Tabora. Watu 23 ambao ni baadhi ya viongozi wa Kampuni ya Alliance in Motion Global, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Tabora kwa tuhuma za kufanya udanganyifu kwa vijana zaidi ya 100 ambao walipigiwa simu kutoka mikoa ya Manyara, Arusha, Singida, Dodoma na Morogoro kwa lengo la kuwapatia ajira zenye mshahara mnono, badala yake wakatapeliwa.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 11, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Deusdedit Katwale amesema wamefikia uamuzi huo baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kubaini kuwa vijana hao wanahangaika baada ya kutapeliwa.
“Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Tabora tumeamua kampuni hii ya Alliance In Motion Global iliyokusanya zaidi ya vijana 100 kufungwa kwa kuwa wamekuwa wakiwatapeli vijana kwa kuwaahidi kuwapa ajira na wanapofika hapa Tabora wanabadilishiwa mitazamo.
“Nimekuwa nikipokea malalamiko ya vijana walio chini ya miaka 18 kwamba wametoka mikoa mbalimbali kuja hapa Tabora kwa ahadi ya kuajiriwa na kampuni ya Alliance in Motion Global ambapo baada ya kufika wanatozwa pesa na kutapeliwa. Mimi kama Mkuu wa Wilaya hapa, sitaki kuona shughuli za kampuni hii zikiendeela kufanyika kwenye manispaa yetu ya Tabora. Sitaki kuona darasa hapa na sitaki kuona mtu hapa,” amesema.
Amesema viongozi wote ambao wamekuwa wakitumika kuwaita vijana hao kutoka mikoa mbalimbali, wanawashikilia na wanaendelea kuwahoji ili ikibainika wamefanya utapeli wafikishwe mahakamani, hadi sasa wamebainika kutokuwa na leseni wala kodi ya mapato wanayolipa Mamlaka ya Mapato (TRA).
Atieno Rigo, Ofisa Ustawi wa Jamii katika Manispaa ya Tabora, amesema wametambua vijana 93 wakiwa wametapeliwa na viongozi wao 10 ambapo utaratibu unafanyika ili watoto hao ambao wengi wako chini ya miaka 18 warejee makwao.
“Hapa tumebaini vijana walio chini ya miaka 18 wakiwa wengi na kinachofanyika wakishapigiwa simu za ajira, wanasafiri hadi Tabora ambapo wanaahidiwa kutafutiwa nyumba na kupewa mafunzo baada ya malipo ya fedha.
“Tumeongea nao wamekiri kuwa hawajaanza kupata faida yoyote, hivyo kwa kuwa maagizo ya mkuu wa wilaya yametolewa, tumeanza kufanya utaratibu ili waweze kwenda makwao,” amesema ofisa huyo.
Nikta John ambaye ni mmoja wa vijana aliyetapeliwa, amesema alipewa taarifa na rafiki yake kuhusu uwepo wa ajira na alipofika alilipa fedha ya kiingilio Sh35,000 lakini hadi sasa hajapata faida yoyote.
“Nililipa Sh35,000 ya kiingilio, baadaye nikalipa Sh450,000 kwa madai kwamba ningefaidika kwa kufanya biashara, lakini hhadi leo sijapata faida yoyote, naiomba Serikali nirudishiwe pesa zangu ili nirudi nyumbani,” amesema.
Kwa upande wake, Obeid Joseph amesema alikuja kwenye mafunzo hayo bila kujitambua, hivyo anaiomba Serikali imsaidie nauli ili arudi nyumbani.
“Nilikuja hapa Tabora bila kujitambua na baada ya kufika hapa wamekuwa wakitufundisha mifumo ambayo ni ya udanganyifu kwa kiasi kikubwa, na kwa kuwa imebainika ni matapeli, nawaomba Serikali iwachukulie hatua kali,” amesema.