Dar es Salaam. Mchungaji wa Kanisa la Gospel Revival Center, Anthony Lusekelo, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako, amesema suala la waumini kutozwa fedha kwa ajili ya kufanyiwa maombi na viongozi wa makanisa ni makubaliano kwa sababu ni mambo ya imani.
Amesema maandiko ya Biblia yameelekeza waumini kwenda kanisani na sadaka, hivyo haipaswi kwenda mikono mitupu kwa sababu Mungu amewawezesha waumini kuwa matajiri.
Kauli ya Mzee wa Upako imekuja wakati kukiwa na mjadala kuhusu utozwaji wa ada hadi mamilioni kwa waumini kwa ajili ya kuwaombea, kufuatia habari za uchunguzi zinazochapishwa kwenye vyombo vya habari vya Mwananchi Communications Ltd.
Akizungumza katika mahojiano na Wasafi TV leo, Julai 11, 2024, Mzee wa Upako amesema, “Mambo ya imani ni makubaliano, ukitaka andiko nitakupa.
Ukienda kwa mtumishi usiende mikono mitupu. Mungu aliandaa watu kuwa matajiri, ukiwa masikini ni uzembe wako,” amesema Mzee wa Upako akinukuu maandiko, alipokuwa akijibu swali kwa nini makanisa yanauza bidhaa kama mafuta na maji kwa waumini.
“Nitawapeleka nchi ya maziwa na asali mtakayolima, mtalima shayiri, zabibu na ngano nchi ya shaba inayofuka chuma, mimi nitawabariki. Wewe kesho unakujaje kanisani bila sadaka?” amehoji.
Akiendelea kujenga hoja ya watu kutoa sadaka, Mzee wa Upako amesema Mungu aliwaambia wafalme kwamba wataongoza nchi kwa kodi.
“Akawaambia watu wa makanisa na ninyi mtaendesha makanisa kwa sadaka. Taratibu zinatumikaje, Mungu akaandika, ‘sadaka hii itakuwa kwa ajili ya wajane, sadaka hii itakuwa kwa ajili ya makuhani, wachungaji na maaskofu ili wasiende kufanya kazi kule,’” amesema.
Alipoulizwa kama mafuta ya upako yanaponya, Mzee wa Upako amesema amewahi kuona watu wakiponywa. “Nimewahi kuona mimi, si mara moja, si mara tatu, mafuta ya upako yanasaidia watu kupona mpaka kuwa matajiri. Ila sasa mafuta ya upako yanaanzia unapoishia wewe, lakini lazima uwajibike, upambane.”
Alipoulizwa sababu ya kuibuka makanisa ya maombezi na wingi wa viongozi wa makanisa hayo, Mzee wa Upako amesema kuna siasa kubwa kwenye makanisa. Hata hivyo, amesema ili mtu awe mchungaji ni lazima aandaliwe kwa muda mrefu.
“Haiwezekani mtu ukaamka asubuhi ukawa mchungaji. Lazima kwanza ukisikia wito, uende kwa askofu wako, unasema nasikia Mungu ameniita. Yule askofu atasema sawa na utaanza ushemasi, baadaye atakupeleka chuo kusoma miaka miwili mitatu, unarudi, unakaa pale, baadaye unafungulia tawi, (askofu) anasema utaenda Shinyanga au Mwanza. Akifika kule kunakuwa na maaskofu wawili watatu wamsimike.
“Hii ya kuibuka tu hapana. Lazima mtu atengenezwe kwanza, mchungaji amthibitishe. Kwa sababu inasema mtu akitaka uaskofu asiwe mchanga, uwe umekomaa, umekaa kanisani miaka 10 au 20, unasikia wito ndio unasikia Mungu amekuita.
“Lakini ukisikia mtu anazuka tu anasema mimi ni mchungaji, unamwacha kwa sababu kuna uhuru wa kuabudu lakini sio sawa,” amesema.