Dar es Salaam. Baada ya mabadiliko ya sheria ya madini yaliyofanyika mwaka 2017, Serikali ya Tanzania imedhamiria kufanya mabadiliko mengine ili kuimarisha udhibiti wa matendo maovu katika sekta hiyo, ukiwemo utoroshaji madini.
Dhamira ya mabadiliko hayo ni kuhakikisha vitendo vya utoroshaji madini na vito vilivyokithiri katika migodi mbalimbali nchini vinadhibitiwa.
Akizungumzia hayo hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema pamoja na mambo mengine, sheria hiyo inatarajiwa kumpa waziri mamlaka ya kuamua gharama za kodi na kwa kuanzia itakuwa asilimia 20 kwa kila anayezalisha madini.
“Kufanya hivi kutasaidia kutatua changamoto zilizopo kwenye masuala ya uchimbaji madini ambapo kuna kipengele kinawataka wachimbaji na wafanyabiashara kufuata taratibu za kisheria, lakini hawafanyi hivyo kwa madai ya utitiri wa kodi,” amesema.
Amesema Tanzania haipo tayari kuruhusu madini yake yatakatishwe katika mataifa mengine, akidokeza kufanya hivyo kunaiondolea nchi sifa yake.
“Kutokana na uaminifu ambao Tanzania imejiwekea, ni ngumu kutumia njia zisizofaa. Hivyo kutumia njia wanazotumia wengine ni kujiondolea sifa ya uaminifu ambayo tumejiwekea kimataifa,” amesema.
Mratibu Mkuu wa Miradi SwissAid, Alice Swai, amesema usafirishaji wa dhahabu usio na mfumo rasmi ndiyo chanzo cha kukosekana kwa taarifa za wachimbaji wadogo.
Kwa mujibu wa Swai, taarifa hizo hazijahusishwa katika ulinganisho wa taarifa za Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), hivyo kuondolewa kwenye taarifa za kila mwaka za fedha.
“Kukosekana kwa taarifa za wachimbaji wadogo kumepelekea kuwepo na mianya ya kuruhusu usafirishaji wa dhahabu kwa mfumo usio rasmi,” amesema Alice.
Amesema kuna haja ya makubaliano ya nchi zinazopokea na kufanya biashara za madini kama uchakataji ili kuwa na mfumo wa pamoja kwa ajili ya kufuatilia taarifa za ugani katika mnyonyoro wa biashara ya kuuza na kununua madini.
“Kuna haja ya kupunguza mlolongo na kurahisisha mfumo wa kusafirisha madini nje ya nchi na kupunguza matamko, ili kukabiliana na usafirishwaji wa vipande vidogo vidogo kwa mtu binafsi kwa njia ya mabegi na ndege,” amesema.
Kwa mujibu wa Swai, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inapaswa itoe bei ya ushindani ili kuhamasisha wafanyabiashara licha ya kuwepo kwa muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2024, unaopunguza mrahaba kutoka asilimia sita hadi asilimia mbili na msamaha wa kibali cha kodi kwa asilimia moja.