Wafanyabiashara Kariakoo wafunga Barabara ya Lumumba Dar

Dar es Salaam. Baadhi ya wafanyabiashara wanaodai majina yao kutokuwamo kwenye orodha ya watakaorejea Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, wamegoma kuondoka katika Barabara ya Lumumba, kwenye ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM.

Wamechukua uamuzi huo wa leo Alhamisi, Julai 11, 2024 baada ya kufika Viwanja vya Mnazi Mmoja kuhakikiwa upya na kueleza kutokuridhika, wakidai haki yao haitapatikana.

Walioandamana ni sehemu ya wafanyabiashara zaidi ya 800 ambao majina yao yamewekwa kando katika orodha iliyotolewa jana Jumatano, Julai 10, 2024 kuwa hawatarejea baada ya ujenzi kukamilika.

Mara baada ya kufika Lumumba, walianza kuimba nyimbo mbalimbali na baadhi ya viongozi wa CCM akiwemo Mkuu wa Utawala wa chama hicho, Marco Mbanga walianza kuwatuliza ikiwemo kuwaeleza kusogea pembeni ili wapishe barabara wakati suala lao la kutaka viongozi wa juu kufika uwasikiliza likifanyiwa kazi.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wamekataa kutoka wakitaka kusikilizwa suala lao wakidai wamechoka kuhakikiwa.

Kitendo hicho kimesababisha foleni ya magari barabarani kwa kuwa yamelazimika kutumia upande mmoja.

Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu amefika na kuwaeleza: “Maelekezo ya Serikali ni wafanyabiashara wote waliokuwa sokoni Kariakoo warudi.”

Kisha amesema Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wanasubiriwa kufika eneo hilo kuwasikiliza.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi

Related Posts