KAMPUNI YA SUKARI YA KILOMBERO YAUNGANA NA WAPANDA MLIMA KUTOKA NCHI 8 KWENYE KAMPENI YA ‘KILIMANJARO EXPEDITION’ HUKU CHAPA YA BWANA SUKARI IKITARAJIWA KUPANDISHWA KWENYE KILELE CHA MLIMA

 Kampuni ya Sukari ya Kilombero, kwa kushirikiana na wapanda mlima 17 kutoka nchi 8 tofauti wanaoiwakilisha ABF Sugar na Illovo Sugar Africa, wameanza safari ya kupanda mlima Kilimanjaro, kilele kirefu zaidi barani Afrika, kama sehemu ya Kampeni yao ya ‘Kilimanjaro Expedition’.

 Kundi hilo lilianza safari yao asubuhi na mapema siku ya jumamosi kwa kupitia njia ya Rongai, hii ikiwa ni sehemu ya kuheshimu urithi wa Mandela na kuchangisha fedha na kuhamasisha hedhi salama. 

Kila mpanda mlima alichaguliwa kwa uangalifu ikiwa sehemu ya kuonesha ukubwa wa Illovo Sugar, kijiografia, makabila, jinsia, umri, dini, ukubwa kibiashara na kikazi.

Hafla ya kuwaaga wageni hao ilishuhudiwa na Mkuu wa wilaya ya Rombo, Mhe. Raymond Mangwala kwa kushirikiana na wawakilishi kutoka Kampuni ya Sukari ya Kilombero ambao ndio wenyeji wa wageni hao kwa hapa nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mangwala, aliwapongeza wapanda mlima wote kwa kuchagua njia ya Rongai, na kusisitiza urahisi wa njia hiyo kuchukua wapandaji wengi kwa wakati mmoja na urahisi wa kupitika. 

Aidha, Mhe. Mangwala alieleza dhamira thabiti ya Serikali ya kusaidia na kuwezesha sekta ya utalii, kuhakikisha kuna kuwepo na mazingira mazuri na yanayofaa kwa shughuli za utalii. 

Akiwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mh. Mangwala aliwapongeza wapanda mlima hao kwa kutumia Kampeni yao ya ‘Kilimanjaro Expedition’ kuchangisha fedha kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya hedhi salama katika jamii ya watanzania na jamii nyinginezo ambako makampuni hayo yanafanya kazi, hivyo kuonesha dira ya ustawi na maendeleo kwa jamii.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Kampuni ya Sukari Kilombero, Bw. Fimbo Butallah alisisitiza jukumu kubwa la Kampuni hiyo kama nchi mwenyeji katika kuhakikisha wanatangaza na kukuza sifa ya mlima Kilimanjaro.

 Alisisitiza umuhimu wa kuonyesha utofauti na ushirikishwaji kwa ushiriki wa vikundi mbalimbali vya wapanda mlima, katika kuonesha uzuri wa Tanzania kama nchi mwenyeji na Mlima Kilimanjaro kuwa kivutio cha watalii kinachoendana na dhamiri na madhumuni.

Bw. Butallah, alikabidhi bidhaa ya chapa ya ‘Bwana Sukari,’ kwa wawakilishi wawili wa Tanzania kuhakikisha chapa hiyo inafika kileleni mwa Mlima Kilimanjaro ili kuashiria ubora, uwepo wake sokoni, na ukubwa wa bidhaa hiyo juu ya mlima.

 Kampuni ya Sukari ya Kilombero inawatakia kheri wapanda mlima wote, usalama na kuhakikisha wageni wanaifurahia nchi ya Tanzania.

Kwa upande mwingine, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), mshirika mkuu katika Msafara wa Kilimanjaro, ikiwakilishwa na Afisa Utalii Bw. Michael Ndaisaba, inaitazama fursa hii kama lango la kuimarisha vivutio vya utalii nchini na imedhamiria kuunga mkono juhudi zinazofanywa kuimarisha uendelevu wa sekta ya utalii.

Kampuni ya Sukari ya Kilombero ambayo ipo chini ya Illovo Sugar, inabaki kuwa imara katika kukuza ustawi wa jamii kupitia mipango mbalimbali kama huu wa ‘Kilimanjaro Expedition’, wenye lengo la kupambana na hedhi salama ambapo katika kutekeleza ahadi hiyo, kampuni imetoa msaada wa pedi 2400 kwa shule ya Sekondari Mieresini iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro.


Related Posts