Usafiri wa boti Bagamoyo – Zanzibar wanukia

Bagamoyo. Huenda changamoto ya usafiri kwa wakazi wa Bagamoyo, Chalinze, Kibaha na mikoa ya jirani kulazimika kupitia Dar es Salaam pale wanapotaka kwenda visiwani Zanzibar, ikafikia ukomo hivi karibuni.

Kufikia ukomo huko kunatokana na uwepo wa maandalizi ya ujenzi wa gati litakalotumika katika safari hizo kwenye bandari ya Bagamoyo.

Akizungumza na Mwananchi jana Julai 12, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Shauri Selenda, amesema kutakuwa na boti za kisasa zitakazowasafirisha wakazi pamoja na watalii.

Selenda alitoa kauli hiyo wakati akizindua mradi wa utunzwaji na uendelezwaji wa rasilimali za bahari wilayani Bagamoyo ulioandaliwa na kuratibiwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilayani Bagamoyo (Bangonet)

Alisema kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi,  inaendelea kuchakata suala hilo huku tathmini na upimaji wa uwezo wa gati hiyo ni miongoni mwa maandalizi ya awali yaliyofanyika hadi sasa.

“Maandalizi ya awali tayari yameshafanyika ikiwemo ya kimazingira ingawa wizara haijaweka rasmi tarehe ya utekelezaji wa ujenzi huo,  lakini utaanza hivi karibuni. Hii itafungua utalii kwani watu watakuwa hawalazimiki kwenda hadi feri jijini Dar es Salaam watakuwa wanapitia hukuhuku Bagamoyo,” amesema.

Amesema gati hiyo wamelifuatilia kwa muda mrefu kupitia Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), ili litakapokamilika liweze kuwaondolea adha iliyopo hivi sasa ya kwenda hadi Dar es Salaam.

“Kwetu sisi ni fursa kubwa kwetu na wakazi wa Bagamoyo kwa utalii na maendeleo kupitia biashara na hoteli zitakazojengwa,” amesema.

Diwani wa Kata ya Dunda ambayo bandari hiyo inapatikana, Amir Mpwimbwi amesema walitoa pendekezo la namna gati hiyo itakavyokuwa ambapo itakua na sehemu tatu.

“Sehemu ya kwanza eneo la mizigo, pili eneo la uvuvi na   tatu eneo la usafirishaji wa abiria. Kutakuwa na mita 500 za kina na 400 za eneo zima la gati hiyo,” amesema Mpwimbwi.

Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, amesema suala lililopo ni kuimarisha huduma na kutengeneza mazingira bora kwa abiria.

“Bandari kujengwa ni kwa ajili ya kuhudumia watu,  ni kweli tunaendelea kuimarisha iliyopo sasa hivi ili kuhudumia abiria na mizigo,” amesema Mbossa.

Akizungumzia kuhusu mradi wa Bangonet wa utunzwaji na uendelezwaji wa rasilimali za bahari wilayani humo Selenda alisema jukumu lililopo ni kuhakikisha bahari inatunzwa kwa lengo la kuwanufaisha wakazi.

Mratibu wa mradi huo, Leonard Bankuwia amesema lengo kuu ni kujenga uwezo wa jamii za wakazi wa maeneo ya ukanda wa pwani ya Bagamoyo katika kutunza, kusimamia na kuendeleza rasilimali za bahari sambamba na kuongeza vipato kwa Taifa.

“Katika kufanikisha mradi huu, tutaandaa mchakato wa kuwepo kwa sheria ndogondogo za utunzwaji,  usimamizi na uendelezwaji wa rasilimali za bahari kupitia halmashauri ya Bagamoyo na Chalinze. Bangonet kwa kushirikiana na halmashauri hizo tutaandaa mkakati wa miaka mitano wa utunzaji,  usimamizi na uendelezaji wa rasilimali bahari,” ameeleza.

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.

Related Posts