Sababu ya Waziri Jr kuifunga Simba hii hapa

KUIPAMBANIA ndoto si kazi nyepesi. Njiani kuna uwezekano wa kukutana na milima na mabonde, lakini jambo la msingi ni kuamini siku ya kicheko inakuja, kama anavyosimulia mshambuliaji Waziri Junior jinsi ambavyo aliwahi kupata uchungu uliomfanya aweke nadhiri kwa Mungu.

Junior anasema kila mchezaji ana historia ya alipotokea hadi kufikia hatua ya kujulikana mbele ya jamii, akiamini yapo ya kujifunza kutokana na hatua za mafanikio yao.

“Mfano mzuri wengi wanapenda wanachokifanya mastaa wa nje kama Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Kylian Mbappe na wengine wengi, ila nyuma yao kuna hatua walizopitia, zipo za kuumiza na kufurahisha, lakini mwisho wa yote kilichowafanya vipaji vyao vionekane kwa ukubwa, hawakuruhusu kukata tamaa.

“Kuna nyakati nimewahi kupitia, hadi nikawa nawaza kwamba labda kuna sehemu nimekosea, ila kuna siku niliamua kukaa chini na kufanya uamuzi wa kuhakikisha sikubali kipaji changu kipotee.”

Junior haifungi Simba kwa bahati mbaya, bali ni dhamira aliyoiweka Septemba 2013 akiwa anatoka katika geti la Uwanja wa Kinesi uliopo Shekilango jijini Dar es Salaam.

Maneno yanaumba kama anavyosimulia Junior kwamba: “Nilitoka kufanya majaribio katika kikosi cha Simba B. Kuna maneno niliambiwa ambayo yaliniumiza sana moyo. Kabla ya kulivuka geti la Uwanja wa Kinesi nilisema Mungu nifungulie milango ya kupata timu ili nikija kukutana na Simba niwe naifunga.

“Siwezi kusema ni maneno gani na niliambiwa na nani. Ila kwa mara ya kwanza kucheza Ligi Kuu ilikuwa 2015 nikiwa na Toto Africans, bao pekee nililoifunga Simba liliiathiri ikakosa ubingwa na taji likaenda kwa Yanga.

“Nikiwa na Mbao FC niliifunga Simba mabao mawili, KMC mabao mawili hivyo nimeifunga jumla ya mabao matano ukijumlisha na la Toto Africans. Nitaendelea kuifunga hadi Mungu atakapoamua nisiifunge. Pia mashabiki wajue Yanga nimeifunga kama ninavyoweza kuzifunga timu nyingine.” 

Yanga ilimsajili Junior akitokea Mbao FC na timu ilikuwa chini ya kocha Cedrick Kaze, ambapo awali alishindwa kupata nafasi, lakini baada ya ujio wa Nasreddine Nabi akawa anacheza baadhi ya mechi na kukaa benchi.

“Nilisajiliwa Yanga wakati kocha ni Kaze nilicheza mechi moja. Baada ya kuja Nabi nikawa napewa dakika chache za kucheza na pia nilikuwa nakaa benchi, hivyo jibu sahihi kilichonifelisha ni kukosa nafasi ya kucheza,” anasema.

Anafichua pia alichoambiwa na Nabi kwamba alikuwa anapenda ushambuliaji wake wa kutokea nyuma ya mabeki.

Anakiri kuona mashabiki mitandaoni wakimsema akienda timu kubwa anashindwa kuonyesha uwezo wake, lakini anataka wafahamu jambo moja, kuna ugumu kwa wazawa thamani zao kufanana na wageni ndani ya klabu hizo.

“Kitu kigumu kwa mchezaji ni kutokucheza, hali hiyo inaweza ikamtoa mchezoni, lakini ninawashauri wanaobahatika kusajiliwa katika klabu hizo, waongeze juhudi ya mazoezi na kuhakikisha wanawashawishi makocha ili wapangwe na kuonyesha uwezo wao,” anasema.

Msimu uliopita kwake ulimfungulia milango mingi baada ya kufunga mabao 12, akaanza kutakiwa na timu mbalimbali za ndani na nje.

“Japokuwa siwezi kukutajia nitacheza wapi hadi sasa hivi, lakini kitu kikubwa baada ya kufanya vizuri, makocha wa timu za Taifa Stars, Hemed Morocco na Juma Mgunda kuniamini tena kunijumuisha katika kikosi pia walinishauri nihakikishe najiunga na timu ambayo nitakuwa napata nafasi ya kucheza.

Anaongeza: “Siwezi kumsahau kocha wa KMC, Abdihamid Moalin, aliniambia maneno ya kunijenga ambayo yalikuwa yananipa nguvu ya kujituma kwa bidii bila kukata tamaa.”

Ukiacha ufundi wake uwanjani, Junior humwambii kitu kuhusu kupika, anataja vyakula anavyoweza kuvipika ni ugali, pilau, wali, chapati, tambi na mboga za kila aina.

“Nikikupikia chakula, utatamani niwe nakupikia kila wakati, mimi ni mtu wa Tanga lazima nijue mapishi, ungenikuta nyumbani ningeonyeasha kwa matendo kwa maana ya maandalizi ya chakula kimoja wapo,” anasema Junior ambaye kifo cha wazazi wake kimemuachia machungu moyoni.

Anawataja mabeki anaowakubali ni Bakari Mwamnyeto (Yanga), Kelvin Yondani (Geita Gold) na Pascal Wawa aliyecheza Azam FC na Simba. “Aina ya uchezaji wao ni wa utulivu, wanatumia akili na ni viongozi dhidi ya wengine, wakiwepo ukuta wao si mwepesi kuupita.

Anaongeza: “Mbali na mabeki hao, mshambuliaji ninayemkubali ni John Bocco, bado ana vitu vya kuonyesha uwanjani, naamini huko JKT Tanzania alikokwenda atafanya makubwa, sisi wengine tunapaswa kujifunza kutoka kwake.”

Mwanaspoti liliona vidole viwili vya Junior akiwa amepaka hina kucha zake, alipoulizwa ina maana gani kwa upande wake, alikuwa na haya ya kujibu: “Kwa imani yangu kupaka hina ni sunna, pia jambo la pili nikiwa naipaka huwa napenda sana kuisikia harufu yake,” anasema Junior ambaye anakiri soka limemlipa ingawa hakutaka kutaja vitu alivyovipata kupitia mchezo huo.

Related Posts