Unguja. Baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuingia makubaliano na kampuni ya kuendesha Bandari ya Malindi, imeanika mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miezi tisa.
Katika mafanikio hayo, asilimia 16 ni ongezeko la ushushaji wa mizigo na mapato kwa asilimia 17.
Septemba 18, 2023, SMZ kupitia Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), iliingia makubaliano na kampuni ya Ufaransa ya AGL chini ya kampuni yake tanzu ya ZMT kuendesha Bandari ya Malindi.
Sababu ya kuingia makubaliano hayo ni kuondoa malalamiko, usumbufu na msongamano kwenye bandari hiyo ambayo ilionekana kuzidiwa huku uwezo wa Serikali kuiendesha ukiwa mdogo.
Licha ya kujitokeza changamoto kadhaa siku za awali za uendeshaji huo mpya, imeelezwa mafanikio ambayo yameanza kupatikana yanatazamiwa kuleta ufanisi zaidi siku za usoni.
Miongoni mwa changamoto zilizojitokeza mara tu baada ya mwendeshaji huyo kukabidhiwa bandari, ilikuwa ni malalamiko ya kuongezeka tozo, kodi na mfumo wa ushushaji wa mizigo kuwa mibovu.
Serikali yenyewe ilikiri malalamiko yaliyoelezwa na wadau wa bandari yalikuwa na mashiko na kubainisha udhaifu uliokuwapo awali.
Ilifafanua kuwa kilichodaiwa kama kuongezeka kwa kodi hakikuwa sahihi, kwa kuwa mwendeshaji huyo hakuiongeza, bali alifuata taratibu za kisheria ambazo wakati bandari hiyo inaendeshwa na ZPC zilikuwa hazifuatwi, licha ya kutambulika katika Sheria ya Uendeshaji wa Bandari ya mwaka 2018.
Kuhusu madai ya mwekezaji kutokuwa na vifaa, Waziri wa Ujenzi, Masiwasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Muhamed amesema vifaa vinanunuliwa kwa mujibu wa mahitaji na kwa wakati unaostahili, hivyo katika hali ya dharura, mwekezaji ameleta mtambo mpya wa kushusha, kupakia na kuondosha makontena katika eneo la bandari.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Dk Khalid amesema kabla ya mwendeshaji huyo kuanza kazi, zilikuwa zinashushwa wastani wa tani 237.5 kwa siku, lakini kwa sasa wanashusha wastani wa tani 275, sawa na ongezeko la asilimia 16.
Amesema katika mikataba walijiwekea viashiria vya kumpima mwendeshaji na kuwa kabla ya mwendeshaji huyo kufika zilikuwa zikitia nanga meli saba, kwa sasa ni meli kati ya tisa na 11.
Kipimo cha pili, muda wa kukaa kwenye gati, zamani meli ilipokuwa ikipata ukuta kushusha, inakaa zaidi ya siku nane lakini kwa sasa meli inakaa kwenye ukuta saa 41 sawa na siku mbili.
“Hiki ndicho kilikuwa kinatakiwa na Serikali na ufanisi huu unaleta tija kwenye uchumi wa nchi. Ni jambo la msingi na muhimu, kwa sasa wafanyabiashara wameanza kuleta mizigo mingi kwani haigandi (haichelewi) tena bandarini,” amesema.
ZMT imechukua wafanyakazi 392 waliokuwa wafanyakazi wa Shirika la Bandari na kutengeneza ajira mpya 40 na kutoa mafunzo kwa wafanyakzi hao na hivyo kuongeza ufanisi na usalama katika bandari.
Moja ya masharti aliyopewa mwendeshaji huyo katika mkataba, ni kuongeza eneo la kuhifadhi makontena, na alipewa hekta mbili katika eneo la Maruhubi ambalo alilijenga.
Waziri Khalid alisema, kati ya hekta hizo, tayari hekta moja imeshatengenezwa takribani asilimia 50 ya kazi yote.
Ikifika Agosti mwaka huu, bandari kavu katika eneo hilo itakuwa imekamilika kwa asilimia 100 na likikamilika msongamano utakuwa umeisha katika Bandari ya Malindi.
“Haya yote yamepatikana, tumempata mwendeshaji huyu tunashirikiana naye, kupitia mikataba hiyo shughuli zinakwenda,” amesema.
Amesema kwa hesabu mapato ya shirika yameongezeka kwa asilimia 17 kwa kipindi cha miezi tisa tangu mwendeshaji mpya aingie.
