Utata polisi ikimsaka anayedaiwa kupotea Dar

Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam likitangaza kufuatilia taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya kupotea Adinani Hussein Mbezi (32), mkewe Pendo Simon anadai anashikiliwa na jeshi hilo.

Kwa mujibu wa taarifa za mitandao ya kijamii, Adinani maarufu Adam, mkazi wa Kinyerezi, Mtaa wa Faru alipotea Septemba 12, 2023 alipokuwa safarini Mwanza.

Taarifa zinadai Adinani alikamatwa na polisi kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam inakodaiwa alikuwa akihamishwa kwenye vituo mbalimbali vya polisi.

Taarifa hizo zinadai wakati Adinani akikakamatwa, ndugu walikuwa wakipigiwa simu na wanaodaiwa kuwa askari polisi kwa namba tofauti na kuombwa watume fedha kupitia namba za simu mbalimbali ili ndugu yao aachiwe huru lakini mpaka sasa hawajamuona ndugu yao na baadaye simu hizo zikawa hazipatikani.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa juzi Julai 13, 2024 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro imekanusha maelezo hayo.

“Ukweli wa tukio hili ni kwamba, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamtafuta mtu huyo anayejulikana kwa jina la Adinani Hussein Mbezi @Adam na wenzake kwa tuhuma za kuteka watu hasa wafanyabishara wakubwa,” inaeleza taarifa hiyo.

“Wakati wakitenda makosa hayo walikuwa wakijitambulisha kama maofisa wa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Polisi au Usamala wa Taifa,” imeeleza taarifa ya Polisi.

Kamanda Muliro amesema Septemba 11, 2023 walimteka mtu mmoja mwenye asili ya Kihindi aliyejulikana kwa jina la Maaz Mohamed (27) mkazi wa Upanga saa 5.05 asubuhi maeneo ya Barabara ya Bibi Titi, wakamnyang’anya Sh357 milioni na Dola 38,000 za Marekani (zaidi ya Sh101.54 milioni).

“Walimuachia baada ya kupora pesa hizo kwa sharti la baadaye kuwamalizia kiasi cha pesa Sh100 milioni vinginevyo watapoteza maisha yake,” inaeleza taarifa ya Kamanda Muliro.

Amesema baada ya polisi kupata taarifa Septemba 12, 2023 saa 8.00 mchana waliwekewa mtego maeneo ya Daraja la Tanzanite walipotaka kumteka tena mfanyabiashara huyohuyo na walipotaka kukamatwa walikurupuka na gari lenye namba T 146 DPY ambalo baadaye walilitelekeza eneo la Muhimbili wakakimbia.

“Gari lilivutwa na polisi na kuwekwa Kituo cha Polisi Selander Bridge kama sehemu ya kielelezo cha tukio hilo la kumteka mfanyabiashara huyo,” inaeleza taarifa.

“Watuhumiwa hao bado wanatafutwa na si kweli kwamba walikamatwa Mwanza na kuletwa Dar es Salaam na kuzungushwa kwenye vituo vinavyotajwa, na taarifa hiyo iliyotolewa siyo ya kweli,” amesema Kamanda Muliro.

“Namba hizo za simu zilizotajwa yaelekea zilitumiwa na matapeli, wakawatapeli pesa wahusika na ndiyo maana baada ya utapeli hawakupatikana tena,” inaeleza taarifa hiyo. 

Akizungumza na Mwananchi juzi, Pendo Simon aliyejitambulisha kuwa mke wa Adinani amesema mume wake alipotea tangu Septemba 12, 2023.

Amedai kuwa, siku aliyoondoka alimwambia kuna askari wanayefahamiana anakwenda kuonana naye.

Pendo amedai kuwa, baada ya mume wake kupotea, alikwenda kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam akiwa na ndugu za mume wake (anawataja) ambako alikutana na ofisa wa ngazi za juu (anamtaja) aliyesema wanamfahamu mume wake kwa kuwa huwa anawauzia viatu na amekuwa na ushirikiano na askari wao.

Amedai kuwa, ofisa huyo aliwaambia wanamtafuta Adinani na baadhi ya askari kwa sababu kuna tukio walilomfanyia mfanyabiashara mmoja maeneo ya Kariakoo.

“Nikaomba kukutana na huyo mfanyabiashara, lakini alikataa akisema bado wanafanya uchunguzi,” amedai Pendo.

“Alisema walimwekea mtego lakini alikimbia. Nikawauliza, mbona gari lake limepigwa risasi na limetelekezwa katika Kituo cha Polisi Selander Bridge? Yule ofisa wa polisi akasema katika harakati za kujibizana risasi walifanikiwa kukamata gari lake,” anadai.

Pendo amedai kuwa, alikataa taarifa za ofisa huyo, akisema kuna askari aliyekuwa rafiki wa mume wake aliwahi kufika nyumbani kwao na kuomba ufunguo wa gari na alimpatia.

“Kwa sababu kabla mume wangu hajapotea, aliwahi kurudi nyumbani akasema gari limepata pancha ameliacha Muhimbili, hivyo nikipata nafasi nikalichukue,” amedai Pendo.

