Iringa. Zaidi ya Sh3.4 bilioni zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kipya cha parachichi katika eneo la Nyololo, Wilayani Mufindi ili kusaidia uchakataji wa zao hilo kabla ya kufika sokoni.
Ujenzi wa kiwanda hicho utaongeza fursa za kiuchumi kwa wakulima wa parachichi, ambao kwa sasa wamekuwa wakitegemea wanunuzi binafsi huku baadhi wakilalamika bei ya zao hilo kuyumba.
Tayari Wizara ya Kilimo imemkabidhi mkandarasi Afas Engeneering Limited, eneo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kiwanda hicho ndani ya siku 14 kuanzia sasa.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Julai 14, 2024, Mbunge wa Mufindi Kusini na Naibu Waziri wa Miundombinu, David Kihenzile amesema ujenzi wa kiwanda hicho utasaidia kuinua uchumi wa wakulima wa zao hilo.
Amewataka kuchangamkia fursa kwa kuendelea kuwekeza kwenye parachichi, zao ambalo soko lake ni la uhakika kama ilivyo kwa mazao ya misitu.
“Ni kiwanda kikubwa kujengwa kwenye jimbo letu na hii ilikuwa ahadi ya Rais wetu, Samia Suluhu Hassan. Kazi kwetu kuwekeza kwenye kilimo cha parachichi bila hofu kwa sababu tayari soko la uhakika ni hiki kiwanda,” amesema Kihenzile.
Awali, Mtaalamu aliyekuwa akimwakilisha Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwenye makabidhiano hayo Julai 11, 2024, Florian Kahemela alisema Serikali imekusudia kufungua fursa mbalimbali kupitia sekta ya kilimo likiwemo zao la parachichi.
Amesema mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga kiwanda hicho atatumia siku 180 wakati muda wa matazamio ikiwa ni siku 365 na ameshalipwa malipo ya awali ambayo ni asilimia 15.
“Wanunuzi wa parachichi wapo na wanafuata mpaka shambani lakini tatizo ni bei zao hazitabiriki wakiamua zinapanda na kushuka wakati mwingine zipo juu na wakati mwingine zinakuwa chini. Lakini kuna wakati wanapungua kwa hiyo parachichi zinaharibika, ujio wa kiwanda utatusaidia,” amesema Yusta Nyigu, mkazi wa Nyololo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyololo, Ernest Manga amesema idadi ya wananchi walioanza kulima parachichi imeongezeka baada ya Kihenzile, kuwapa uhakika wa ujenzi wa kiwanda hicho.