WAKATI mwingine ni ngumu kuamini, lakini ndivyo ukweli ulivyo. Kuna watu huwa wanakumbwa na majanga, lakini kwa sababu maalumu, hufichwa kwanza ili kutekeleza jambo, kisha huja kuambiwa baadae.
Hivi ndivyo ilivyowahi kumkumba nyota wa zamani wa JKT Oljoro, Mbeya City, Yanga, Mwadui, Lipuli na Gwambina, Paul Nonga ‘Mtumishi’.
Nonga aliyestaafishwa kwa lazima kucheza soka licha ya kuwa na nguvu kutokana na majeraha, amefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti na anaelezea maisha yake baada ya kustaafu, pia maisha ya soka aliyowahi kuyaishi na kusimulia mkasa uliowahi kumfanya acheze mechi ngumu ya ligi akiwa na msiba.
Mbali na mkasa huo, Nonga anasimulia misimu miwili aliyokuwa na Yanga na mikasa aliyokutana nayo, huku akiwataja Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Erasto Nyoni kama wachezaji wa aina yake sambamba na kupanga kikosi bora cha msimu cha Ligi Kuu, huku akiwachomoa nyota wote wa Simba. Ebu endelea naye…!
Nonga anasema hakuna tukio la huzuni litakalobaki kichwani mwake kama lile la kulazimika kucheza pambano la Ligi Kuu Bara kwa dakika zote 90, ilihali baba yake mzazi alikuwa amefariki dunia na hakuna aliyemwambia hadi mchezo ulipomalizika.
Anasema tukio hilo lilimtokea wakati akiichezea Mwadui dhidi ya Yanga Yanga na kama ilivyo mechi yoyote dhidi ya vigogo vya soka, maandalizi na protoko zake huwa ni tofauti kama ilvyowakumba wachezaji karibu wote wa timu hiyo ya Shinyanga.
“Nakumbuka ulikuwa ni mchezo wa Ligi Kuu kati yetu (Mwadui) dhidi ya Yanga, siku moja kabla ya mchezo viongozi walitunyang’anya simu ili kuweka utulivu kwa ajili ya mchezo huo, nakumbuka baba alikuwa mgonjwa hivyo niliwaambia ndugu zangu kama kutakuwa na shida yoyote basi wawasiliane na viongozi,” anasema Nonga na kuongeza;
“Kumbe siku ya mchezo kaka alipiga simu na kuwapa taarifa viongozi, baba yetu alikuwa amefariki dunia na taarifa ilitoka kabla ya mechi kuanza, lakini viongozi wa klabu hawakuniambia kwa vile nilikuwa katika mpango wa kocha na waliamini tayari amefariki dunia, hivyo hata wakiniambia hakuna kitakachobadilika.”
Nonga anasema alikuwa na dakika 90 ngumu sana kwani moyo ulikuwa unamuuma sana kwa kutojua hali ya baba yake kwa vile hakuwa na mawasiliano, ila mara baada ya mchezo ndipo aliambiwa na viongozi hao, wamepokea taarifa ya msiba, hivyo kutakiwa kujiandaa kwa safari.
“Hili ni tukio lililoniumiza na kunitia simanzi na sitalisahau katika maisha ya soka, kwani lilinifanya nicheze dakika 90 nikiwa sipo sawa, licha ya kupambana uwanjani kwa masilahi ya timu, lakini yote ilikuwa mipango ya Mungu na tulishukuru na kuwahi msiba wa mzee,” anasema Nonga.
Mastaa wengi duniani wamekuwa wakistaafu kulingana na umri wao kwenda huku wakikiri kuamua kutundika daruga kutokana na umri kwenda na sababu nyingine, lakini kwa Nonga imekuwa tofauti na alipata maumivu ya nyonga uwanjani bila ya kugongana na mtu.
“Nakumbuka mechi yangu ya mwisho ilikuwa dhidi ya Yanga, wakati nikiwa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, sikugongana na yeyote, lakini ghafla tu nilipata shida hiyo ambayo ilithibitishwa na daktari wa timu,” anasema Nonga na kuongeza;
“Baada ya kubaini shida hiyo iliyotakiwa kufanyiwa upasuaji, lakini kutokana na uwezo wa fedha wa timu niliyokuwepo kipindi hicho kuwa mdogo ikanibidi niendelee kutibiwa mdogo mdogo kitendo ambacho kiliniweka nje ya uwanja kwa muda, ndipo nilipoamua kuingia katika kazi ya ukocha.”
Anasema alifanya mazungumzo na daktari baada ya kumfanyia vipimo vya awali na kumwambia shida ya nyonga na aligundua ilikuwa ndo basi tena kwake kucheza soka, kwani tatizo lilimweka nje kwa muda mrefu.
