SINGIDA Black Stars imekuwa timu ya kwanza ya Tanzania kuaga michuano ya Kombe la Kagame 2024 inayoendelea jijini Dar es Salaam baada ya juzi jioni kuchapwa tena mabao 3-1 na SC Villa ya Uganda siku chache tangu iliponyukwa 1-0 na APR ya Rwanda, lakini hilo halijamshtua Kocha Patrick Aussems.
Kocha huyo wa zamani wa Simba, ametua Singida hivi karibuni na mechi hizo mbili za Kagame zilizoifanya timu hiyo ishike mkia ikiwa haina pointi na kuaga mapema, ziwe za kwanza kwake, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa madai, bado anaendelea kuisoma timu na mechi hizo zilikuwa kama sehemu ya mazoezi tu.
Singida iliyopo Kundi C, imebakisha mchezo mmoja wa kukamilisha ratiba dhidi ya Al-Merrikh ya Sudan Kusini, lakini hata kama itashinda haiwezi kumaliza kama mshindwa bora kwani itafikisha pointi tatu zilizopitwa na APR yenye sita na SC Villa, huku Wasudan wakiwa na alama moja mkononi kwa sasa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Aussems alisema, haikuwa lengo lao kufanya vibaya katika michuano hiyo ila wameitumia kama sehemu ya maandalizi ya msimu ‘pre Season’, huku akijivunia kikosi bora anachoamini kitaleta ushindani msimu ujao.
“Tunajaribu kuhakikisha tunafanya kila liwezekanalo ili kutengeneza kikosi bora ambacho tunaamini kitaleta ushindani kwa msimu ujao, matokeo tuliyopata ni chachu ya sisi kufanya vizuri kwa sababu makosa tuliyofanya ni njia ya kujirekebisha,” alisema kocha huyo wa zamani wa AFC Leopards ya Kenya.
Kocha huyo aliyeipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara mbili na kuifikisha hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2018-2019 alisema mashabiki waendelee kuiamini na kuisapoti timu hiyo kwani mambo mazuri yanakuja huko mbeleni.
Michuano ya Kagame iliyoanza Jumanne ya Julai 9, itahitimishwa Julai 21 na awali ilipangwa kufanyika Julai 20 hadi Agosti 4, ila baada ya ratiba ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kubana ikabidi kurudishwa nyuma ili kukidhi mahitaji ya timu.
Michuano hii inawakilishwa na timu 12 kutoka Mataifa tofauti ya Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati maarufu (CECAFA), zikiwa makundi tofauti ambapo kundi ‘A’ ni Coastal Union (Tanzania), Al Wadi (Sudan), JKU (Zanzibar) na Dekedaha kutokea Somalia.
Al-Hilal Omdurman ya Sudan, Gor Mahia (Kenya), Red Arrows (Zambia) na Djibouti Telecom ya Djibouti zinaunda Kundi ‘B’ huku Kundi ‘C’ likiwa na timu za SC Villa (Uganda), APR (Rwanda), Singida Black Stars (Tanzania) na Al-Merrikh ya Sudan.