LICHA ya kikosi chote kipya cha Simba kuwa kambini Ismailia, Misri, hiyo haijawazuia mabosi wa klabu hiyo kuendelea kushusha mashine mpya, baada ya kumnasa beki aliyekuwa Singida FG, Kelvin Kijiri ili kuimarisha eneo hilo la kulia lenye mkongwe Shomari Kapombe.
Kijiri amemalizana na Simba kwa mkataba wa miaka miwili na Mwanaspoti linafahamu, beki huyo amemwaga wino baada ya Israel Mwenda aliyeongezewa mkataba wa miaka miwili Msimbazi kuelezwa amesaini timu mbili.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli Kijiri amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo msimu ujao na wakati wowote atatambulisha na kusafiri kwenda kuungana na wenzake Misri ambako wameweka kambi.
“Hatukuwa na sababu ya kusajili eneo hilo kwani tayari kulikuwa na Shomari Kapombe na Mwenda lakini kuna shida imetokea ndio maana umefanyika usajili huo ambao pia tunaamini utaongeza nguvu,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Simba kilichoongeza;
“Kijiri ameungana na msafara wa pili wa timu hiyo sambamba na makocha kwenda kambini Misri.”
Mwenda ameripotiwa kusaini mkataba Singida Black Stars ili kumkwepa Kapombe ambaye alitarajia asingeongezwa mkataba Simba ili yeye ndio abaki.