WAKATI Ken Gold ikijichimbia Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya kuanza kambi ya kujiandaa na Ligi Kuu msimu ujao, uongozi na benchi la ufundi wameeleza sababu za kujificha huko na matarajio yao.
Timu hiyo ya wilayani Chunya inajiandaa kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, ambapo tayari imemalizana na baadhi ya mastaa huku ikiendelea na usajili kwa ajili ya michuano hiyo.
Baadhi ya waliosaini hadi sasa ni kipa Aaron Kalambo, Ally Ramadhan ‘Kagawa’, Helbet Lukindo, Haji Ugando na Joshua Seleman huku Abdallah Seseme na Abadalah Mfuko wakinukia.
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Benson Mkocha alisema wameamua kutimkia huko kutokana na hali ya hewa kuwa nzuri sawa na ambavyo wangekaa jijini Mbeya na kukwepa muingiliano wa mashabiki.
Alisema kutokana na ugeni wao kwenye Ligi Kuu wameamua wachezaji kuwaficha na kuondoa starehe ambazo hazina afya kwao hivyo matarajio yao katika kambi hiyo ni kutengeneza timu imara.
“Wakiwa mjini starehe ni nyingi na muingiliano ni mkubwa, tumeamua kuwaficha huku ili wajue wapo kazini, pia tumeona kwakuwa Ligi itakuwa kwenye kipindi cha baridi, Tukuyu itakuwa muafaka,” alisema Mkocha.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Fikiri Elias alisema usajili walioufanya wamezingatia mahitaji ya timu na kwamba wameamua kuwa na kikosi cha vijana wanaojitafuta ili kufikia malengo.
“Tumeamua kufanya hivyo kwa sababu kila mchezaji ana ndoto zake, kimsingi ni kutengeneza mbinu na falsafa wakishaingia kwenye mfumo watafanya vizuri,” alisema kocha huyo.