Kesi ya ukahaba yaibua mapya, hakimu kuwashtaki waendesha mashtaka

Dar es Salaam. Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Sokoine Drive, Dar es Salaam, Lugano-Rachae Kasebele amewashtaki Mahakama Kuu, waendesha mashtaka katika kesi ya ukahaba inayowakabili washtakiwa watano, baada ya kuidharau mahakama hiyo kwa kushindwa kutekeleza amri alizotoa kwao.

Hakimu Kasebele amefikia hatua hiyo baada ya amri mbili alizotoa Julai 8,2024 dhidi ya upande wa mashtaka kushindwa kutekelezwa.

Kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kutekeleza amri hiyo, hakimu Kasebele amesema anapeleka jalada la shauri hilo Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya maelekezo, kwa sababu mawakili wa Serikali wanadharau amri zake anazotoa.

Amri hizo ambazo upande wa mashtaka umeshindwa kuzitekeleza na hivyo kuwaweka matatani, ni kuwasilisha taarifa ya kitabibu kuthibitisha ugonjwa wa shahidi wake wa nne katika kesi hiyo WP Konstebo (PC) Masadi Kassim Madenge wa kituo cha Polisi Magomeni Usalama.

Amri nyingine ni kufikisha mahakamani uthibitisho wa mashahidi wake wengine ambao pia ni askari polisi waliodaiwa wako kwenye kazi maalumu.

Uamuzi huo wa kuwashtaki Mahakama Kuu waendesha mashtaka hao, aliutoa Ijumaa ya Julai 12, 2024 muda mfupi baada ya kumaliza kusikiliza kesi ya ukahaba inayowakabili washtakiwa watano wakazi wa  Dar es Salaam.

Kabla ya kutoa uamuzi huo, hakimu Kasebele aliwauliza upande wa mashtaka kuhusiana na amri aliyotoa wiki iliyopita kama wametekeleza, baada ya kiongozi wa jopo la wakili wa Serikali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraji Ngukah kueleza mahakama hiyo kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi na upande wa mashtaka wana shahidi mmoja, ambaye yupo tayari kusikiliza.

Ngukah baada ya kueleza hayo,  Kasebele aliwauliza kuhusu amri ya mwisho iliyotolewa na mahakama wanasemaje.

“Ehhh, kuhusu amri ya mwisho iliyotolewa na Mahakama hii mnasemaje,” amehoji Hakimu Kasebele.

Hata hivyo, Ngukah amejibu wanasubiri uamuzi wa Mahakama na wapo tayari kuupokea uamuzi wa mahakama iwapo itautoa.

“Mheshimiwa hakimu, tunasubiri uamuzi wa mahakama na tupo tayari kupokea uamuzi wa mahakama iwapo itatoa uamuzi” amedai wakili Ngukah.

Hakimu Kasebele amesema kutokana na kilichotokea, ataanza kwanza kusikiliza shahidi aliyefika mahakamani hapo kwa ajili ya kutoa ushahidi na baada ya shahidi huyo ambaye ni F1379  Sajent Ramdhani Kumaliza kutoa ushahidi wake ndipo atatoa uamuzi.

“Sasa, kutokana na hicho kilichotokea, tutasikiliza shahidi mmoja halafu baada ya shahidi huyu kumaliza kutoa ushahidi, nitatoa uamuzi kuhusiana na amri zilizotolewa na mahakama,” amesema hakimu.

Hata hivyo, baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, hakimu alitoa uamuzi kuhusiana na upande wa mashtaka kushindwa kutekeleza amri zilizotolewa na mahakama hiyo.

Katika uamuzi wake, hakimu Kasebele amesema, bado upande wa mashtaka hamjatekeleza amri mbili mlizopewa na mahakama.

“Kuhusiana na amri mbili zilizotolewa na Mahakama hii dhidi ya upande wa mshtaka, naona bado hazijatekelezwa hivyo, jalada la kesi hii nalipeleka Mahakama Kuu kwa ajili ya maelekezo kwa sababu mawakili wa Serikali wamedharau amri zilizotolewa na mahakama hii,” amesema Hakimu Kasebele.

Baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 24, 2024 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo jalada hilo limefanyiwa kazi Mahakama Kuu.

Mahakama ilitoa amri hizo baada ya mawakili wa utetezi katika kesi hiyo, Peter Madeleka, Jebra Kambole na Maria Mushi, kupinga taarifa za ugonjwa wa shahidi huyo, wakidai mahakama haiwezi kutambua ugonjwa kwa kuangalia kwa macho tu.

Badala yake walitaka upande wa mashtaka uwasilishe uthibitisho wa taarifa ya matibabu.

Kwa kuwa baada ya upande mashtaka kueleza shahidi wake huyo aliyekuwa ameandaliwa kutoa ushahidi kupatwa na matatizo ya kiafya na hivyo kesi ikaahirishwa mapema, mawakili wa utetezi pia waliomba mahakama ielekeze upande wa mashtaka uwe unaandaa mashahidi wengi.

Hata hivyo, waendesha kesi hiyo mawakili wa Tumaini Mafuru na Winfrida Ouko, wamedai mashahidi wao wengine ambao ni askari polisi walikuwa kwenye kazi maalumu, taarifa ambayo pia ilipingwa na mawakili wa utetezi wakitaka uthibitisho huo.

Mahakama ilikubaliana na hoja za upande wa utetezi ndipo ikatoa amri hizo mbili, kuwasilisha taarifa ya kitabibu kuthibitisha ugonjwa wa shahidi huyo na uthibitisho wa mashahidi wengine kuwa katika kazi maalumu.

