Katibu Mtendaji wa PPAA James Sando akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na utendaji wa PPAA wakati alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji wa PPAA James Sando akipata maelezo Kwa watumishi wa PPAA wakati alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji wa PPAA James Sando akipata maelezo kutoka watumishi wa Benki ya TIB wakati alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
MAMLAKA ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imesema kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, Sheria hiyo imesaidia PPAA kuanzisha Moduli ya kuwasilisha Malalamiko na Rufaa kieletroniki, ambapo Moduli hiyo inapatikana katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma Kieletroniki (NeST).
Mafanikio hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando alipotembelea banda la PPAA katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Bw. Sando amesema mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, yamepelekea PPAA kuanzisha Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa zitokanazo na michakato ya zabuni kieletroniki. “PPAA kwa kushirikiana na PPRA tumeanzisha Moduli hiyo ambayo inapatikana katika mfumo wa NeST, ambapo moduli hiyo itasaidia kuokoa gharama na muda kwa wazabuni” alisema Bw. Sando
“Kuanzishwa kwa moduli hiyo kuna faida kadhaa ikiwa ni pamoja na kuokoa mud ana gharama kwa wazabuni,” aliongeza Bw. Sando
Pamoja na mambo mengine, Bw. Sando amesema Mamlaka hiyo ipo katika hatua za mwisho kukamilisha Kanuni za Ununuzi wa Umma za Uwasilishaji wa Rufaa za Zabuni za Umma za Mwaka 2024.
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Fedha iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi ya Umma Na. 3 ya mwaka 2001 ambapo baada ya Sheria hii kufutwa, Mamlaka ya Rufani iliendelezwa chini ya Sheria ya Ununuzi ya Umma Na. 21 ya mwaka 2004 na kuhuishwa tena kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 baada ya ile Sheria Na. 21 ya mwaka 2004 nayo kufutwa. Mwaka 2023 Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 nayo ilifutwa na Mamlaka ya Rufani ilihuishwa tena kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya mwaka 2023.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo, jukumu kuu la PPAA ni kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi ya malalamiko au rufaa zitokanazo na maamuzi ya Maafisa Masuuli wa taasisi mbalimbali za Umma katika michakato ya ununuzi wa Umma. Pia, ina jukumu la kupokea na kusikiliza malalamiko ya wazabuni ambao hawakuridhishwa na uamuzi wa kufungiwa (blacklist) na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).