“Baada ya kuanza matibabu ya awali kadri siku zilivyozidi kwenda nikapata ahueni, ila shida ilikuwa ni kubwa sana hivyo ilinichukua muda mrefu kukaa nje, ndipo niliamua kuachana na soka na kusomea ukocha,” anasema.
Kinachomuuma ni ameondoka uwanjani akiwa na umri ambao bado alikuwa na fursa ya kucheza kwa muda mrefu akitolea mfano kina Kelvin Yondani na wengine hapa nchini wanaoendelea kucheza licha ya kumzidi umri.
Wachezaji wengi wakongwe wameamua kujikita katika ukocha baada ya kuacha kucheza miongoni mwao ni Pato Ngonyani, huku Nonga akisema yupo kwenye mchakato wa kusomea Leseni B ya CAF akisomea nafasi mbili tofauti.
“Leseni B niliyonayo inanifanya niweze kuwa Kocha Mkuu wa Ligi ya Championship, pia nina uwezo wa kuwa kocha msaidizi Ligi Kuu Bara na nina cheti cha ukocha wa viungo na ndio kitengo nilichokabidhishwa Mbeya City kwa sasa,” anasema Nonga na kuongeza;
“Mwanzo nilikuwa naamini ukiamua kuachana na soka kwa sababu umeucheza muda mrefu unaweza kwenda moja kwa moja kuwa kocha, lakini mara baada ya kusoma nimebaini mawazo yangu yalikuwa tofauti kwani kuna utofauti mkubwa sana kufundisha bila kusoma na ukisoma.”
Nonga anasema malengo yake makubwa ni kufikia mafanikio ambayo yamefikiwa na baadhi ya makocha waliomtangulia huku akiweka mipango ya kutaka kufundisha timu nje ya Tanzania.
“Malengo yangu ni kuweka rekodi nzuri ndani, kitu ninachoamini katika mipango, ndivyo itakayonifanya nitokea Tanzania na kwenda kufundisha nje kutokana na ubora nitakaouonyesha.”
“Ninavyosema naamini katika mipango namaanisha kwa kuanza kubadilisha mafanikio niliyoyapata kwenye soka nikicheza na kuwa katika ufundishaji na hatua niliyopo sasa ni kuwekeza nguvu kwa kufanya vizuri ndani.”
“Emmanuel Kimbe ambaye alikuwa ni mtendaji mkuu wa Mbeya City ndiye aliyenishawishi niingie kwenye masuala ya ukocha na ndiye aliyelipia kozi zangu za awali.
“Mtu mwingine ni Peter Matoli ambaye kwa sasa yupo Marekani, huyu pia alikuwa akinisisitiza mimi kuingia kwenye masuala ya ukosa na kadri siku zinavyozidi kwenda na mimi naendelea kuwa bora eneo hilo,” anasema.
Nonga anasema pia hata kwa upande wake mwenyewe aliamua kuchagua kusomea ukocha kuliko kuendeleza fani aliyosomea ya madini kwani aliamini soka ndilo litakaloweza kumtengenezea muunganiko na watu wengi.
Licha ya kuishusha Mbeya City kocha mwenye leseni A ya CAF, Abdallah Mubiru ametajwa na Nonga ni mmoja wa makocha wanaomvutia kutokana na mbinu zake za ufundishaji.
“Nafikiri mpangilio wake wa mazoezi na namna ya kumfundisha mchezaji mmoja mmoja najiona kabisa mfumo wangu na wa kwake vinaendana na nilikuwa navutiwa na utendaji kazi wake,” anasema na kuongeza;
“Mbali na Mubiru pia Juma Mwambusi ni miongoni mwa makocha wanaoendana na utendaji kazi wangu tangu nimeingia kwenye sekta ya ukocha,” anasema.
Akizungumzia mfumo anaopenda kuutumia mshambuliaji huyo wa zamani wa City, Mwadui na Yanga amesema anapenda kutumia 4-2-3-1, pia amekuwa akibadilisha kutokana na aina ya mpinzani anaetarajia kukutana naye.
“Tayari nimeshakuwa kocha, sasa najiona kabisa naendana nao kwenye mifumo na aina ya ufundishaji wangu, kuhusu mfumo huwa nabadilika kulingana na aina ya mpinzani ninaekutana naye, ili kutengeneza mfumo mzuri lazima umsome mpinzani ili uweze kuwa na ushindani,” anasema.
Kelvin Yondani ni beki mkongwe ambaye anakipiga Geita Gold ambayo imeshuka daraja msimu huu. Licha ya kucheza soka kwa muda mrefu na umri wake kwenda, lakini bado amekuwa ni miongoni mwa mabeki bora kama anavyothibitisha Nonga.
