Polisi yakiri kumshikilia Kada Chadema aliyedaiwa kutoweka kwa siku 29

Tanga. Siku 29 tangu kada wa Chadema, Kombo Mbwana (29) atoweke, Polisi Mkoa wa Tanga limesema linamshikilia kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mtandao. 

Kombo mkazi wa Komsala wilayani Handeni, aliripotiwa kutoweka tangu Juni 15, 2024.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari leo Jumapili Julai 14, 2024 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zacharia Bernard amesema Kombo anatuhumiwa kutumia vifaa vya kielektroniki na laini za simu za mitandao mbalilmbali zisizo na usajili kutekeleza uhalifu huo kinyume cha sheria za nchi.

Amesema upelelezi wa matukio hayo umefikia hatua nzuri na wakati wowote mtuhumiwa atafikishwa mahakamani. Anadaiwa kutenda makosa hayo kwenye mikoa tofauti.

Kada wa Chadema, Kombo Mbwana 

Amesema Jeshi hilo linatoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo ni kosa kisheria.

Mariam Rajabu (20), mke wa Kombo alizungumza na Mwananchi hivi karibuni alieleza alipokuwa anafanya usafi nyumbani kwao alifika mtu aliyehoji ni nani anayejenga msingi wa nyumba, alimjibu ni mama na mume wake.

Alidai maswali yalipokuwa mengi, alimuita mume wake aliyekwenda kumsikiliza.

Kwa mujibu wa Mariam, mtu huyo alimweleza mumewe kuwa eneo hilo ameuziwa pamoja na shamba na kama atahitaji kuona nyaraka, waende kwenye gari lililokuwa limeegeshwa jirani na nyumba yao akazione.

“Basi wakaondoka kuelekea kwenye gari huku wakionyeshana eneo na alipoingia tu kwenye gari, nilishtuka kuona gari hilo linaondoka kwa kasi,” alidai na tangu wakati huo hakumuona tena.

“Naiomba Serikali imtafute mume wangu wapi alipo nijue, nina mtoto mdogo ambaye anahitaji huduma nyingi na baba yake ndiyo alikuwa kila kitu,” alisema Mariam.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Komsala, Joseph Minango alisema hana taarifa kama shamba la Kombo limeuzwa kama ilivyodaiwa na mtu aliyeondoka naye.

Awali, Katibu wa Chadema Jimbo la Handeni Mjini, Kombo Matulu alisema wamefuatilia sehemu mbalimbali lakini hawajapata majibu yupo wapi.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando alisema tukio hilo lipo kwenye uchunguzi chini ya Jeshi la Polisi na aliwaomba wanafamilia na wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikilishughulikia.

“Serikali haijawahi kushindwa jambo, nawaomba tuwe watulivu,” alisema Msando.

Related Posts