USAJILI wakati mwingine ni kama kamari. Unaweza kupatia. Pia unaweza kukosea. Ni ngumu kubetia usajili utakliki moja kwa moja. Hutokea mara chache sajili zikabamba. Ilitokea kwa Emmanuel Okwi alipotua Simba mara ya kwanza na hata alipokuwa akija na kuondoka. Lakini alichemka aliposajiliwa Yanga.
Kuna Kipre Tchetche alipotua Azam. Usajili wake ulikuwa na maana kubwa. Azam hadi leo bado inahangaika kusaka mrithi wa Kipre Chamazi.
Tuliona Clatous Chama alipotua mara ya kwanza kutoka Zambia. Tuliona pia kwa Luis Miquissone pale Msimbazi kwa mara ya kwanza. Lakini mambo yalienda kinyume aliporejea kutoka Al Ahly ya Misri.
Kuna Fiston Mayele. Usajili wake Yanga ulitiki kama ulivyokuwa kwa Pacome Zouzoua, Diarra Djigui. Khalidi Aucho. Yao Kouassi na hata Maxi Nzengeli na Stephane Aziz KI.
Azam wamebahatika kumnasa Feisal Salum ‘Fei Toto’, Kipre Junior na wengine na sajili hizo kulipa. Kipre tayari ameshaondoka, lakini alama alizoacha katika Ligi Kuu Bara na hususani katika klabu hiyo sio ndogo.
Amefunga mabao tisa na kuasisti tisa akiwa kinara wa msimu uliopita na ushirikiano wake na Fei Toto, Gibril Sillah na wengine umeipeleka Azam katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuondoa ufalme wa ligi ya timu Bara kwa Simba na Yanga kwa kutwaa nafasi ya pili juu. Hii hutokea kibahati sana.
Ndio, kuna sajili ngapi Azam ilifanya na ikawa inashindwa kutofautishwa na timu za madaraja ya kati. Haikuwa na maajabu. Ilikuwa inasajili na kuacha kwa zile nyingi zilikuwa bahati nasibu, hadi msimu uliopita kuwalipa.
Hata, Yanga inayotawala soka kwa misimu mitatu mfululizo, ilisumbuka sana katika sajili zake. Iliwaleta hadi kina Yikpe Gnamien Gislain, Klaus Kindoki, Michael Sarpong na wengine ambao waliiangusha timu. Wakati huo sajili za Simba za kina John Bocco, Aishi Manula, Okwi, Meddie Kagere, Luis, Chama na wengine zikitoa matunda Msimbazi na kutawala soka la nchi kwa misimu minne mfululizo.
Kwa sasa klabu hizo kubwa na nyingine zipo bize kushusha na kutambulisha mashine mpya. Simba imesajili sura saba za kigeni mpya na sita za wazawa. Ameletwa Debora Mavambo, Jean Ahoua, Augustine Okejepha, Steven Mukwala, Joshua Mutale, Valentin Nouma na Karaboue Chamou.
Wamekuja kuchukua nafasi za kina Luis, Chama, Henock Inonga, Sadio Kanoute, Saido Ntibazonkiza, Moses Phiri na Babacar Sarr, Kramo Aubin na wengine waliotemwa.
Chama amehamia Jangwani kutoka Msimbazi. Ni kama alivyowahi kufanya Bernard Morrison, Haruna Niyonzima, Ibrahim Ajibu, Jonas Mkude na wengine waliohama mtaa moja kwenda kwingine.
Hata hivyo, presha zilikuwa kubwa sana kuondoka kwa Chama kwenda Yanga. Ni tofauti na ilivyokuwa kwa Mkude. Augustine Okrah aliyewahi kuichezea Simba kabla ya kuibuka Yanga, kama anavyofanya sasa Jean Baleke.
Simba inapaswa kukubali kuanza maisha mapya kwa kuagana na Chama. Kisha akili na nguvu kubwa zihamie kwa nyota wapya waliosajiliwa, hususani Ahoua anayetajwa kama mrithi wa Mzambia huyo.
Ni kweli wachezaji wote waliosajiliwa Simba ni wakali. Wasifu wao unawabeba. Ahoua ametoka kuwa MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast. Anakuwa MVP wa tatu mfululizo wa Ivory Coast kutua Ligi Kuu Bara. Alianza Aziz KI akafuata Pacome na wote wameonyesha makubwa Yanga. Pia kuna MVP kutoka DR Congo waliokuja kwa kasi, Inonga na Maxi. Juzi kati Simba ilimpokea Willy Onana kutoka Rwanda.
Hata hivyo, Simba wanapaswa waweke mapozi, kwa sasa. Wasianze kuwatambia sana wachezaji hao na kuamini wataleta miujiza. Wawape muda ligi ianze wajue kama wamekula au kuchana mikeke yao katika sajili zilizofanyika.
Pia kuwakaushia kwa sasa itasaidia kuwapunguzia presha kabla ya kuanza kuzitumikia. Kuanza kumtaja Ahoua ndiye mrithi wa Chama ni kumbebesha mzigo mzito. Chama anabaki kuwa Chama na Ahoua ni Ahoua. Kila mmoja ana soka na ubora wake.
Ahoua na wenzake wanaweza kujikuta wakikwama mapema kwa kuvalishwa viatu vya watangulizi wao ambao wameacha alama kubwa Msimbazi. Ni kweli tambo kwa Simba na Yanga ni kawaida, lakini mashabiki wa klabu hizo hawana dogo.
Tuliona Onana alipopata wakati mguu kutokana na kupambwa sana. Ilikuwa hivyo hivyo kwa Kramo. Hajacheza hata mechi moja ya mashindano hadi anaondoka Msimbazi.
Tuwaache kina Ahoua, Okejepha, Debora na wengine wafanya kazi iliyowaleta kwa kutengeneza ufalme wao Msimbazi. Wanasimba wasilazimishe kuwavisha mataji yaliyoachwa na wenzao waliotangulia kwani ni msalaba mkubwa kwao.
Ni kama ilivyomtokea Kennedy Musonda, Hafiz Konkoni nam Joseph Guede pale Yanga kwa kutaka kulinganishwa na alama alizoziacha Mayele kabla ya kwenda Misri.
Vinginevyo, Simba inaweza isirejeshe makali na kukata kiu ya Wanasimba kwa nyota wapya kupambwa sana kisha waje kuchemsha kama ilivyowahi kumtokea Laudit Mavugo, Danny Sserunkuma, Brian Majwega, Raphael Kiongera, Frederick Blagnon na Perfect Chikwande.
Sajili zao zilipambwa sana na matarajio yalikuwa makubwa mno kwa mashabiki juu yao na mwishowe kushindwa kufanya kiu na kuishia kuondoka mmoja mmoja kimya kimya kwa aibu.
Ndio maana Mtu wa Mpira nasema mapema, Simba waache kuchonga sana, wasubiri ligi ianze wajue mkeka umelipa au la, vinginevyo watachekesha sana kama Yanga ilivyowahi kuchekesha kwa Robert Jama Mba na Mwenyekiti wa enzi hizo, Imani Madega alimpamba sana, lakini aibu ikamrudi mwenyewe, kama ilivyoirudia klabu hiyo kwa yule Mbrazili, Genilson Santana Santos ‘Jaja’.