Biden asema hang’oki licha ya makosa ya aibu – DW – 12.07.2024

Msimamo wake ulijiri wakati miito ya kumtaka kusitisha kampeni ikiongezeka, ambapo wabunge 17 wa chama cha Democratic wamejitokeza wazi na kumhimiza rais huyo mwenye umri wa miaka 81 kuachana na kampeni.

Katika mkutano muhimu na waandishi wa habari mwishoni mwa mkutano wa kilele wa NATO mjini Washington, Biden alikiri ipo haja ya kutuliza hofu miongoni mwa Wanademokrati lakini akasisitiza dhamira yake ya kuendelea na kampeni, na kusema hayumo kwenye kinyang’anyiro hicho kwa ajili ya urathi wake.

“Siko katika hili kwa ajili ya urathi wangu. Niko katika hili kukamilisha kazi niliyoanza,” Biden alisema. “Ratiba yangu imekuwa ya kuchosha kwa hivyo nikipunguza kasi na siwezi kufanya kazi hiyo, hiyo ni ishara kwamba sitakiwi kuifanya. Lakini bado hakuna dalili ya hilo. Hakuna.”

Soma pia: Mkutano wa Jumuiya ya kujihami NATO umehitimishwa, huku washirika wakiahidi mshikamano zaidi na Ukraine

Hata hivyo juhudi za kujionyesha kama kiongozi alie imara bado zilitiwa doa na hatua yake ya awali alipomtambulisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kama adui yake wa Urusi Vladmir Putin, na kisha kumtaja Makamu wa Rais Kamala Harris kama “Makamu wa Rais Trump” kwenye mkutano wa habari wa NATO.

Kampeni ya Biden imekumbwa na mgogoro tangu alipoboronga kwenye mdahalo wa televisheni dhidi ya Trump wiki mbili zilizopita, na kuibua wasiwasi mpya kuhusu umri wake– na mkutano huo wa waandishi habari uliodumu kwa karibu saa nzima, ulikusudiwa kuonyesha kwamba bado anao uwezo.

Marekani| Mkutano wa habari wa Rais Joe Biden mjini Washington.
Biden akizungumza na waandishi habari akiwa pekee yake na bila maandishi yoyote kujaribu kuonyesha yuko timamu bado. Mkutano huo ulifuatia kukamilika kwa mkutano wa kilele wa NATO Julai 11, 2024.Picha: Kevin Dietsch/Getty Images

Rais huyo amekabiliwa na wito unaoongezeka wa Wademokrat kuachana na kampeni yake, wakihofia kwamba Trump atamshinda kwa urahisi, na idadi hiyo iliongezeka baada ya mkutano wa wa jana ambapo mpaka sasa wabunge 17 wa chama hicho wamjitokeza wazi wazi kumtolea wito Biden aachane na kampeni.

Majaribio ya uwezo wa Harris kuchukua mikoba

Biden aliweka wazi kuwa anamuunga mkono Harris — ambaye kama makamu wa rais angechukua nafasi yake katika hali ya dharura, lakini pia anaonekana na idadi inayoongezeka ya Wanademokrat kama mgombea mwenye nguvu kwa tiketi ya chama hicho.

Huku kukiwa na ripoti kwamba timu ya kampeni ya Biden inapima kimya kimya nguvu ya Harris katika mchuano wa kinadharia dhidi ya Trump, rais huyo alisema asingemchagua kuwa makamu wake kama asingekuwa na uwezo wa kuwa rais.

Soma pia: Shinikizo la kumtaka Biden kutowania muhula wa pili laongezeka

Pia alikanusha ripoti kwamba alihitaji kulala ifikapo saa mbili usiku, wakati ambao alikuwa bado akifanya mkutano wake na wanahabari siku ya Alhamisi.

Lakini baada ya kulaumu utendaji mbaya katika madahalo kwa mchanganyiko wa uchovi wa safari za ndege na baridi, alikiri kwamba itakuwa “ni jambo la busara kwangu kujiweka sawa kidogo.”

Alisisitiza pia kwamba uchunguzi wa mishipa ya fahamu ulionyesha alikuwa katika “hali nzuri” na kusema angechukua vipimo vingine ikiwa madaktari wake watapendekeza hivyo, lakini bado hawajafanya hivyo.

