Gofu na Simba? Serengeti wana jibu

SIO rahisi kuelezea msisimko ambao mcheza gofu ataupata wakati akicheza gofu huku akipishana na makundi ya Simba, Chui au Twiga.

Jibu sahihi litakuwa katika uwanja wa kisasa wa gofu unaoendelea kujengwa katika mbuga za Serengeti na kazi ya kuutengeneza imefikia zaidi ya asilimia 40 sasa, ikiwa ni moja ya mikakati ya ubunifu ya kuboresha michezo na utalii kwa kutumia gofu.

Mpango wa Serekali kupitia Mamlaka ya Mbuga za Taifa(TANAPA) kama ilivyoelezwa na kaimu Kimishina wa uhifadhi, Juma Kuji kwa mwandishi wa jarida la Royal Golf Magazine, ambalo ni mahsusi kwa masuala ya gofu nchini, unatarajiwa kuiingizia nchi kiasi cha Dola 1.803.70 bilioni hadi kufikia mwaka 2030.

Alisema ujenzi wa uwanja huo umebuniwa na Bodi ya Wadhamini ya TANAPA chini ya Mwenyekiti, Generali Mstaafu, George Waitara na utakuwa wa kipekee kwani utajengwa karibu kabisa na hifadhi ya Serengeti ambayo ni moja ya maeneo bora ya kitalii Afrika.

Uwanja huo unafadhiliwa na kitengo cha uwekezaji cha TANAPA kilichotoa  Dola 3.8 milioni (Sh 9.5 nilioni) na ujenzi wake unatazamiwa kukamilika mwaka huu.

Mcheza gofu ya kulipwa mkongwe Salim Mwanyenza ndiye aliyebuni mchoro wa uwanja huu wakati wacheza gofu ya kulipwa, Frank Mwinuka na Bryson Nyenza wakiwa ndiyo waangalizi.

“Uwanja uko eneo zuri na naamini Watanzania na wasio Watanzania watafurahia kucheza gofu Serengeti mara utakapokamilika,” alisema Nyenza jijini Arusha wakati wa michuano ya gofu ya Lina PG Tour.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kitengo cha uwekezaji cha TANAPA na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dr. Richard Matolo alisema ujenzi wa uwanja huo umefanyiwa utafiti wa kutosha ili kuhakisha usalama wa wanyama, watu na mazingira.

Uwanja huu utakuwa na mashimo 18 katika eneo la ekari 400 na utajengwa katika eneo la Fort Ikoma, karibu na Mugumu, wilayani Serengeti.

Ili kucheza mashimo yote 18, mcheza gofu atajikuta ametembea zaidi ya kilomita saba, kati ya hizo, kilomita 3.528 ni za mashimo tisa ya kwanza na kilomita 3.357 ni za mashino tisa ya mwisho.

Related Posts