Ukweli kuuzwa kwa Alliance FC ni huu

BAADA ya uwepo wa taarifa za timu ya wavulana ya Alliance FC ya jijini hapa kuuzwa mkoani Arusha, uongozi wa klabu hiyo umeibuka na kutolea ufafanuzi huku ukiwatoa wasiwasi mashabiki wake.

Timu hiyo ambayo iliponea chupuchupu kushuka daraja kutoka First League msimu uliopita baada ya kusuasua kwa kile kinachotajwa ni ukata unaoikabili, hivi karibuni zimeibuka taarifa za Alliance FC kuuzwa jijini Arusha kwa tajiri kutoka nchini Kenya.

Mwenyekiti wa Alliance za jijini hapa, Stephano Nyaitati alisema uvumi huo siyo wa kweli kwani timu hiyo bado ni mali yao na hawana mpango wa kuiuza, huku wakiwa kwenye hatua za mwisho za kuleta benchi la ufundi na kuanza kutambulisha wachezaji wapya.

“Tumeuza? Hata kama njaa tunayo siyo ya namna hiyo, hizo taarifa siyo za kweli hatujauza na hatuna mpango wa kuuza kwa hiyo huo mpango hautakuwepo. Tunajua sana umuhimu wa kuwa na timu ya wanaume kwenye taasisi yetu kwa hiyo hatuwezi kuuza hayo ni maneno tu ya watu,” alisema Nyaitati na kuongeza;

“Kimsingi taarifa hizi hazina ukweli wowote. Naomba nikuhakikishie hatujauza na ukitaka uamini tutaanza kutambulisha usajili wetu, mashabiki wasubiri wataona kurasa za mitandao yetu ya kijamii zinaanza kuchafuka.”

Mchezaji wa timu hiyo, Yohana Shija akizungumzia tetesi hizo akiwa mapumzikoni mkoani Tabora alisema bado wachezaji hawajapewa taarifa yoyote na uongozi wa timu kama imeuzwa ili waanze maisha mapya kwingine.

“Huo uvumi wa timu kuuzwa ulikuwepo tangu msimu uliopita kutokana na mwenendo wa timu, lakini sijasikia lolote labda niulizie kwa viongozi nini kinaendelea. Wachezaji hatujapata taarifa hizo hadi sasa kama kuna lolote tungekuwa tumeambiwa,” alisema Shija.

Related Posts