Baada ya mazungumzo na ofisa huyo anadai aliwapatia ofisa upelelezi.

Amedai kuwa, tangu wakati huo hajawahi kumwona tena mume wake, ila kuna wakati alikuwa akimpigia simu akitaka atumiwe fedha za kuwapa polisi waliomkamata.

“Ilikuwa Novemba 16, 2023 mume wangu alinipigia simu na kuniambia amekamatwa na alipokata simu namba ile haikuwahi kupatikana tena,” amedai Pendo.

“Baada ya wiki akanipigia kwa namba ngeni akasema amekamatwa na polisi mkoani Mwanza anapelekwa Kituo cha Polisi Tazara, Dar es Salaam,” amedai Pendo.

“Akasema huyo askari aliyenaye anahitaji Sh500,000. Nilikuwa na hiyo hela nikamtumia, akasema baadaye atanijulisha nini kinaendelea.”

Amesema kwa kuwa alikuwa na mtoto mchanga hakuweza kwenda Kituo cha Polisi Tazara usiku huo, bali alikwenda kesho yake.

“Tulipokwenda pale kituoni tukaambiwa hakuna mtu kama huyo,” amesema Pendo.

Amesema baada ya wiki moja, kuna simu ilipigwa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni polisi wa kituo cha Mburahati akieleza yuko na mume wake wanamshikilia.

“Akasema inabidi nitume pesa ili maaskari wagawane waache kumtesa. Nikauliza kwani ana kesi gani? Akasema hayo si muhimu bali utume pesa,” amedai.

Pendo amedai, “Akanipa nikaongea na mume wangu, nikamtambua ni yeye, lakini akasema hawezi kuongea sana kwani ana maumivu, ila niwatumie Sh1.5 milioni kwenye hela zangu za dukani atanirudishia akitoka.”

Baada ya kutuma fedha, anadai namba ile ikawa haipatikani tena.

Wiki moja baadaye anadai alipigiwa simu na ndugu wa mume wake, akitaka wajadiliane kuhusu kupotea kwa mumewe.

“Akatoka nyumbani kwake akaja Kinyerezi, tukajadiliana suala hilo. Akasema ana rafiki yake ambaye ni kamishna wa Wizara ya Mambo ya Ndani (alimtaja jina).

“Akampigia huyo kamishna ambaye alisema licha ya kuwa mbali anaweza kusaidia. Akasema atamtuma kijana wake, lakini tumpe Sh10 milioni ili akasaidie kukamilisha jambo hilo, kwani bila hela itakuwa ni ngumu, tutampoteza,” amedai.

“Kutokana na hofu tuliyokuwa nayo, nikamwambia (ndugu wa mume) mimi kwenye akaunti nina Sh5 milioni naye akasema ataongezea Sh5 milioni,” alidai.

“Basi yule kijana alifika na gari aina ya Toyota Land Cruiser V8, akasema ameagizwa na bosi wake Sh10 milioni. Nikamwambia tupande gari lake hadi Benki ya NBC Segerea nikampatie,” amedai.

Amedai kuwa, baada ya kumpatia kijana huyo fedha hizo, huyo kamishna alimpigia simu na kumtoa wasiwasi akisema mume wake atakuwa salama, akieleza ameshaanza kupiga simu kwa vongozi kujua kuna shida gani.

Baada ya wiki mbili bila mafanikio, anadai kamishna huyo alipiga tena simu akieleza katika ufuatiliaji amepiga simu Kituo cha Polisi Tazara wakamwambia hakuna mtu kama huyo, japo kuna mtu alikamatwa anaitwa Adinan lakini si mume wake.

Amedai kuwa, kuanzia hapo wakawa hawatoi tena fedha kila wanapopigiwa simu na wakaanza kufuatilia kwenye vituo vya polisi.

“Ilipofika Machi 2024, nikaenda kwa yule mpelelezi kufuatilia. Mpelelezi akasema ameomba mawasiliano ya simu katika kampuni (jina linahifadhiwa) kwa sababu anaitafuta namba ya mwisho ya Adinani aliyoitumia na sasa haipatikani,” amedai.

“Kuna ofisa mmoja pale Central (kituo kikuu cha polisi) namfahamu, akaniambia shemeji unahangaika bure, huyo mtu yupo mikononi mwa polisi na walimkabidhi kwa maofisa usalama wamempeleka Tanga,” amedai.

“Akasema ni kweli walimzungusha kwenye vituo vya polisi na walimpiga sana na pesa walizotokanazo kwenye hilo tukio walimnyang’anya,” amedai.

“Huyo ofisa alisema baada ya tukio la kujibizana risasi, Adinani alitoroka akasafiri kwenda Mwanza. Kwa sababu alikuwa na urafiki na maofisa wa polisi, alimpigia simu askari mmoja akamtumia Sh2 milioni akimwomba amtolee gari lake,” amedai.

“Kumbe yule askari naye alimwekea mtego, hivyo akawajulisha maofisa wenzake, kweli akalitoa lile gari na kusafiri nalo hadi Mwanza na alipofika kule akampigia Adinani ili aende akalichukue na hapo ndipo alipokamatwa na kuletwa Dar es Salaam,” amedai.

Related Posts