Kina Diarra watishia kujiondoa Mali kisa sakata la Traore

Dar es Salaam. Kufuatia kusimamishwa kwa nahodha wa timu ya Taifa Mali, Hamari Traoré wachezaji wenzake wametishia kujiondoa kwa pamoja kwenye kikosi hicho kwa kile walichokitaja uonevu kwa nahodha wao.

Nahodha huyo amefungiwa kwa kosa la yeye na baadhi ya wachezaji wenzake kumfokea na kumsonga mithili ya kumpiga mwamuzi Mohammed Adel raia wa Misri katika mechi ya robo fainali ya Kombe la mataifa ya Afrika mwezi Februari dhidi ya Ivory Coast baada ya kupewa kadi nyekundu.

Tukio hilo lilitokea baada ya Mali kupoteza mchezo wa  robo fainali dhidi ya wenyeji wa mashindano ya Afcon 2023 Ivory Coast kwa mabao 2-1 baada ya dakika 120.

Wachezaji wametoa taarifa leo Julai 12, 2024 wakifafanua kuwa maamuzi yote ya awali kuhusu masuala ya timu yalifanywa kwa pamoja na kundi lote la wachezaji na siyo Traoré pekee na kueleza hapaswi kuwajibishwa peke yake kwa vitendo vilivyoamuliwa kwa pamoja.

Taarifa hiyo inasomeka: “Kufuatia uamuzi Na. 051 wa Shirikisho la Soka la Mali, kuhusu kusimamishwa kwa muda kwa nahodha wa timu ya taifa, Hamari Traoré, sisi, wachezaji wa timu ya taifa, tunafahamisha kwamba maamuzi yote yaliyotangulia yalifanywa kwa pamoja na wachezaji wote na si kwa niaba ya Hamari Traoré peke yake.”

Uamuzi wa wachezaji kujiondoa kwenye timu ya taifa ni ishara ya mshikamano na kumuunga mkono nahodha wao na kuweka wazi kuwa hawatacheza tena kwenye timu ya taifa hadi adhabu hiyo itakapofutwa.

Aidha, hatua hiyo inaonyesha mshikamano na umoja ndani ya timu hiyo, ikisisitiza msimamo wao wa pamoja dhidi ya kile wanachokiona kama uamuzi usio wa haki.

“Tukiwa na ufafanuzi huu, tunalijulisha shirikisho kwamba sisi, wachezaji, tunajiondoa kwenye timu ya taifa hadi kusimamishwa kwa Hamari Traoré kutakapofutwa,” walisema wachezaji.

Hatua hiyo ya wachezaji imesababisha mshtuko mkubwa katika soka la Mali na imeweka shinikizo kubwa kwa shirikisho hilo kufikiria upya uamuzi wao wa kusimamishwa kwa Traoré na kujiondoa kwa wachezaji kunaweza kuwa na athari kubwa kwa timu ya taifa, hasa kwa mechi za kimataifa zijazo.

Shirikisho la Soka la Mali bado halijatoa jibu rasmi kwa taarifa ya wachezaji na kujiondoa kwao.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts