TANGU mara ya mwisho kufanya kile ambacho waliweza kufanya na kuandika jina lao katika historia, Uingereza imeongozwa na Mawaziri Wakuu 14. Ilikuwa mwaka 1966. Ni miaka 58 sasa. Tanzania ilikuwa ina miaka mitano tu tangu ipate uhuru.
Timu ya taifa ya England ilitwaa Kombe la Dunia pale England mwaka 1966 kwenye Uwanja wa Wembley. Haijawahi kutwaa tena taji kubwa lolote la soka. Na hata kabla ya hapo walikuwa hawajahi kutwaa taji lolote kubwa la soka. Kile kikosi chao cha Kombe la Dunia mwaka ule katika kikosi cha kwanza kilichoanza dhidi ya Ujerumani amebaki mchezaji mmoja tu ambaye yupo hai. Sir Geoff Hurst.
Wengine wote wamefariki. Aliyefariki karibuni ni Sir Bobby Charlton. Wamemuacha hai rafiki yao kipenzi, Sir Geoff Hurst ambaye katika pambano la fainali dhidi ya Ujerumani Magharibi alifunga hat-trick. Ilibakia kuwa hat- trick pekee ya mechi ya fainali la Kombe la Dunia hadi mwaka 2022 pale Qatar wakati Kylian Mbappe alipoifungia Ufaransa hat-trick dhidi ya Argentina, ingawa Les Bleus hawakutwaa ubingwa.
Kesho Waingereza wanarudi tena katika fainali ya michuano mikubwa. Wanacheza fainali ya Euro dhidi ya Hispania. Fainali yao ya pili mfululizo baada ya kupoteza ile ya miaka minne nyuma. Ni fainali yao kubwa nyingine. Huwa zinatokea mara chache katika soka lao ingawa ni wapiga kelele maarufu.
Wanaingia katika Uwanja wa Olimpiki pale Berlin kucheza dhidi ya Hispania. Uwanja huu wa Olimpiki Berlin ndio ambao mwaka 1936 ulimuacha mdomo wazi Dikteta Adolf Hitler wakati mwanariadha mweusi wa Marekani, Jesse Owens alipotwaa medali nne za dhahabu katika Michezo ya Olimpiki.
Ilikuwa zama zile za ubaguzi uliotopea, lakini hadi leo ubaguzi upo. Na katika kikosi kile cha kina Charlton wakati ule hakukuwa na mtu mweusi. Kesho Waingereza wanaingia uwanjani wakiwa na wachezaji kibao weusi ambao ni mashujaa wa timu. Nyakati zimekwenda wapi?
Kina Bukayo Saka ambaye aliipeleka timu nusu fainali. Kina Ollie Watkins ambaye ameipeleka timu fainali. Kina Kyle Walker. Vipi kuhusu bwana mdogo fundi, Kobbie Mainoo. Mtoto wa wazazi kutoka Ghana. Ili mradi tu nyakati zimebadilika.
Waingereza wana jukumu moja tu. Kutwaa ubingwa. Nje ya hapo watakuwa wamefeli tena. Walishawahi kufika nusu fainali Italia mwaka 1990 katika Kombe la Dunia. Paul Gascoigne ‘Gazza’ alionyeshwa kadi ya pili ya njano na akawa anacheza, huku akilia akiamini kwamba ameikosa mechi ya fainali dhidi ya Argentina. Haikuwezekana. Waliishia hatua hiyo hiyo ya nusu fainali.
Wakarudi tena katika Euro ya kwao mwaka 1996 walipoishia nusu fainali. Wakaenda tena nusu fainali ya Kombe la Dunia pale Russia mwaka 2018. Wakatupwa nje. Wakaenda fainali ya Euro miaka minne iliyopita. Hakuna walichoambulia. Na sasa wanarudi kufanya ushujaa wa Jesse Owens. Wataweza? Hatujui.
Watu wengi wanaipa nafasi Hispania. Wamecheza vema michuano hii. Wana watoto wawili kule pembeni ambao wana akili nyingi. Lamine Yamal na Nico Williams. Nilimzungumzia Nico wikiendi iliyopita. Nitamzungumzia Yamal siku chache zijazo.
Bado shilingi yangu imesimama katikati. Haitakuwa mechi rahisi sana. Waingereza wana wachezaji wengi ambao wanajua kukaa na mpira katika nyakati hizi kuliko wakati mwingine wowote ule. Kawaulize Wadachi katika pambano lile la Jumatano usiku pale Dortmund watakwambia ukweli.
Hawa watoto walio nao ambao wanaweza kukaa na mpira na kuufanya watakavyo wapo wengi kwa sasa kuliko zile zama za kina Paul Scholes. Kwa Kiingereza kitamu huwa wanaitwa ‘Ballers’. Mainoo anajua kukaa nao. Declan Rice anajua kukaa nao. Saka anajua kukaa na mali. Fundi Jude Bellingham anajua kukaa na mali. Phil Foden hauhitaji kusema, anajua kukaa na mali. Walker anajua kukaa na mali. Cole Palmer anajua kukaa na mali. Karibu kila mchezaji anajua kukaa na mali. Wengine wamewaacha nyumbani na wanajua kukaa na mali. Kina Marcus Rashford, Jack Grealish, Jadon Sancho na wengineo kibao.
Haitakuwa mechi rahisi pia kwa sababu watoto wengi wa Kiingereza sio tu kwamba wanaweza kuweka mali mguuni, lakini wanacheza pia katika timu za viwango vya juu ambazo zinafundishwa na makocha wa kisasa. Wengine wanatoka katika taifa hilo hilo ambalo wanacheza nalo kesho.
Kuna watoto wa Pep Guardiola na watoto wa Mikel Arteta. Kuna vijana wa Jurgen Klopp kina Trent Alexander Arnold nao wapo humo humo. Pengine kwa sasa Waingereza wanapitia katika nyakati bora kuliko wakati mwingine wowote katika miaka ya hivi karibuni.
Pambano dhidi ya Hispania ni pambano la kufa au kupona kwao. Sina ushabiki. Sitaki kuwazungumzia sana Wahispaniola kwa sababu historia inaonyesha hawana cha kupoteza sana katika miaka ya hivi karibuni. Walikuwa katika ardhi ya Nelson Mandela wakitwaa Kombe la Dunia miaka 14 iliyopita. Baada ya hapo wakatwaa Euro. Vipi kuhusu ambao hawajatwaa taji lolote kubwa kwa miaka 58 iliyofuata? Hawa wachezaji waliotwaa taji lile wamekufa. Wamemuacha Sir Geoff Hurst tu akisubiri kutazama kama kuna timu nyingine inaweza kufanya hivyo.
Hapa katikati wamepita wengi. Kina Gary Lineker. Kina Gazza na Alain Shearer. Kina David Platt. Tony Adams. Halafu kikaja kizazi cha kina Wayne Rooney na rafiki zake Steven Gerrard, Paul Scholes, Frank Lampard. Walionekana kama vile ni kizazi cha dhahabu, lakini hawakufanya chochote zaidi ya kuwatia aibu Waingereza ambao wanasifika kwa kelele nyingi za vyombo vya habari.
Tusubiri na kuona kesho pale Berlin. Huenda historia mpya ikaandikwa. Hatuwezi kujua. Kama kina Saka wataweza kufanya hivyo, basi watakuwa wameinua mioyo ya Waingereza wengi ambao imekufa kwa kipindi cha miaka 58 iliyopita. Twendeni Berlin.