Akitoa uamuzi kuhusiana na mwenendo wa upande wa mashtaka kushindwa kutekeleza amri hizo, Hakimu Kasebelea kwanza alirejea historia ya mwenendo wa amri zake kwa upande wa mashtaka na jinsi ambavyo umeshindwa kuzitekeleza.

Pili, alibainisha msimamo au maelekezo ya Mahakama za juu (Mahakama Kuu) kwa suala kama hilo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Amesema Juni 27, 2024 mahakama ilitoa amri mbili kwanza kuhusu uthibitisho wa ugonjwa wa shahidi ambaye alitarajiwa kutoa ushahidi wake siku hiyo.

Alisema hoja hiyo ilizua utata baada ya upande wa utetezi kupinga wakihitaji uthibitisho wa kitabibu na kwamba ili kuondoa wasiwasi mahakama ikaamuru iletwe taarifa ya kitabibu kuthibitisha ugonjwa huo wa shahidi.

Hakimu Kasebele alisema Juni 28, 2024 shahidi huyo alifika mahakamani, lakini upande wa mashtaka ukaeleza kwamba alikuwa anatakiwa kwenda hospitalini na Mahakama ikaamuru tena kuwa akitoka hospitalini taarifa ya matibabu yake iwasilishwe mahakamani.

“Lakini tangu tarehe hiyo mpaka Julai 2, hakuna taarifa iliyoletwa.

Kwa hiyo amri ya Mahakama haikutekelezwa na mpaka sasa haijatekelezwa,”amesema hakimu Kasebele.

Amesema kuwa amri ya pili ilikuwa kwambam kwa kuwa upande wa mashtaka una mashahidi kumi basi wawe wanaitwa watatu ili kutocheleweshwa haki (yaani kama ikitokea dharura kwa shahidi mmoja mashahidi wengine wanaendelea).

Vile vile amesema kuwa mahakama ilielekeza kuwa kama kuna tatizo basi taarifa ya tatizo la kushindwa kuwaita mashahidi wengine itolewe mahakamani.

“Lakini taarifa tuliyopewa na Wakili Tumaini ni kwamba mashahidi wengine walikuwa kwenye kazi maalumu ambayo hatujaambiwa inaishi lini,” amesema Hakimu Kasebele.

“Hili nalo linazua wasiwasi wa kucheleweshewa kesi kutokana na sababu zisizo za msingi. Mahakama inasisitiza kuletwa mashahidi zaidi ya watatu na kama kuna changamoto taarifa itolewe, Lakini mpaka sasa hizo hazijatekelezwa”

Hakimu Kasebele amesema Julai 2, 2024 alipohoji kuhusu taarifa ya uthibitisho wa ugonjwa wa shahidi huyo, upande wa mashtaka ulijibu kuwa shahidi tayari alikuwa ameshafika mahakamani na kutoa ushahidi wake.

Siku hiyo wakili wa Serikali, Mwasiti Ally alijibu hawakuwa taarifa hiyo na kwamba hawawajibiki, huku akidai kuwa kwa kuwa tayari shahidi huyo alikuwa ameshafika mahakamani na kutoa ushahidi wake,  basi yeye ndiye alipaswa kutoa taarifa hiyo.

Ameendelea kufafanua kuwa, hata Mahakama katika amri zake hizo haikusema kuwa kama shahidi huyo aliyedaiwa kuwa mgonjwa atafika mahakamani basi amri zake zinakoma.

“Hivyo Julai 3, 2024 Mahakama iliamua kutoendelea na kesi kutokana na kuona kuna kitisho au wasiwasi wa amri zake kutoendelea kutekelezwa,” amesema Hakimu Kasebele.

Amesisitiza licha ya mawakili wa utetezi kuwasilisha kesi rejea kuhusiana na maelekezo au msimamo wa mahakama kuhusu utekelezaji wa amri za mahakama,  cha kusikitisha upande wa mashtaka umeendelea kutotekeleza amri hizo.

Hakimu Kasebele amesisitiza kuwa kwa mujibu wa hukumu mbalimbali za Mahakama Kuu (ambazo amezibainisha), kama upande wa mashtaka hawakuwa wameelewa amri hizo ilizozitoa mahakama walipaswa kuomba ufafanuzi.

Amesema kuwa hatua ya pili wangekata rufaa dhidi ya uamuzi/amri hizo, au kuiomba mahakama ya juu ikatoa ufafanuzi wa amri hizo lakini upande wa mashtaka katika hatua zote hizo hakuna ilichokifanya badala yake umeendelea kutotekeleza amri hizo.

Amesema kuwa amri ya mahakama ni uamuzi rasmi wa mahakama, na kwamba amri hiyo yaweza kuwa ni agizo au maelekezo kwa upande husika ili kuhakikisha haki inatendeka au sheria inafuatwa.

Amesema Mahakama Kuu imesema kutoheshimu amri ya Mahakama ni jambo baya ambalo halivumiliki na kwamba kuna hukumu mbalimbali ambazo imetoa maelekezo amri za mahakama zisipotekelezwa na upande husika.

Ameyataja maelekezo hayo kuwa mahakama husika inaweza kutoa adhabu kali kwa wale wanaokaidi amri zake kama kutoa onyo, kulipa faini, adhabu ya vifungo, kufuta kesi pale itakapoonekana kuna haja ya kufanya hivyo  na kuwapeleka wahusika wanaokaidi amri hizo kwenye kamati za nidhamu.

Washtakiwa katika kesi hiyo  ni Mariam Yusufu Mkinde (25) mkazi wa Magomeni, Mwazani Nassoro (25) mkazi wa Kigogo, Mwanaidi Salum (25) mkazi wa Mabibo, Faudhia Hassan (35) mkazi wa Ubungo na Tatu Omary (40) mkazi wa Ubungo.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 17277/2024, washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.

Related Posts