Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amemrejeshea nyumba Bi Leticia Benedict Choma mwenye umri wa zaidi ya miaka 80 mkazi wa Kigoma Ujiji baada ya kuihangaikia kwa zaidi ya miaka 10 bila mafanikio.
Bi. Leticia Choma anadaiwa kudhulumiwa nyumba aliyoachiwa na marehemu baba yake Bw. Benedict Choma iliyopo eneo la Mwanga barabara ya Bibi Titi Kigoma Ujiji kama urithi baada ya nyumba hiyo kuuzwa na msimamizi bandia wa mirathi asiyeidhinishwa na mahakama kwa madai ya kutokuwa na haki ya kumiliki nyumba hiyo licha ya wazazi wake kujenga na yeye kuzaliwa na kuishi hapo kwa miaka yote.
Kwa mujibu wa Bw. John Benedict Matata aliyemsimamia Bi. Leticia, mgogoro wa nyumba hiyo ulianza mwaka 2010 pale walipoanza kufuatilia kuhuisha hati ya nyumba hiyo Plot Na 212 Kitalu M mtaa wa Mwanga Kigoma Ujiji yenye namba ya usajili 13176 iliyokwisha muda wake mwaka 1989. kuisha kwa muda wa hati hakumkoseshi haki mmiliki ingawa Bi. Leticia amekuwa akizungushwa kwa miaka yote.
Amefafanua kuwa, pamoja na juhudi walizofanya ikiwemo kupita taasisi na mamlaka tofauti kutafuta kwa lengo la kutafuta haki lakini hawakuweza kufanikiwa hadi walipopata fursa ya kukutana na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda wakati wa ziara ya Makamu wa Rais mkoani Kigoma.
Ameeleza kuwa, katika kutafuta suluhu ya suala hilo Mhe Pinda aliwasikiliza kwa makini na baadaye kuitisha kikao cha pamoja kati ya Mwakilishi wa Kamishna wa Ardhi nchini, Msajili wa Hati na Nyaraka mkoa wa Kigoma pamoja na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa.
Bw. Matata ameweka wazi kuwa, kutokana na nyaraka walizokuwa nazo za umiliki wa nyumba yenye mgogoro na maelezo ya Bi. Leticia kuhusiana na sakata hilo pande zote zilikubaliana pasipo shaka kuwa, Bi Leticia Choma ndiye mmiliki halali wa nyumba hiyo.
“Baada ya kufuatilia kwa muda mrefu Mwenyezi Mungu amemleta kiongozi Mhe. Pinda, Mungu amzidishie maisha marefu ndiyo tumepata msaada huu leo kuja kumletea malalamiko na namshukuru sana Mheshimiwa’’ alisema Matata.
Kwa upande wake Mhe. Geophrey Pinda ameagiza Bibi Leticia Choma kutobughudhiwa na mtu yeyote baada ya kurejeshewa nyumba yake huku akimtaka Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kigoma kulisimamia suala hilo.
‘’Hakuna wa kuingilia tena kuleta shida, huyu bibi asibughudhiwe na wale wote wanaoendesha dhulma kama hii tutakufa nao’’ alisema Mhe. Pinda