MKURUGENZI MKUU NIRC AWATAKA WAKANDARASI KUSAIDIA JAMII MAENEO YA MIRADI – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

MKURUGENZI Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliji (NIRC), Raymond Mndolwa, amewataka Wakandarasi wanaojenga miundombinu ya umwagiliaji kuhakikisha wanasaidia jamii hususani maeneo yenye miradi.

 

Mndolwa amesema hayo katika ziara ya ukaguzi na ufuatiliaji wa ujenzi wa miradi ya umwagiliaji katika kata ya Mwamkulu wilayani Mpanda mkoani Katavi.

 

Katika ziara hiyo alikagua na kutoa maelekezo kwa wasimamizi wa miradi pamoja na Wakandarasi, kuwa lengo la serikali ni kusaidia jamii hivyo pamoja na ujenzi wa miradi wakandarasi waone haja ya kutoa misaada maeneo ya miradi.

 

Aidha ameelekeza mradi wa Mwamkulu, mkandarasi ambaye ni kampuni ya M/S SICHUAN ROAD AND BRIDGE (GROUP) CORPORATION LIMITED ya Dar es Salaam, ambayo ndiyo inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika kata ya Mwamkulu aweze kusaidia ukarabati wa miundombinu ya Msingi ikiwemo nyumba ya muuguzi wa zahanati ya Mwamkulu na kutoa msaada wa vifaa katika shule za msingi zilizopo katika eneo la mradi ndani ya kata ya Mwamkulu.

 

Pia alisema kwa upande wa Tume, itakarabati jengo la kituo cha kutolea huduma za afya kwa wanawake na watoto na nyumba ya Mkunga katika zahanati hiyo ya kata ya Mwamkulu. Katika ziara hiyo Mndolwa ameridhishwa na mwenendo wa kazi za ujenzi na kusisitiza kasi ya kukamilika kwa miradi hiyo kwa muhimu wa makubaliano ili wananchi waweze kunufaika.

 

Naye, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Katavi, Samson Bai, amefafanua kwamba, Miradi ya Umwagiliaji inayoendelea kujengwa katika kata ya Mwamkulu ni pamoja na mradi wa Umwagiliaji Mwamkulu wenye thamani ya Shilingi bilioni 31.6 ambao utanufaisha jumla ya wakulima 1300 pamoja na ukarabati wa skimu ya Umwagiliaji Kabage wenye gharama ya bilioni 23.

 

Aidha ujenzi huo unajuimuisha ujenzi wa mifereji ya kusakafia ndani ya eneo la hekta 3500 kwa upande wa Mwamkulu na mitaro kama hiyo katika eneo lenye ukubwa wa hekta 2500 upande wa Kabage pamoja na ujenzi wa mabanio.

 

Pia, ujenzi wa mradi huo utahusisha ujenzi wa barabara yenye jumla ya urefu wa km 90 ndani ya eneo la mradi na ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao, lenye uwezo wa kuhifadhi tani 4000 za mazao.

 

 

Ukaguzi huo wa miradi ya Umwagiliaji umehudhuriwa na Mjumbe wa Bodi Bi. Anna Mwangamilo pamoja na Wakurugenzi na baadhi ya wakuu wa idara na Vitengo kutoka Makao Makuu ya Tume ya Taifa Umwagiliaji.

Related Posts