Marekani | Mdahalo kati ya Biden na Trump mjini Washington
Katika mdahalo wa televisheni na Trump wiki mbili zilizopita, Biden alifanya makosa ya kadhaa yaliozusha wasiwasi kuhusu uwezo wake wa kushinda uchaguzi na kuongoza nchi hiyo kubwa zaidi kiuchumi na kijeshi duniani.Picha: Yuri Gripas/abaca/picture alliance

Sera ya kigeni na uwezo wa kuwashughulikia Putin na Xi

Biden pia alijibu msururu wa maswali kuhusu sera ya kigeni na ya ndani yenye majibu ya kina ambayo wakati mwingine yalipotoka, huku akichanganya Ulaya na Asia.

Huku maswali yakiulizwa juu ya uwezo wake wa kushikilia msimamo wake dhidi ya viongozi wa kiimla kama Putin au Xi Jinping wa China, Biden alisema yuko “tayari kukabiliana nao sasa na miaka mitatu kuanzia sasa.”

Hata hivyo utendakazi wake wa uhakika ulishindwa kuzuia wasiwasi, huku wabunge watatu zaidi wa chama cha Democratic wakimtaka aache kinyang’anyiro hicho, na kufikisha jumla ya 17.

Wakati huo huo Trump alimdhihaki Biden kuhusiana na makosa yake wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Mdanganyifu Joe anaanza mkutano wake na waandishi wa habari wa ‘Big Boy’ na, ‘Nisingemchagua Makamu wa Rais Trump kuwa makamu wa rais… Kazi nzuri, Joe!” Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Kijamii wa Truth Social.

USA | Mgombea wa chama cha Republican Donald Trump
Donald Trump amekuwa akitumia kila fursa anayoipata kumdhihaki Biden na kumuonyesha kuwa kiongozi dhaifu asiweza tena kuongoza.Picha: GIORGIO VIERA/AFP/Getty Images

Viongozi wa NATO wamuunga mkono Biden

Ikulu ya White House iliutaja kama mkutano wa “Big Boy” ikiwa ni mara ya kwanza kwa Biden kuonekana peke yake, bila maandishi ndani ya miezi minane — huku kukiwa na shutuma kwamba uzee wake umemzuwia kuonekana mbele ya umma.

Wasiwasi juu ya afya ya Biden ulizidishwa na kosa la lake kwenye jina la Zelensky, ambalo lilizusha minong’ono ndani ya chumba cha mkutano. Zelensky, kiongozi wa wakati wa vita wa Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi 2022, alicheka.

Soma pia: Mamilioni ya Wamarekani kufuatilia mdahalo wa Televisheni kati ya Joe Biden na Donald Trump

Viongozi wenzake katika mkutano wa NATO walijibu maswali kuhusu utimamu wake na majibu yao yalikuwa yanamuunga mkono kwa ujumla. “Kuteleza kwa ulimi hutokea,” Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisema.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisema Biden alionekana imara wakati wa mkutano, huku Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer akisema “alikuwa katika hali nzuri.”

Mchuano mkali kati ya Biden na Trump

Lakini waungaji mkono muhimu wa Marekani wamejitenga na maneno ya kupamba ya kidiplomasia.

Washington Marekani| Mkutano wa 75 wa kila mwaka wa jumuiya ya NATO
Viongozi kadhaa wa NATO wanatamani Biden aendelee kuongoza wakihofia mhula mwingine wa Trump utaivuruga jumuiya hiyo ya kijeshi.Picha: Yves Herman/REUTERS

Muigizaji wa Hollywood na mfadhili wa chama cha Democratic George Clooney alitoa wito kwa Biden kuondoka kwenye kinyang’anyiro, na bibi wa chama Nancy Pelosi alisita kumuunga mkono kikamilifu.

Kura ya maoni iliyotolewa Alhamisi ilionyesha zaidi ya nusu ya Wanademokrasia wanasema Biden anapaswa kusitisha azma yake ya kuwania muhula wa pili, na theluthi mbili ya Wamarekani wanaamini anapaswa kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.

Biden na Trump wanaendela kukaribiana sana kwenye uungwaji mkono wa umma kwa asilimia 46-47 mtawalia, kulingana na uchunguzi uliofanywa na shirika la uchunguzi wa maoni la Ipsos kwa niaba ya mashirika ya Washington Post na ABC News.

Chanzo: Mashirika

Related Posts