Uongozi wa Simba umefikia makubaliano ya kumwajiri Uwayezu Francois Regis raia wa Rwanda kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, ili achukue nafasi ya Imani Kajula anayejiandaa kumaliza mkataba mwezi ujao.
Kajula ambaye ni mzoefu katika uongozi wa mpira, akiwamo kwenye Kamati ya maandalizi ya Michuano ya Afrika ya vijana chini ya umri wa miaka 17 yaliyofanyika nchini mwaka 2019 alijiunga na Simba kuzipa pengo la Barbara Gonzalez aliyejiondoa Januari mwaka jana baada ya awali kutangaza dhamira Desemba, 2022.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa mazungumzo na Francois yamefika hatua nzuri kilichobaki ni kufikia muafaka wa kumalizana naye ili aweze kuipngoza Simba.
Francois, kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa APR ya Rwanda na amewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka cha Rwanda (FERWAFA).
“Kajula anakamilisha mkataba wake tu ndani ya Simba lakini makubaliano ya kumalizana endapo mkataba ukiisha yamefanyika na ndio maana uongozi umeamua kufanya mazungumzo na Francois ili kuchukua nafasi yake,” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka jina lake litajwe gazetini.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Simba kuwa na CEO kutoka nje ya nchi, kwani awali iliwahi kumuajiri, Senzo Mbatha kutoka Afrika Kusini ambaye baadaye alijiondoa na kutua Yanga kabla ya kurithiwa na Mzambia, Andre Mtine aliyetokea klabu ya TP Mazembe ya DR Congo.
Chanzo : Mwanasport