Nairobi. . Rais wa Kenya, Dk William Ruto, amewafuta kazi mawaziri wote katika Baraza la Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Justin Muturi, kutokana na maandamano yaliyoongozwa na vijana wa Gen-Z dhidi ya serikali yake.
Kwa mujibu wa tovuti ya Nation, ni Waziri Mkuu pekee, Musalia Mudavadi, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, amesalimika kwenye baraza hilo.
Uamuzi huo wa Rais Ruto umekuja baada ya kuwepo kwa mfululizo wa maandamano ya vijana wa Gen-Z, ambao wamekuwa wakidai kwamba kiongozi huyo amewasaliti kwa kutotimiza aliyowaahidi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
“Baada ya kutafakari, nikisikiliza kwa makini kile wananchi wa Kenya wamesema na baada ya tathmini ya kina ya utendaji kazi wa baraza langu la mawaziri na mafanikio na changamoto zake, kwa mamlaka niliyopewa na Kifungu cha 152(1) na 152 (5)(b) cha Katiba na Kifungu cha 12 cha Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, nimeamua kuwafuta kazi mara moja mawaziri wote wa Baraza la Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, isipokuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora,” amesema Rais Ruto kwenye televisheni.
Dk Ruto amesema atahusisha wadau wengine wa kisiasa katika shughuli ya kuunda upya baraza jipya la mawaziri. Wakati huohuo, Rais Ruto amesema shughuli za serikali zitaendelea chini ya uongozi wa makatibu wakuu na viongozi wengine husika.
Rais Ruto aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri Alhamisi asubuhi ili kutathmini maandamano ya vijana kote nchini ambayo yamesababisha vifo na uharibifu.
“Nitashiriki mara moja katika mashauriano ya kina katika sekta mbalimbali na mifumo ya kisiasa, kwa lengo la kuunda serikali pana ambayo itanisaidia katika kuharakisha utekelezaji wa lazima na wa haraka, wa programu za kukabiliana na mzigo wa madeni, kuongeza rasilimali za ndani, kupanua nafasi za ajira, kuondoa ubadhirifu na matumizi yasiyo ya lazima kwenye mashirika ya serikali. Pia kupambana na rushwa na kuifanya serikali ijiendeshe, iwe ya gharama nafuu, yenye ufanisi na thabiti,” ameongeza.
Jumanne iliyopita, Dk Ruto alitangaza “mpango mkubwa wa kisiasa” na kutoa uthibitisho kwa tetesi kwamba huenda anafikiria kukijumuisha chama cha Raila Odinga cha Orange Democratic Movement (ODM) katika utawala wake, ambao umetawaliwa na Kenya Kwanza.
Gazeti la Nation la Kenya limebaini kuwepo uwezekano wa Rais Ruto kuunda “Serikali ya Umoja wa Kitaifa” na viongozi wa upinzani katika utawala wake kama sehemu ya kujiondoa katika mzozo wa kisiasa uliopo, uliochochewa na vijana waliokuwa wakiandamana kumzonga na kutaka mtikisiko mkubwa kwenye serikali yake.
Haitakuwa mara ya kwanza kwa Kenya kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Rais wa tatu, Hayati Mwai Kibaki, aliposhindwa katika kura ya maoni mwaka 2005 katika kambi ya Hakuna iliyoongozwa na Waziri wake wa Ujenzi wakati huo, Raila Odinga, alijibu kwa kuvunja baraza lake lote la mawaziri.
Alipounda upya Baraza la Mawaziri, wiki mbili baadaye, Odinga na wanachama wake wa Liberal Democratic Party (LDP) waliachwa.
“Kufuatia matokeo ya kura ya maoni, imenilazimu mimi kama Rais wa Jamhuri kupanga upya serikali yangu ili kuifanya iwe na mshikamano na kuwahudumia vema watu wa Kenya,” Kibaki alilieleza taifa la Kenya.
“Nimeelekeza ofisi za mawaziri wote na mawaziri wasaidizi wote ziwe wazi. Kwa hivyo, waliokuwa wakishikilia nafasi hizo sasa wanakoma kushikilia ofisi hizo mara moja,” amesema.