Dar es Salaam. Waumini wa Kanisa Tanzania Assemblies Of God (TAG) wameadhimisha miaka 85 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo, huku wakisisitizwa kulinda amani na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu.
Ibada ya maadhimisho hayo imefanyika leo Jumapili, Julai 14, 2024 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini hapa, ikihudhuriwa na maelfu ya waumini kutoka mataifa 11 akiwamo Rais mstaafu wa Benin, Thomas Boni Yayi.
Akizungumza katika ibada hiyo, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, amewasisitiza waumini na Watanzania wote waliofikia umri wa kupiga kura, kujitokeza kushiriki hatua hiyo muda ukifika.
Amesema, Julai 20 watakapozindua uboreshaji wa daftari la mpiga kura, watu wajitokeze kujiandikisha na kuboresha taarifa zao.
“Jambo muhimu ambalo ni haki yenu, mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kila Mtanzania anayo haki kuchagua au kugombea, tutakapozindua maboresho ya daftari la mpiga kura Julai 20, kila mmoja aende kuhakiki jina lake.
“Waliobadili makazi pia waende kuhamisha taarifa zao na kila Mtanzania ajiweke tayari kwa uchaguzi na wenye sifa za kugombea wakagombee,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu pia aligusia umuhimu wa amani na kuwasisitiza waumini hao na Watanzania kuendelea kuilinda.
“Sote tunafahamu umuhimu wa amani tuendelee kuliombea Taifa, tumuombee Rais wa nchi yetu,” amesema Waziri Mkuu wakati akitoa salamu za Rais akieleza amemuagiza kumwakilisha kwa kuwa yeye (Rais) ana majukumu mengine ya kitaifa.
Majaliwa pia amelipongeza kanisa hilo kwa kufanya waumini kuwa wamoja, pia kusapoti juhudi za Serikali katika elimu na afya.
“Serikali inatambua michango ya taasisi za dini katika jamii na kuchochea maendeleo ikiwamo TAG, pia tunawategemea katika kuimarisha maadili na umoja.”
“Nchi zetu za Afrika zinapata athari ya kuiga utamaduni wa nje, makanisa yameendelea kukemea na kama Serikali tunawategemea katika kampeni hii ya maadili kwa kuendelea kutumia mahubiri yenu kuijenga jamii,”amesema.
Awali, Askofu Mkuu wa makanisa ya TAG, Mchungaji Barnabas Mtokambali aliipongeza Serikali katika sekta ya usafirishaji, akielezea namna ambavyo treni ya umeme imekuwa mkombozi.
“Tangu nikiwa Askofu msaidizi hadi nilipokuwa Askofu Mkuu nilikuwa nasafiri na mabasi wakati mwingine hadi napanda malori kutoka Morogoro ninapoishi kuja Dar es Salaam au kwenda Dodoma, ilipoanza treni ya umeme, imeleta unafuu sana, haya ni maendeleo,” amesema.
Ibada hiyo ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wakiwamo maaskofu wakuu kutoka nchi mbalimbali, baadhi ya wabunge na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Akitoa taarifa ya kanisa Katibu Mkuu wa TAG, Mchungaji Joseph Marwa amesema tangu kuanzishwa mwaka 1939, limefanya mambo mbalimbali ya maendeleo.
Amesema, Askofu Mkuu Mtokambali, ameiongoza TAG ilipokuwa na mikoa 10 ya kikanisa hadi sasa.
Amesema tangu wakati huo, TAG imetoa huduma za kijamii katika sekta ya elimu kwenye shule za msingi 17 za sekondari saba na za chekechea 117 na inaendelea na ujenzi wa shule nyingine nane.
“Kanisa pia lina vyuo vya ualimu viwili, linatoa huduma za zahanati na vituo vya afya na vingine vinaendelea kujengwa ili kuihudumia jamii,” amesema.
Ibada hiyo ilianza saa 11 Alfajiri kwa waumini kutoka maeneo mbalimbali kuanza kuwasili hadi saa 1 asubuhi ilipozinduliwa na iliyofikia tamati saa 8:41 mchana.