wa tatu kwa muda wa saa 2:18:41.

Michezo ya Olimpiki 2024 itafanyika mwezi huu na Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Magdalena ambaye anakimbia mbio ndefu za kilometa 42 na hapa anaelezea namna gani amejipanga kufanya vyema.

Anasema amejiandaa vizuri na mashindano hayo na kwake kila kitu kinakwenda kama alivyopanga akiamini kilichobaki ni kufanyia marekebisho sehemu chache sana ili kwenda kufanya kweli.

“Nafanya mazoezi kwa kujiamini nikitarajia mbele naenda kufanya kitu, siyo naenda kutalii, yaani naen-da kufanya mambo makubwa na kubadilisha nchi iwe inayojulikana kwenye riadha.”

Anaweka wazi ana matumaini kibao kwani nafasi ya kushiriki Olimpiki imekuwa ikimponyoka mara kwa mara lakini mara hii ameipata, hivyo amedhamiria kufanya makubwa.

“Nina imani ya kufanya kweli, kikubwa tu Watanzania wawe na subra na wamwombe Mungu wala haitakiwi kuwa wepesi wa kukata tamaa, uhakika wa medali upo.”

Mwamko wa Tanzania katika michezo hasa wa riadha ndio inamfanya kuwa na jeuri kwa kuamini wote wanne ambao wanaenda Olimpiki wanaweza kufanya kweli kwani sapoti imekuwa kubwa kutoka kwa uongozi wa shirikisho hadi Serikali.

“Kwa sasa tumenyanyuka siyo kama miaka ya nyuma ambayo ilikuwa imedidimia, yani hapa miongoni mwa nchi ambazo pia zinaogopeka kwenye riadha na sisi tupo”.

Kuhusu wenzake, Magdalena anasema binafsi anaridhika na viwango vya wanariadha wenzake, Al-phonce Simbu, Gabriel Gaey na Jackline Sakilu ambao pia wataenda kushiriki Olimpiki na namna am-bavyo wanafanya mazoezini hana shaka watarudi na medali.

“Ninafurahishwa na upambanaji wao na tunashikana mikono na kocha wetu ambaye amekuwa ni msaada mkubwa sana kwetu, yote ni kuhakikisha tunaenda kuwawakilisha vyema mamilioni ya Watanza-nia”.

“Kocha wetu anapambana sana, ujue tunaenda zile njia ngumu ngumu, Olimpiki si ya kitoto na ukisha-kuwa ndio unaenda kuiwakilisha nchi lazima uhakikishe unapambana haswa”.

Magdalena anaweka wazi katika mbio ambazo hawezi kusahau ni za Berlin Marathoni ambazo ndizo zimemfanya sasa anaenda kushiriki mashindano ambayo kila mwana michezo anatamani kushiriki duniani kote.

“Kwangu inabaki ni kumbukumbu nzuri katika maisha ya riadha ukizingatia hakuna mtu ambaye ata-mani kushiriki Olimpiki, sasa unasahau vipi daraja ambalo limekuvusha hadi huko?”

Anasema ya zamani si ya sasa, mambo yamebadilika hivyo mashabiki na wadau wote wa michezo nchini wamtarajie Magdalena mpya na siyo yule ambaye wamemzoea  kwa sababu amejipanga kuweka na kuvunja rekodi zaidi iwe ambayo ameweka yeye au na mtu mwingine.

Anasema anaenda Olimpiki akiwa wa tofauti kabisa bila kuangalia rekodi yake ya taifa ya marathoni ambayo anashikilia na nguvu na akili vyote anaelekeza kwenye kushinda jambo ambalo ndiyo muhimu.

“Olimpiki siyo ishu ya muda, muda tunatafuta kwenye kufuzu na hii siyo ya kutafuta kufuzu hapa ni medali yani nafasi nzuri basi baada ya kushinda nitaunganisha na rekodi yangu.

“Yani hata ucheze saa ngapi sifa ni medali tu wala hakuna mtu atakuja kukusifia eti umekimbia muda mzuri hata siku moja sahau kitu kama hicho.”

Anasema kati ya mambo yanayomnyima usingizi ni la tangu Tanzania imeanza kushiriki Olimpiki haku-na hata mwanamke ambaye amepata medali yoyote, hivyo amekuwa akipambana usiku na mchana kwa kufanya mazoezi kwa bidii ili kuja kuwa sehemu ya historia.

“Kiu yangu kubwa nataka nishinde mashindano haya makubwa na kuweka rekodi ambayo itafanya dunia nzima initambue lakini pia kubadilisha pale palipoandikwa hakuna mwanamke ambaye amewahi kushinda medali Olimpiki kutoka Tanzania.”

Anasema moja kati ya mikakati aliyonayo ni pamoja na kuvunja rekodi ya marathoni ya dunia ambayo inashikiliwa na mwanariadha kutoka Ethiopia, Tigist Assefa kwa muda wa saa 2:11:53 kwani anafikiri ka-ma ataivunja basi aivunje na saa kama 2:10 au chini zaidi ya hapo.

Licha ya kwamba Olimpiki ya mwaka huu itakuwa na upinzani mkubwa sana kwani mastaa wakubwa na wenye uzoefu na mbio hizo nao watakuwepo huku yeye akiwa anashiriki kwa mara ya kwanza, lakini uwepo wao wala haumtishi na amejipanga kivyake kwenda kuiwakilisha Tanzania na hao nao wamejipan-ga kwenda kuwakilisha nchi zao hivyo watakutana na kuonyeshana umwamba nani mbabe zaidi.

“Ukifika kwenye sehemu ya matukio usiangalie huyu ni nani na nani yupo, mimi nilivyofanya mazoezi ina maana naenda kuwa mshindi, sasa nikianza kuangalia sijui fulani yupo nitakata tamaa.”

Related Posts