Katika toleo lililopita tuliangazia jinsi migogoro ya ardhi inavyoongezeka kutokana na mkanganyiko wa sheria na mianya katika usimamizi wa ardhi, huku wataalamu wakipendekeza marekebisho ya sheria na elimu ya kisheria kwa wananchi ili kupunguza migogoro hiyo. Endelea..
Kuvunjika kwa ndoa ni miongoni mwa changamoto inayotajwa kuchochea wanawake kukosa haki ya kumiliki ardhi nchini, hususani katika Mkoa wa Pwani.
Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa Mwaka 2024, kilichotolewa na Wizara ya Fedha kinaonyesha ndoa zilipungua kwa asilimia 10.89 mwaka 2023, huku talaka zilizosajiliwa zikiongezeka kwa asilimia 93.7 ikilinganishwa na mwaka 2022.
Mbali ya hayo, takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 zinaonyesha talaka zimeongezeka kutoka asilimia 0.9 mwaka 2012 hadi asilimia 3.7.
Farida Matagisa, mkazi wa Kijiji cha Njia Nne, wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani, ni miongoni mwa wanawake waliofikwa na kadhia hiyo katika umiliki wa ardhi baada ya kuachana na mumewe.
Akizungumza na Mwananchi, Farida amesema baada ya kuachana na mumewe aliyeishi naye kwa miaka 10, alipata shida kupewa ardhi waliyonunua wakiwa pamoja.
“Niliolewa kata jirani katika Kijiji cha Mtungani, Kata ya Msonga (Wilaya ya Mkuranga). Baada ya kuolewa, pamoja na mume wangu tulinunua mashamba matatu; shamba la mikorosho, minazi na la vyakula,” amesimulia.
“Baada ya kuishi naye kwa miaka 10 aliniacha na kunipa talaka, tatizo likaanzia hapo kwa sababu tulinunua mali pamoja, ikiwamo ardhi ilikuwa ngumu kukubali tugawane,” amesema.
Farida amesema mvutano ulikuwa mkubwa katika kugawana mashamba hayo, mume wake akikataa jambo hilo lisiende mahakamani akisema hakuoa huko.
“Katika kugawana mali changamoto ikaanza hapo, kwa sababu alinipa shamba moja ambalo liko porini sana nikaona litaniwia ugumu kuliendeleza, yale mashamba ya karibu akawa hataki kunipa.
“Ikabidi kuwe na ubishi, baada ya kesi kwenda mabaraza ya dini akakubali kunigawia mawili kwa kugawana,” anasema.
Kwa sasa Farida ni Katibu wa Taasisi ya Hakiardhi katika Wilaya ya Mkuranga akijihusisha na uchechemuzi wa migogoro ya ardhi kwenye jamii inayomzunguka.
Simulizi ya Farida, inafanana na ya Mariam Ndeche, mkazi wa Minaki, wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani, anayesema alilazimika kulala nyumba moja na mume wake baada ya kuachana ili alinde mali, ikiwamo ardhi.
“Tabia za kuachwa na kuondoka bila kugawana mali ni kawaida huku kwetu, lakini sikukubali hilo, nililazimika kukaa nyumba moja ila vyumba tofauti na aliyekuwa mume wangu ili tu nipate haki yangu.
“Alinioa 2018, mwaka 2020 aliniacha tukiwa tumenunua kiwanja ambacho tulijenga, sasa baada ya kunipa talaka akaniambia niondoke. Nilikataa, nilihama chumba tu tukawa tunaishi nyumba moja,” anasimulia Mariam.
Amesema baada ya kuvutana kwa muda mrefu walikubaliana wauze eneo hilo wagawane hela na kila mtu aendelee na maisha yake, hapo ndipo muafaka ulipopatikana.
“Alipokubali kuuza nyumba, tuligawana hela mimi nikarudi nyumbani pamoja na mtoto mmoja tuliyempata,” amesema.
Simulizi hizo zinaungwa mkono na Ripoti ya Takwimu za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi Matokeo Muhimu iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inayoonyesha idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi kuwa ndogo.
