Dar es Salaam. Watu 32 wamejitokeza kuomba mikopo ya Sh75 milioni inayotolewa na Serikali kwa ajili ya kujenga vituo vya mafuta vya gharama nafuu maeneo ya vijijini, ikiwa ni hatua ya kutokomeza uuzwaji wa mafuta ya dizeli na petroli kwenye vidumu.
Maombi hayo ambayo sasa yapo katika mchakato wa kufanyiwa tathmini, pia yanakuja wakati ambao Serikali imekusudia kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na kituo cha mafuta nchini.
Ni mwaka mmoja sasa tangu Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kutangaza kuanza kupokea maombi juu ya utoaji wa mikopo hiyo Mei, 2023 ili kukabiliana na madhara yatokanayo na njia zisizo salama zinazotumika katika uuzaji wa mafuta vijijini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Wakala wa Umeme Vijijini, Jones Ololo wakati akitoa tathmini ya utendaji wa wakala huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Ololo amesema fedha hizo zipo wazi kwa watu wote wanaotaka kuwekeza katika ujenzi wa vituo vidogo ikiwemo watu binafsi au kampuni, lakini wakiwa wametimiza masharti yote ikiwemo vibali vya ardhi, kibali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Amesema matamanio ya Rea ni kila kijiji kiwe na kituo cha mafuta kwa sababu wapo watu wanayauza kwa kutumia vidumu na wanalala nayo chini ya uvungu wa kitanda ili wasiibiwe.
“Ikitokea bahati mbaya kuna mvuta sigara au moto wengi wanalipukiwa na wakati mwingine wanafariki sasa tunataka tumalize tatizo hilo, fedha zipo wazi kwa watu, kampuni, mtu binafsi au yoyote anayeweza kuwekeza,” amesema Ololo.
Amesema awali kigezo cha mtu kuwa na hati ya ardhi ilikuwa kikwazo kwa watu wengi ndipo waliamua kubadili na kuamua kupokea hadi hati ya Serikali ya kijiji.
Amesema mpaka sasa wameshapokea maombi takribani 32, wanayafanyia uchambuzi na atakayekidhi vigezo atapewa fedha kwa ajili ya kwenda kuendeleza mradi.
“Bado tunapokea maombi na kufanya uchambuzi na atakayeshinda atapewa fedha, mpaka sasa maombi tuliyopokea hayazidi 32, kikubwa ni uelewa na tumeendelea kutoa elimu kwa wananchi, urahisi wa vibali, hati mwanzo tulikuwa tunapata shida watu kuwa nazo lakini sasa hata hati za vijiji na kimila tunazipokea,” amesema Ololo.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakienda kutafuta fursa hiyo ya kukopa lakini wanaogopa itakavyokuwa baadaye, jambo linalowalazimu kutumia wataalamu wa biashara kuwaondolea hofu waliyonayo.
Katika tangazo lake la Mei mwaka jana, Rea ilisema mpango huo unalenga kuondosha gharama kubwa za upatikanaji wa bidhaa hizo maeneo ya vijijini tofauti na bei elekezi, gharama za usafirishaji na kuadimika kwa bidhaa hizo hasa maeneo ya vijijini.
Katika hilo, mmoja wa wauzaji wa mafuta mkoani Lindi, Masoud Mwandiga amesema matangazo yaongezwe zaidi ili watu wengi waweze kunufaika na fursa hiyo.
“Watangaze kwenye redio kila wakati ili tusikie kwa sababu siyo wote tunaweza kupata matangazo hayo sehemu wanayoweka,” amesema Mwandiga na kuongeza “Biashara yangu inakua na najua kuna siku nitamiliki sheli (kituo cha mafuta),” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Ololo amesema kama Rea imekuja na majiko kwa ajili ya taasisi ambayo yanatumia mifumo mitatu ikiwemo gesi asilia, gesi ya kupikia kutoka nje (LPG) na gesi inayozalishwa kutokana na kinyesi.