MAUMIVU ya kushuka daraja kwa Mbeya yameanza kuuma baada ya uongozi kukiri kupata hasara ya Sh1 bilioni kwa mwaka, huku ikiapa kuwa msimu ujao wa 2024/25 ndio mwisho wa kucheza Championship.
City ilishuka daraja msimu wa 2022/23, ambapo msimu uliopita ilishindwa kupanda tena ilipomaliza katika nafasi ya sita kwa pointi 37 na sasa imeanza kujitafuta upya kurudi Ligi Kuu.
Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Ally Nnunduma alisema kushuka daraja si kuumia tu kukosa furaha bali hata kiuchumi wametikisika kwa kuingia hasara ya Sh1 bilioni kwa mwaka.
Amesema katika kurejesha upya heshima na hadhi ya City, tayari wapo ukingoni kufunga usajili baada ya wachezaji 22 kumalizana nao kati ya 26 wanaohitajika na kwamba mkakati ni kurejea Ligi Kuu.
“Huku siyo sehemu ya kudumu kwa Mbeya City, tunatangaza rasmi 2024/25 ndio mwisho wetu kucheza Championship, mkakati upo wa makusudi ndani na nje ya uwanja kufikia lengo hili,” alisema Nnunduma.
Kigogo huyo alisema kuanzia Agosti 1 wataanza kutembelea matawi yote ya timu, huku Agosti 17 wakitambulisha jezi mpya na kadi za wanachama akieleza kuwa siku tatu baadaye wataenda kushiriki mashindano huko Zambia.
Alisema kuwa wanahitaji kuingia kambini mapema ili kutoa nafasi kwa benchi la ufundi kutengeneza timu itakayoweza kufikia malengo na kwamba uongozi umejipanga kimkakati.
“Kujua bajeti ya msimu tuliache, ila uongozi utasimamia kila kitu na kwa wakati, tunahitaji timu iende kwenye hadhi yake, huku siyo kwetu, tunaendelea na mazungumzo na wadhamini wawili muda wowote tutaweka wazi,” alisema bosi huyo.