“Takriban theluthi moja (asilimia 32.5) ya watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi nchini Tanzania wanamiliki ardhi kwa matumizi tofauti, yakiwemo kilimo, makazi, biashara au viwanda. Kati yao wanawake ni asilimia 29.2 huku wanaume wakiwa wakiongoza kwa asilimia 36.2,” imeeleza ripoti hiyo.
Akizungumzia changamoto wanayopitia wanawake katika kumiliki ardhi, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amesema vitendo hivyo ni unyanyasaji na ili kuviondoa, Serikali imekuja na mkakati wa kumiliki hati pamoja kwa wanandoa.
“Sheria ya umilikishwaji wa ardhi ipo wazi, hakuna sehemu inayotaja jinsia katika kumilikisha ardhi na kwa sasa tunahimiza wanandoa kuwa na hati miliki ya pamoja katika kumiliki ardhi, ili kuondoa yale mambo ya mmoja akifariki mwingine kunyanyaswa au wakiachana,” amesema.
“Lakini hili la mwanamke kutopewa ardhi baada ya mume wake kufariki au namna yoyote ni unyanyasaji tu, kwa sasa tunatatua tatizo hilo kwa utoaji wa hati ya pamoja,” amesema.
Pinda amesema mpango wa hati ya pamoja umeleta matokeo chanya na kuna mwitikio mkubwa kwa familia kusajili ardhi kwa majina ya mume na mke.
“Tangu tuingie katika mpango huu wa umiliki wa pamoja wa ardhi kati ya mume na mke, mwitikio ni mkubwa. Mfano maeneo ya vijijini takribani familia 500 zimeshapata hati hii. Sijajua Pwani chanzo hasa, ila hapo ni mfumo dume,” amesema.
Mtaalamu wa Sheria za Ardhi, Japhet Kasuka ametaja mila kandamizi na mfumo dume kuchangia wanawake kuminywa katika umiliki wa ardhi.
“Kuna mila kandamizi ya wanawake kwenye umiliki wa ardhi kwa sababu makabila mengi yanaamini mwanamke hana haki ya kumiliki ardhi, pia jamii yetu bado ipo kwenye mfumo dume kuhusu fikra kuwa mwanamke hawezi,” amesema.
Ili kuondoa changamoto ya umiliki wa ardhi kwa wanawake, hasa baada ya ndoa kuvunjika, Farida anapendekeza: “Mtu akishachuma na mumewe hiyo ibaki kuwa mali yake pia, siyo mtu akiachika anyimwe mali alizochuma pamoja na mtu wake.”
Akizungumzia nafasi ya wanawake kumiliki ardhi, Askofu Msaidizi mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini amesema mara nyingi suala hilo linaendeshwa kwa kuzingatia utamaduni wa eneo husika, japo Kanisa linaweka nguvu kuhakikisha usawa unakuwepo.
“Mpaka sasa mara nyingi mgawanyo wa mali, ikiwamo ardhi unazingatia utamaduni wa eneo husika, mara nyingi ikitokea ndoa imevunjika tunaangalia watoto,” anasema.
“Katika ukristo hatutamani talaka itokee, lakini ikifikia huko na mwanamke akiwa hana mtoto, hapo ndipo sheria ya nchi itafuatwa. Kwa sasa Kanisa linaweka nguvu katika watoto wa kike kugawiwa mali katika mazingira hayo,” anasema.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka akizungumzia haki ya mwanamke kugawiwa mali baada ya ndoa kuvunjika, amesema mali iliyochumwa pamoja inapaswa kugawanywa sawa.
“Kwenye Uislamu kuna kitu kinaitwa ushirika, ni ile mali ilichumwa na mwanamume na mwanamke kwa pamoja, endapo wakiachana dini inasema wagawane nusu kwa nusu.
“Na inapotokea mmoja amefariki dunia, mali igawanywe kati kisha baada ya hapo suala la urithi linafuatwa,” amesema.
Sheikh Mataka amesema kama mali hiyo imechumwa na mwanamume pekee akiwa ndani ya ndoa, ikitokea wameachana anatakiwa ampe mwanamke kiliwazo, ambacho ni kitu chochote alichojaliwa.
Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.
Makala hii imeandikwa kwa udhamini wa Bill & Melinda Gates Foundation