“Nimecheza mechi nyingi za ushindani na nimekutana na mabeki wengi lakini kwangu tishio na aliyekuwa ananisumbua nikikutana na timu yake ni Kelvin Yondani. Alikuwa anapambana kuhakikisha sifungi na mimi nilikuwa napambana kuhakikisha nafunga mbele yake,” anasema na kuongeza;
“Yondani ana nidhamu nje na ndani ya uwanja, ndiyo sababu anaendelea kucheza hadi sasa na ni mchezaji ambaye nipo naye karibu kila tulipokuwa tukikutana, kulikuwa na bato kubwa kati yetu, hii ni kwa sababu tumeanza kusaka maisha ya soka pamoja kutoka madaraja ya chini,” anasema Nonga ambaye alitaja tukio lake bora na nzuri kwenye maisha yake ya soka ni siku akiwa Lipuli FC walikutana na Yanga mechi ya nusu fainali wakashinda mabao 2-0 alifunga bao moja na kutoa pasi iliyozaa bao lililofungwa na Daruweshi Saliboko.
Mchezaji hadi upate nafasi ya kucheza soka la ushindani kuna changamoto nyingi lazima uzipitie ndio utoboe, kama ambavyo anathibitisha Nonga alishawahi kuamua kuachana na soka na kutumikia kazi ya uchimbaji madini aliyoisomea kutokana na kushindwa kupanda timu za madaraja ya juu.
“Nakumbuka kuna muda niliamua kuachana na soka na kurudi Mwadui sehemu ya uchimbaji madini, hii ni baada ya kuona wachezaji wenzangu ambao tulikuwa pamoja na kucheza pamoja wanafanikiwa mimi nabaki pale pale,” anasema na kuongeza;
“Tukiwa Mwanza kuna timu ya madaraja ya chini nilikuwa na Jerrson Tegete, Mrisho Ngasa na Kelvin Yondani, wenzangu walifanikiwa mapema lakini mimi waliniacha timu za chini, niliamua kutangaza kuacha kucheza soka na kurudi Mwadui,” anasema Nonga ambaye ametaja siri ya kuvaa jezi namba 13 mgongoni kuwa ni kutokana na kuwa na mapenzi na mchezaji wa zamani wa Chelsea timu anayoishabikia Michael Ballack.
Anasema alipofika Mwadui sehemu ya machimbo alikuta kuna timu, hivyo kutokana na mapenzi na mchezo huo pamoja na kutangaza kutokucheza tena akajikuta anazamia huko na kuanza kucheza timu hiyo ikiwa madaraja ya chini na ndiyo iliyomfanya akaonekana na kusajiliwa Rhino Rangers.
“Niliamua kuacha kazi Mwadui na kujiunga na Rhino ambayo ilinifanya nikajulikana na kutua JKT Oljoro iliyokuwa imepanda Ligi Kuu Bara, hiyo ndio timu ilinifanya nicheze ligi na ndipo Juma Mwambusi aliponiona akaniita nikasajiliwa na Mbeya City baadae nikarudi Mwadui nikacheza nusu msimu,” anasema.
TIBOROHA ALIMPELEKA YANGA
Hakuna mkate mgumu mbele ya chai, hivyo ndivyo unaweza kusema baada ya Nonga kukiri kupokea simu ya aliyekuwa katibu mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha kumhitaji kujiunga na Yanga.
Licha ya kutokuamini ni kweli, hakusita kutimka Mwadui na kujiunga na timu hiyo yenye maskani yake Jangwani.
“Baada ya kucheza miezi sita tu Mwadui nilipigiwa simu na Tiboroha, mwanzo nilifikiri ni michezo ya wenzangu kujaribu kunitingisha, lakini akapiga tena na kusisitiza kunihitaji, nikamjibu nina mkataba na Mwadui, lakini kauli yake ilikuwa ni moja tu, usijali kuhusu hilo wewe njoo Dar es Salaam, nikakubali wakatuma tiketi ya ndege nikatua mjini na kufanya makubaliano nikasaini mkataba,” anasema na kuongeza;
“Baada ya kusaini mkataba nikarudi Mwadui kuwaaga wenzangu, lilifanyika sherehe kwa kununua makreti ya soda ambayo nakumbuka wachezaji walipata soda mbili mbili kila mmoja,” anasema Nonga.
KUNYOLEWA NYWELE BILA KUJUA
Kwenye soka kuna matukio mengi lakini mara nyingi bora ndio yamekuwa yakizungumzwa, huku matukio tata ya kisahaulika. Mwanaspoti limepata nafasi ya kusimuliwa tukio tata alilowahi kukutana nalo Nonga kwenye maisha yake ya soka.
