SIMBA imeingia siku ya pili ya mazoezi ikiwa kambini katika jiji la Ismailia, Misri lakini hadi jana mastaa wa timu hiyo walikuwa wakifanyishwa mazoezi magumu pekee, huku kipa Ayoub Lakred akiongeza mzuka kwa kutimba kambini humo akitokea Morocco alikokuwa mapumzikoni.
Lakred aliungana na wenzake katika kambi hiyo ya siku 18 ya kujiandaa na msimu mpya wa mashindano, huku leo ikiwa ni siku ya tatu tangu msafara wa Simba utue jijini humo na kuanza mazeozi kwa siku mbili mfululizo.
Tangu ifike Misri, timu hiyo imekuwa ikijifua chini ya kocha mmoja pekee, Seleman Matola ambaye ndiye aliyetangulia na kikosi hicho.
Ratiba ambayo Matola amekuwa akianza nayo na mastaa wa timu hiyo ni ile ya pumzi na stamina, wakikimbia sana na kufanya matizi mengine ya kuimarisha nguvu ya miili kabla ya kesho Ijumaa kuhamia kwenye gym na wiki ijayo kuanza kusukuma boli uwanjani ambapo kocha mkuu, Fadlu atakuwa akitoa maujuzi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kambini Misri ni kwamba ratiba hiyo Matola amekuwa hataki kumuangalia mtu usoni, kwani unaambiwa amekuwa akiwatoa mbio wachezaji wote ili kuhakikisha kabla ya makocha wengine kufika wawe wameanza kuwa sawa.
FADLU, JESHI ZIMA FRESHI
Simba ilipoondoka iliwaacha nyuma makocha wote wapya chini ya kocha mkuu Fadlu Davids ambao hati zao za kusafiria zilichelewa kupatikana.
Hata hivyo, alfajiri ya kuamkia jana makocha hao walifanikiwa kusafiri na leo watakuwa na ratiba ya kwanza ya mazoezi na kikosi hicho.
Wakiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere makocha hao walionekana sambamba na baadhi ya wachezaji waliobaki nyuma akiwamo beki David Kameta ‘Duchu’ na Hussein Kazi ambaye alikwama juzi kuondoka na kundi la kwanza.
KAMBI YA KISHUA
Simba imefikia kwenye hoteli ya kishua ya Mercure Ismailia Forsan Island ambayo itatumiwa na watu zaidi ya 40 waliosafiri na timu hiyo wakiwamo wachezaji, watu wa benchi la ufundi na maofisa wengine wa klabu hiyo.
Kukaa kwenye hoteli hiyo sio kitu rahisi kwani chumba cha chini kinaanzia bei ya 170,000 hadi 420,000 kwa siku moja ikitegemea na unataka chumba cha upande upi wa bahari au eneo jingine.
VIGOGO WAKO NYUMA
Baadhi ya vigogo wa Bodi ya Wakurugenzi wakitaka kujiridhisha kwamba kikosi chao kinaiva sawasawa kabla ya kurejea inaelezwa nao watasafiri kwenda nchini humo kujionea namna mambo yatakavyokuwa yanafanyika.
Ikiwa kambini, Simba inatarajiwa kucheza mechi zisizopungua tatu za kirafiki kabla ya kurejea nchini mapema Agosti kuwahi Tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 3 ambapo inatarajiwa kucheza mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa kisha kuanza maandalizi ya Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga katika Ngao ya Jamii.
Michezo ya Ngao ya Jamii inatarajiwa kupigwa kati ya Agosti 8-11 ikishirikisha klabu nne zikiwamo Coastal Union na Azam FC zitakazoumana katika mechi nyingine ya nusu fainali na washindi wa mechi hizo watakutana fainali. Msimu uliopita Simba iliifunga Yanga kwa penalti 3-1 katika fainali.