Na Mwandishi Wetu
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana amesema kwa kazi kubwa ambayo imefanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo nchini ana uhakika katika uchaguzi mkuu mwaka 2025 atashinda kwa kura nyingi.
Aidha amesema kazi kubwa iliyofanywa na Chama Cha Mapinduzi katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ana uhakika katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani wagombea wa Chama hicho watashinda kwa kishindo.
Kinana ameyasema hayo leo Julai 11,2024 alipokuwa akifungua Kongamano la Maadili na Malezi lililoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi , ambapo amesema akitokea mtu akasema hakuna kilichofanyika chini ya uongozi wa CCM basi atakuwa hasemi ukweli.
“Tumeona maendeleo makubwa sana na Katavi imepiga hatua.Kazi ya CCM ni kutenda, kazi ya wenzetu wengine ni kusema kutenda ni kazi,kusema raisi, kujenga ni kazi kukosoa rahisi.Tuwaachie wao kazi ya kukosoa , na waendelee na kazi hiyo.
“Sina shaka hata kidogo Watanzania wana imani na wataendelea kuwa na imani kwa Chama Cha Mapinduzi.Tunauchaguzi mwaka huu wa Serikali za Mitaa , tutachaguliwa kwa kishindo na tuna uchaguzi mkuu mwaka ujao wa madiwani ,Wabunge nao nina hakika tutapata madiwani na Wabunge wengi.”