MTANDA AKEMEA KAMATI ZA SIASA NA MA-DC ,UPAMBE KWA WAGOMBEA

NA BALTAZAR MASHAKA,ILEMELA .


MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda amewataka wajumbe wa kamati za siasa wakiwemo wakuu wa wilaya(Ma-DC),wasiwe wapambe wa watu kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

Pia watumishi wa umma waweke taswira nzuri ya CCM na serikali kwa wananchi kwani kuchukiwa kwa serikali kunasababishwa na wao waliopewa dhamana ya kuwahudumia.

Aidha kamati za maadili zifanye kazi ya kubaini ukiukwaji wa taratibu na kujadili hali ya kisiasa,kubaini dosari na kudhibiti mambo yanayoharibu hali ya siasa mkoani Mwanza.

Mtanda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,amesema leo alipojitambulisha kwa uongozi wa CCM Wilaya ya Ilemela akisema lengo ni kujitambulisha na kuhimiza ushirikiano kati ya Chama na Serikali.

“Nimekuja kujitambulisha na kuhimiza ushirikiano na uhusiano lakini wanasiasa wana mambo tofauti tofauti wanaweza kutafsiri vinginevyo,Chama ni mdau wa serikali na ushirikiano kati ya Chama na serikali nausisitiza sana, unajengwa na uhusiano bila uhusiano watu hawawezi kushirikiana,”amesema.

Mtanda amesema serikali ya wilaya na Chama vikiwa na mahusiano mazuri mambo yatakuwa sawa,yakiwa mabaya ushirikiano unaosemwa hauwezi kuwepo,hivyo katibu na mkuu wa wilaya ni washirika wanaofanya kazi pamoja.

“Serikali lazima ishirikiane na Chama kinapotengeza ilani serikali inatekeleza,katibu na mkuu wa wilaya waongee lugha moja na kupanga tarehe ya kusoma taarifa ya utekelezaji wa ilani ili wajumbe wapate uelewa na kuwaeleza wananchi,”amesema.

Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu wa Mkoa amewaonya viongozi wasijifanye wenye mamlaka juu ya wananchi kwani wananchi wa sasa wanapaswa kutizamwa kwa jicho la mbali,wakigoma ni vigumu kuwarudisha ni lazima uwepo uhusiano ambao ni muhimu baina ya wananchi na serikali.

“Viongozi wa kisiasa wanapaswa kusaidiwa,wajumbe wa kamati za siasa za wilaya wasiwe wapambe wa watu,kila mjumbe akiwa mpambe na mgombea wake CCM itapoteza,viongozi hawastahili kuwa wapambe wa watu,kazi yao ni kuonesha njia na Ma-DC wana haki ya kuwapa ushirikiano viongozi waliopo madarakani ili kama ni kuanguka waanguke kwa matendo na tabia zao,”amesema Mtanda.

Ameongeza kuwa; “Kamati za maadili lazima zifanye kazi ya kubaini ukiukwaji wa kanuni na taratibu unaofanywa na wanaopita pita kabla ya wakati,kujadili hali ya kisiasa,kubaini dosari na kudhibiti yanayoharibu hali ya siasa,msipofanya hayo tutawatilia shaka kuwa hamuoni macho yamepofushwa kwa rushwa.”

Mkuu huyo wa mkoa amesema viongozi ili washawishi watu lazima wawe na taarifa sahihi ya utekelezaji wa ilani,usalama wa watu na maendeleo kwani wapo baadhi hawaoni maendeleo hayo kwa sababu wana maradhi katika mioyo yao nao wataongezewa.

Amesistiza umuhimu wa uhusiano baina ya wananchi na serikali huku akiwataka watumishi wa umma kutatua changamoto na kudumumisha ushirikiano ili kuisadia CCM kwa sababu kufanya kazi ni ibada si kupata fedha tu.

“Kazi ni ibada hatufanyi ili kupata fedha hata mtaani wakikuona ukiwa mtatuzi wa kero watajua sura ya CCM,hivyo tuweke taswira nzuri ya Chama na Serikali,kwa sababu kuchukiwa kwa serikali kunasababishwa na watumishi waliopewa dhamana taswira zao na utendaji wao,”amesema Mtanda.

Awali Mwenyekiti CCM Wilaya ya Ilemela,Yusufu Bujiku amesema mafanikio na maendeleo yaliyopatikana wilayani humo ni kwa sababu ya ushirikiano uliopo baina ya Chama na serikali.

“Kazi kubwa ya viongozi na wanachama mbali na kukiimarisha Chama ni kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa kushirikiana na serikali.Nia na dhamira yetu kama Chama kazi anazozifanya Rais Dk. Samia na msimamizi wa serikali ni kuhakikisha mitaa yote 172 zikiwemo kata 19 zinaelendelea kubaki,tuna kituo cha kuanzia hatuanzi upya,”alisema.

Bujiku amesema hata fedha za maendeleo zinazotolewa an serikali katika wilaya hiyo wanazifuatilia ili wapate nguvu ya kuzisimamia na kuwaleza wananchi yanayofanywa na serikali yao. “Tunaamini kwa uzoefu wako unaweza kutushauri kama Chama mtusaidie kupata watu wenye sifa watakaowania uongozi kuhakikisha mitaa na kata zote zinabi CCM akiwemo mbunge,tukipoteza mtaa au kata zitakuwa ni fitna na hilo hatutalikubali,”amesema.

 

Related Posts