ALLIANCE Caravans iliitia adabu Balakshina Foundation kwa ushindi mnono wa mikimbio 64 katika mchezo wa mizunguko 20 uliofanyika jijini Dar es Salaam, Jumamosi.
Alliance ilishinda kura ya kuanza na kutengeneza mikimbio 149, huku ikipoteza wiketi tisa na kuwapa kazi nzito Balakshina kuzifikia alama hizo na kupata mikimbio 80 tu baada ya wote kutolewa.
Kassim Nasoro wa Alliance ndiye alikuwa nyota wa mchezo baada ya kutengeneza mikimbio 36 na kuangusha wiketi mbili za timu pinzani, ikichangiwa pia na Aderah Dileep (mikimbio 27) na Gunesh Giri (21).
“Ilikuwa ni mechi nzuri sana kwetu, kwani kila mmoja alijituma uwanjani,” alisema Kassim ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya kriketi.
Msemaji wa chama cha kriketi nchini (TCA), Atif Salim alisema chama hicho kimeridhishwa na msisimko wa Ligi ya Caravans pamoja na ile ya vijana wa shuleni inayoendelea mkoani Tanga.
Ligi ya Vijana ya TCA iliwapa burudani ya kutosha wakazi wa Tanga mwishoni mwa juma na timu ya wasichana ya Ukombozi ndiyo ilianza kung’ara kwa kuichapa timu ya wasichana ya Gofu Juu kwa wiketi nne.
Gofu Juu ndiyo ilianza kubeti baada ya kushinda kura na kutengeneza mikimbio 41 katika mchezo mfupi wa mizunguko 10.
Matokeo hayo hayakuwapa taabu sana Ukombozi na walizifikia alama hizo kwa kutengeza mikimbio 44 huku wakipoteza wiketi sita.
Katika mchezo mwingine kwa wasichana, Mwang’ombe iliibuka na ushindi mnono wa mikimbio 64 dhidi ya Sahare.
Mwang’ombe ndio walianza kubeti na kupata mikimbio 97 huku wakipoteza wiketi nne, huku Sahare ilishindwa kabisa kufikia idadi hiyo ya mikimbio baada ya wote kutolewa ikiwa na mikimbio 33 tu.