KIUNGO mkabaji mpya wa Simba, Mnigeria Augustine Okejepha amesema amefurahishwa na maandalizi ya timu hiyo yanayoendelea kambini, Ismailia Misri, huku akiweka wazi kila mchezaji kwa sasa anaonyesha anataka kukipambania kikosi hicho msimu ujao.
Nyota huyo aliyejiunga na Simba akitokea Rivers United ya Nigeria, alisema licha ya ugeni wake ndani ya timu hiyo na kutozoeana na wachezaji wenzake ila amefurahia namna walivyompokea jambo linalompa imani mbeleni.
“Najisikia kama nipo nyumbani kwa sababu nimepokelewa vizuri na wenzangu jambo linalonipa furaha moyoni mwangu, kiukweli maandalizi ni mazuri na wachezaji wote wameonyesha ni kwa jinsi gani msimu ujao tunataka kufanya vizuri zaidi,” alisema.
Okejepha aliyewahi kuchezea Kano Pillars aliyojiunga nayo akitokea Warri Wolves FC zote za Nigeria, aliongeza, tangu wameanza mazoezi kwa ajili ya msimu mpya, ari imekuwa ni kubwa kuanzia wachezaji, benchi la ufundi na viongozi.
“Kila kitu kinaenda vizuri na viongozi wamekuwa nasi bega kwa bega kuhakikisha tunatoa kilichokuwa bora kwa mashabiki zetu, naamini msimu ujao utakuwa ni mzuri na jambo linalonipa kiburi ni jinsi kila mmoja wetu anavyoonyesha mazoezini.”
Nyota huyo mwenye miaka 20, alisema, haikuwa rahisi kuikataa ofa ya FC Ural Yekaterinburg kutoka Urusi inayoshiki Ligi Daraja la Kwanza iliyomuhitaji kwa sababu alihitaji kufuata nyayo za mastaa wakubwa kutoka Nigeria walioichezea Simba.
“Wapo wachezaji wengi kutoka Nigeria ambao walipita au wapo hadi sasa hivi katika soka la Tanzania kama, Nelson Okwa, Victor Akpan, Benjamin Tanimu na Morice Chukwu, hivyo nami nilipenda kuona nikiwa sehemu kama hiyo pia.”
Nyota huyo ameonyesha kiwango bora akiwa na Rivers United ambapo ameiwezesha kumaliza msimu ikiwa nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu ya Nigeria (NPFL) na jumla ya pointi 53, baada ya kushinda michezo 15, sare minane na kupoteza 15.
Katika ligi hiyo, Enugu Rangers imetwaa ubingwa baada ya kushinda jumla ya michezo 21, sare saba na kupoteza 10 na kukusanya pointi 70, nyuma ya Remo Stars iliyoshika ya pili na pointi 65, huku Enyimba ikimaliza ya tatu na pointi 63.