Dar es Salaam. Makocha na nyota wa zamani wa soka nchini wamezitabiria makubwa timu za Tanzania Bara zinazoshiriki mashindano ya klabu Afrika msimu ujao huku wakiamini zinaweza kutwaa ubingwa.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Tanzania itawakilishwa na Yanga na Azam wakati kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, wawakilishi ni Simba na Coastal Union.
Kwa mujibu wa Droo ya hatua za mwanzo za mashindano hayo iliyochezeshwa Alhamisi huko Afrika Kusini, Yanga imepangwa kuanza na Vital’O ya Burundi katika hatua ya awali huku Azam ikipangwa na APR ya Rwanda.
Simba yenyewe haitocheza hatua ya awali huku Coastal Union ikipangwa kukabiliana na One Bravos ya Angola.
Aliyekuwa kocha msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor ‘Cheche’ alisema kiufundi anaona timu zimesajili vizuri, hasa ambazo ambazo zimepata nafasi ya kushiriki michuano ya CAF na anaamini mojawapo itachukua ubingwa na nyingine kufika fainali.
“Azam, Yanga, Coastal Union na Simba itakayoanza hatua inayofuata, zina asilimia kubwa ya kufika fainali na nyingine kuchukua ubingwa, hilo lipo mikononi mwao kabisa, kulingana na timu walizopangwa nazo.
“Kitu kikubwa makocha wazingatie mbinu, aina ya mechi hizo, matokeo yanapatikana kwa mbinu na siyo ufundi mwingi, mfano mzuri ni Yanga walivyocheza na Mamelodi mwaka jana, kilichoamua matokeo ni mbinu, ufundi haukuwa mkubwa,” alisema Cheche
Kwa upande wa kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, alitoa utabiri wake mapema kwamba kuna timu itafika fainali na nyingine itachukua ubingwa wa michuano.
“Nimefuatilia usajili wa timu hizo, mfano Yanga imeongeza watu wengine mbele kama Prince Dube, Clatous Chama, Jean Baleke, Azam FC imesajili mafundi wanaojua mpira, Simba imesajili wachezaji vijana na wenye vipaji vikubwa kama Joshua Mutale, Steven Mukwala, bila kuisahau Coastal Union, hilo linaniaminisha utakuwa msimu wa Tanzania kutamba kimataifa.
“Jambo linalotakiwa ni wachezaji kujitambua na kuweka dhamira ya kuandika rekodi zao kimataifa ambazo zutawapa heshima wao wenyewe na klabu zilizowaajiri,” alisema Julio.
Kocha mkongwe wa makipa, Idd Pazi alisema kama maandalizi ya timu hizo, yatafanywa kikamilifu, anaamini msimu huu utakuwa wa neema kwa Tanzania, kuandika rekodi za heshima Afrika hasa kwa kuchukua ubingwa.
“Naiona nafasi kubwa kwa timu zetu kufika fainali na mojawapo kuchukua ubingwa, jambo la msingi wajue mechi za michuano hiyo, zinatumia zaidi mbinu kwa maana hiyo wachezaji wajengwe kimbinu kulingana na timu watakazokutana nazo,”alisema.
Kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amekuwa na mtazamo tofauti ambapo amesema timu za Tanzania, zijipange kisawasawa bila kudharau nchi ambazo wapinzani wao wanatoka, ili kujitengenezea mazingira ya kufika mbali kwenye michuano hiyo.
“Soka la Afrika kwa sasa viwango vya wachezaji ama uwezo wao umeshabiana, hivyo viongozi wa klabu wafanye majukumu yao kwa wakati, ili kurahisisha kazi ya makocha, pia wachezaji walipwe stahiki zao ili wakianza kazi wasiwe na manung’uniko,”alisema.