Makalla; Takwimu za maji Dar ziakisi uhalisia wa huduma

Dar es Salaam. Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla ameelekeza zinapotajwa  takwimu za upatikanaji wa maji Mkoa wa Dar es Salaam, ziakisi uhalisia wa upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.

Sambamba na hilo, amesisitiza kila mwananchi katika mkoa huo anaposikia takwimu za upatikanaji wa maji, ajione ni sehemu ya hizo bila kujali eneo alilopo.

Msingi wa kauli ya Makalla ni kile alichofafanua kuwa, wakati mwingine zinatajwa takwimu kubwa za upatikanaji wa huduma ya maji mkoani humo, ilhali wananchi hawaoni huduma hiyo.

Juni mwaka huu, gazeti hili liliandika mfululizo wa ripoti maalumu kuhusu changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji, ikibainisha ukubwa wa tatizo kiasi cha kuwalazimu baadhi ya wananchi kutumia saruji kusafisha maji machafu wanayoyatumia.

Kutokana na ripoti hiyo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alifanya ziara katika mkoa huo na kubaini kile alichokiita uzembe uliokuwa unafanywa na watendaji wa Dawasa.

Kutokana na mazingira hayo Juni 30 mwaka huu, Aweso alimsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu na Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji wa Maji wa mamlaka hiyo, Shaban Mkwanywe.

Kusimamishwa kwao kulitokana na matenki mengi ya maji mkoani Dar es Salaam kutokuwa na maji.

“Hakuna sababu ya msingi ya kukosekana maji Dar es Salaam, kwa sababu vyanzo vya maji vina maji ya kutosha na umeme wa uhakika,” amesema Aweso.

Makalla ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Julai 14 2024 alipotembelea mradi wa tenki la maji la mshikamano, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Dar es Salaam.

“Haya ni maelekezo ya chama kwamba zinapotajwa takwimu za upatikanaji wa huduma ya maji na wakazi wa pembezoni wajihisi kuwa sehemu ya takwimu hizo,” amesema.

Bila kujali eneo alipo mwananchi, amesema ni muhimu kuhakikisha anapata huduma ya maji kama inavyohitajika.

Sambamba na maelekezo hayo, Makalla ameitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), kuhakikisha haisubiri kusukumwa katika utendaji wake.

“Nisingependa kuona mnalazimika kusukumwa na Waziri ( Jumaa Aweso) ndiyo muanze kutekeleza wajibu wenu,” ameeleza.

Maelekezo mengine yaliyotolewa na Makalla ni kuitaka Dawasa kuhakikisha inawaunganishia wananchi maji haraka baada ya kulipia.

“Nilianza kupata malalamiko katika eneo la Wazo na nimesikia mmeanza kugawa vifaa vya kuunganishia maji kwa wananchi ambao tayari wameshalipia.”

“Wananchi wanapolipia kuunganishiwa maji hawapaswi kuchukua muda mrefu kupata huduma hiyo, hakikisheni mnawapatia vifaa na kuwaunganishia huduma haraka,” ameeleza.

Akizungumzia mradi huo, Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu amesema Sh4.8 bilioni zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa tenki hilo.

Tanki hilo, amesema lina ukubwa wa lita milioni sita na linatarajiwa kuhudumia wananchi wa Jimbo la Kibamba.

Sambamba na juhudi zilizofanyika, Mtemvu amesema yapo baadhi ya maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji ikiwemo Kata ya Msakuzi na Mpiji.

“Miradi iliyoandikwa muda mrefu bado haijafika na wengine wamelipia kuunganishiwa maji lakini hilo halijatekelezwa,” amesema Mtemvu.

Sambamba na mradi huo, katika ziara hiyo ametembelea pia Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dar es Salaam, iliyojengwa kwa gharama ya Sh4.4 bilioni.

Akizungumzia mradi huo, Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Voster Mgina amesema ujenzi wa shule hiyo umegharimu Sh4.4 bilioni.

Amesema kukamilika kwa shule hiyo kunaufanya  Mkoa wa Dar es Salaam utakuwa na jumla ya sekondari 74, kati ya hizo 36 zinamilikiwa na Serikali na 38 ni binafsi.

Kwa mujibu wa Mgina, Oktoba mwaka jana shule hiyo ilifunguliwa na hadi sasa ina jumla ya wanafunzi 460 na walimu 26.

Katika ujenzi huo, amesema Sh1.3 bilioni imetolewa na Manispaa ya Ubungo kama mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

“Lengo ni kujenga shule maalumu ya sekondari kwa ajili ya wanafunzi wa kike wanaosoma masomo ya Sayansi na hii inachukua kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita,” ameeleza.

Shule hiyo iliyopo katika eneo la ekari 27, amesema itakapokamilika inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.

Related Posts