Washington. Rais Joe Biden amelaani jaribio la mauaji dhidi ya Rais wa zamani Donald Trump kwenye mkutano wa hadhara, akisema kuwa hakuna nafasi ya ghasia za kisiasa nchini Marekani
“Huu ni ugonjwa,” amesema. “Hatuwezi kuruhusu hili litokee. Hatuwezi kuunga mkono hili.”
Biden amesema alijaribu kumpigia Trump, lakini alikuwa na madaktari wake. “Inaonekana anaendelea vizuri,” amesema.
Ofisa wa Ikulu ya Marekani amesema baadaye kuwa Biden alikuwa amezungumza na Trump, Gavana wa Pennsylvania, Josh Shapiro na Bob Dandoy, meya wa Butler, Pennsylvania, ambapo mkutano huo ulifanyika. Hakuna maelezo ya yaliyotolewa kuhusu mazungumzo hayo.
Trump alikimbizwa kutoka jukwaani baada ya milio ya risasi kusikika alipokuwa akizungumza na wafuasi wake kwenye mkutano huko Butler, karibu na Pittsburgh. Alionekana kuwa na damu sikioni na usoni.
Mtu mwingine kwenye mkutano huo, ambaye maofisa hawajamtaja jina, aliuawa kwenye shambulio hilo na mwingine alikuwa katika hali mbaya.
Shambulio dhidi ya Trump lilikuja siku chache kabla ya kukubali rasmi uteuzi wa kuwa mgombea urais katika mkutano wa kitaifa wa chama cha Republican huko Milwaukee.
Biden, ambaye anashindana tena na Trump, ambaye alimshinda mwaka 2020, amesema Trump alipaswa kuwa na uwezo wa kufanya mkutano wake “kwa amani, bila tatizo lolote.”
Biden amekatisha safari yake ya mwisho wa wiki kwenda Delaware na kuelekea Ikulu baada ya shambulio hilo dhidi ya Trump. Biden alikuwa amepanga kutumia mwisho wa wiki kwenye nyumba yake ya ufukweni huko Rehoboth, kisha kusafiri Jumatatu kwenda Texas kutoa hotuba kuhusu haki za kiraia na demokrasia katika Maktaba ya Rais ya LBJ huko Austin.
Badala yake, Biden aliondoka Rehoboth Jumamosi usiku na kufika Ikulu mapema Jumapili asubuhi.