“Mapato ya jumla ya Serikali ni Sh13.6 bilioni, sasa ukiziangalia kwa hesabu, walipokuwa wanaendesha wenyewe ZPC walikuwa wanakusanya Sh30 bilioni lakini wakati huohuo walikuwa wakitumia Sh18 bilioni (miezi tisa),” amesema.
Kwahiyo SMZ ilikuwa inabaki na Sh12 bilioni, kwa sasa gharama zimeamia upande wa ZMT.
Dk Khalid amesema katika kipindi cha miezi tisa kuanzia Septemba 18, 2033 hadi Mei 2024 mgawo wa Serikali wa asilimia 30, ni Sh10.035 bilioni.
ZMT anachukua asilimia 70 ambayo ni sawa na Sh33.453 bilioni na gharama zote za uendeshaji wakiwemo wafanyakazi analipa yeye.
“Imani yetu ni kwamba ikikamilika bandari kavu Agosti, mapato yataongezeka zaidi ya hapo, kwa hiyo uamuzi uliofanywa na Serikali ni sahihi na wenye tija,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Khalid, katika utafiti ambao haukuwa rasmi zilikuwa zinapotea Dola za marekani 13 milioni katika bandari hiyo, lakini hilo jambo kwa sasa limeanza kupungua.
Hata hivyo, Serikali inaendelea na mchakato wa kujenga Bandari jumuishi ya Mangapwani, iwapo ikikamilika bandari ya Malindi itabaki kuwa ya utalii na shuguli zote za mizigo zitahamia Mangapwani.
Bandari ya Mangapwani inayojengwa inatakiwa angalau ianzie makontena 260,000 kwa mwaka lakini mategemeo yake ni kuchukua makontena 800,000 kwa muda huo.
Bandari ya Mangapwani ambayo imeshaanza kupokea hifadhi ya mafuta, imejengwa kwenye eneo la kilometa 12 za bandari. Serikali imetenga Sh160 bilioni katika bajeti ya mwaka 2024/25 kuanza ujenzi huo.
Wakati shughuli za mizigo zikihamia Mangapwani, bandari ya abiria itakuwa Mpigaduri na tayari wameshasaini mkataba na kampuni ya Devco kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo.
Katika kuimarisha shughuli za usafirishaji kuna pia Bandari ya Fumba yenye uwezo wa kuchukua makontena kati ya 80,000 hadi 90,000.
Bandari ya Malindi ilijengwa mwaka 1920 kipindi hicho Zanzibar ikiwa na watu 120,000 kwa sasa idadi ya watu kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 ni milioni 1.8
Wakizungumza kuhusu hali hiyo, baadhi ya wadau wa bandari wameeleza tija kuanza kuonekana licha ya kudai bado kuna changamoto ambazo zinahitaji kushughulikiwa.
Ahmed Bombani, mfanyabiashara katika bandari hiyo amesema wanaona mabadiliko katika kushusha na kupandisha mizigo kwenye bandari hiyo, lakini kuna changamoto katika malipo ambayo mchakato wake unakuwa mrefu.
“Ufanisi upo ikilinganishwa na awali alipoanza kuendesha bandari hii, kasoro ndogondogo hazikosekani lakini kuna tofauti ilivyokuwa awali na sasa,” amesema.
Haji Khamis mbeba mizigo katika bandari hiyo amesema kuna utofauti mkubwa awali na sasa kwani hata masuala ya usalama yanazingatiwa kwa kiasi kikubwa.
“Huwezi kuingia ndani kwa sasa bila mavazi maalumu, kitambulisho mwanzoni tuliona kama usumbufu lakini kadri tunavyoendelea tunaona umuhimu wake,” amesema.
Amesema wamedhibiti, na watu wanaingia kwa utaratibu maalumu huku masuala ya udanganyifu yakiondolewa na usalama kumarika zaidi.
Akizungumza kuhusu athari za mizigo kukaa muda mrefu bandarini, Juma Abdulla Khamis, mtaalamu wa masuala ya uchumi, amesema mizigo ikikaa muda mrefu si hasara kwa wafanyabiashara pekee, bali ni hasara kwa taifa na pengo ndani ya uchumi.
Amesema hali hiyo inaongeza bei ya vitu, huduma zinazorota na wanachi wanapata shida kwani yapo mahitaji ya vitu ambayo bei zake zitapanda mara dufu.
“Mapato yasitazamwe tu pale bandarini, lakini yaangaliwe faida katika mnyororo mzima wa uchumi, mizigo ikikaa pale hasara inayopatikana ni kubwa kuongezeka kwa vitu, bei na huduma unakuwa mzigo mkubwa ndani ya uchumi,” amesema.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.