Dar es Salaam. Idadi ya sokwe katika Hifadhi ya Taifa Gombe imetajwa kupungua kutoka 150 hadi 85, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo milipuko ya magonjwa na shughuli za kibinadamu zinazofanyika kwenye hifadhi hiyo.
Kuelekea siku ya Sokwe duniani inayoadhimishwa Julai 14, kila mwaka, watafiti kutoka Taasisi ya Dk Jane Goodall (JDI) wameshauri kulindwa kwa mnyama huyo adimu duniani.
Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha JDI, Dk Deus Mjungu amebainisha hayo Julai 12, 2024 jijini Dar es Salaam alipotembelea Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).
Amesema wamefanya utafiti kuhusu tabia na maisha ya sokwe waliopo hifadhi ya Gombe kwa miaka 65 na kwamba eneo hilo ni miongoni mwa makazi machache yaliyosalia ya sokwe mtu duniani.
Ameeleza kuwa wakati anaanza kufanya utafiti hifadhi hiyo ilikuwa na sokwe kati ya 120 hadi 150 na kwamba hadi sasa idadi yao imepungua, kwa sababu ya magonjwa ya njia ya hewa wanayoyapata kutokana na mwingiliano wao na binadamu.
“Kuna magonjwa mengine ya mlipuko na ya asili ambayo hutokana na mwingiliano kati yao na binadamu na husambaa kwa njia ya hewa,” amesema Dk Mjungu.
Ameongeza kuwa kwa miaka hiyo, msitu huo ulikuwa na uwezo wa kuwapatia sokwe chakula cha kutosha, hivyo hawakuwa wanaenda nje ya hifadhi lakini kutokana na shughuli mbalimbali za binadamu, huwafanya sokwe kwenda nje ya hifadhi hiyo kutafuta chakula.
“Tunashirikiana na serikali za vijiji kwa ajili ya kuongeza uhamasishaji wa kutunza hifadhi hii lakini pia kuwepo kwa ushoroba wa msitu kutoka Kaskazini hadi Kusini mwa hifadhi hii ambayo ni karibu na Burundi, kutasaidia sokwe kuwa na uwezo wa kubadilishana vinasaba na sokwe wengine waliokaribu na hifadhi,” ameeleza.
Pia, amesema mbinu hiyo itawezesha kuwa na aina mbalimbali za sokwe na kutokana na utofauti wa maumbile, utazuia sokwe wote kufa.
“Tulinde hifadhi hii kwa kupunguza shughuli za kibinadamu, hii italeta faida kwa wanyama wengine lakini pia itawezesha kizazi kijacho kushuhudia sokwe,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Dk Goodall amesema JGI inashirikiana na serikali za mitaa kushughulikia matishio ya uhifadhi kwa kutumia sayansi na teknolojia, sambamba na kutoa elimu kuhusu usimamizi wa maliasili na mazingira.
Mtafiti huyo amesema kadri idadi ya binadamu inavyoongezeka na misitu inapungua, hivyo idadi kubwa ya sokwe hugawanyika na kupunguza utofauti wa kigeni na uwezekano wa kuishi kwa muda mrefu kwa kila jamii.
“Taasisi ya Jane Goodall inaamini kwamba njia bora ya kulinda makazi yenye afya ni kuzingatia vitendo ambavyo sio tu vinalinda wanyama walio hatarini na makazi yao, lakini pia kunufaisha watu wa eneo hilo ambao maisha yao yanategemea mazingira bora,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu amesema utafiti huo wa sokwe ni wa muda mrefu tangu ulipoanzishwa na mtafiti mwandamizi na mwanzilishi wake, Dk Goodall ambaye amefikisha umri wa miaka 90 sasa.
“Leo nimetembelewa na watafiti kutoka hifadhi ya Gombe wanaofanya utafiti wa sokwe. Utafiti huu ni mkubwa na wa muda mrefu ambao umetoa matokeo ambayo yamebadili taswira ya uhusiano wa binadamu na wanyama kwa dunia nzima,” amesema Dk Nungu.
Amesema utafiti wa sokwe ni miongoni mwa tafiti mbalimbali ambazo wanazitolea vibali na hata kuzifadhili moja kwa moja.
“Dk Goodall na timu yake wamekuja kushukuru sababu mtafiti huyu amefikisha miaka 90 ya kuzaliwa lakini pia anashukuru Costech kwa kutoa vibali vya utafiti nasi tumekuwa tukiangalia wanavyoendelea na tumeona matokea ya utafiti wao umeleta uhusiano kati ya binadamu na wanyama,” amesisitiza.