“Nakumbuka mara baada ya kuwathibitishia wachezaji wenzangu naenda kucheza Yanga nilikumbwa na tukio tata ambalo bila mchezaji mwenzangu kunisaidia hadi leo nisingeweza kufahamu, nilinyolewa nywele kwenye mazingira ambayo hata mimi siyafahamu nilijikuta tu sina nywele kichwani,” anasema na kuongeza;
“Emmanuel Memba ndio alibaini sina nywele kichwani na ndio ilikuwa sababu ya mimi kuanza kunyoa kipara nilidumu na staili hiyo ndani ya miezi mitatu baada ya nywele kuanza kuota sehemu ambayo nilinyolewa,” anasema.
Kipindi anatua Yanga, mshambuliaji huyo alikutana na pacha ya Amis Tambwe na Donald Ngoma msimu ambao wachezaji hao walikuwa bora na alipata ugumu wa kuingia kikosi cha kwanza.
“Kwa muda ambao nilikuwa nikiupata nilikuwa nautumia vyema lakini sikuwa na uhakika wa kucheza mara kwa mara, nikaamua kuiandikia timu barua kuomba kuondoka, kila mmoja alihamaki kwani hawakutarajia kama nitaondoka kwani kipindi hicho kulikuwa na marehemu Yusuf Manji lakini niliamua kuondoka.”
“Niliandika barua kuomba kuondoka kutokana na kuwa na nafasi ndogo ya kucheza na mimi nilikuwa na hamu ya kuona nacheza, nashukuru Mungu waliridhia kuniacha na niliomba wanipeleke Mwadui FC timu ambayo nilitoka wakati natua Yanga na walifanya hivyo,” anasema Nonga ambaye amethibitisha akiwa ndani ya timu hiyo wakiwa wanajiandaa kucheza na Yanga walikuwa wanafanya maandalizi ya nguvu tofauti na kucheza na timu nyingine.
AMEWACHAMBUA SURE BOY, NYONI
Tanzania imebarikiwa kuwa na viungo wengi tofauti na eneo la ushambuliaji, Nonga amethibitisha hilo huku akimtaja Abubakar Salum ‘Sure Boy’ kuwa ni kiungo bora kwake kutokana na kurahisisha mambo mengi uwanjani akiwa eneo la kiungo huku akimtofautisha na mkonge Erasto Nyoni ambaye pia amekiri ni bora na anamuofa kocha vitu vingi uwananji.
“Sure Boy ni bora ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi na kuchezesha timu na ndiyo maana hadi muda huu anaendelea kucheza na ni mmoja wa viungo bora ambao tumebarikiwa nao kwenye nchi yetu, haina maana waliopo wengine hawana uwezo ila kwangu huyo ni bora,” anasema na kuongeza;
“Kwa upande wa Nyoni ni mchezaji ambaye anaweza kukupa vitu vingi uwanjani, unachagua mwenyewe umtumie eneo gani na kila utakapompanga atafanya kitu sahihi na bora kitu ambacho ni tofauti na Sure Boy ambaye ubora wake ni eneo moja uwanjani,” anasema Nonga ambaye amekiri ujio wa mastaa wa kigeni kwenye soka la Tanzania unaongeza chachu ya ushindani kwa wazawa kupambana ili waweze kupata nafasi ya kucheza huku akiomba timu zinazoleta mastaa hao wa kigeni zilete mastaa bora watakaoweza kutoa ushindani na sio kuleta wachezaji wanaocheza miezi mitatu au minne wanatimumliwa.
Licha ya kwamba Nonga hajacheza kabisa ligi msimu huu, lakini amekuwa akishuhudia mechi za Ligi Kuu Bara kutokana na mapenzi aliyonayo kwa mchezo huo na hapa anakitaja kikosi chake bora kwa msimu ulioisha, huku akiwachomoa nyota wote wa Simba, akimbakisha Chama aliyehamia Jangwani.
Anasema hicho ni kikosi kwa mtazamo wake kwa namna wachezaji walivyokimbizana msimu mzima na mawazo yake yaheshimiwe, hata kama yatawakera wengine.
Nonga ametaja kikosi hicho kikiwa na Diarra Djigui langoni, akisaidiwa na Yao Kouassi wote wa Yanga, David Luhende (Kagera Sugar), Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho (wote Yanga), Clatous Chama, Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki (wote Yanga), Sixtus Sabilo (JKT Tanzania) na Joseph Guede (Yanga).
Alikopita: JKT Oljoro, Mbeya City, Yanga, Mwadui, Lipuli, Gwambina, Mbeya City
35 Umri alionao Nonga ambao bado ulikuwa unampa nafasi ya kuliamsha ila majeraha yalimstaafisha.
2011 Mwaka alioanza kucheza soka akianzia JKT Oljoro kabla ya kudakwa na Mbeya City
2016 Mwaka ambao Nonga alijiunga na Yanga na kuitumikia kwa misimu miwili tu
2022 Mwaka ambao Nonga alistaafu soka akiwa na Mbeya City kisha kugeukia ukocha.